Wasiwasi bado mkubwa Dar es Salaam
22 Disemba, 2011 - Saa 14:46 GMT
Hali ya wasi wasi bado
inazingira maeneo ya mabondeni katika jiji la Dar Es Salaam kutokana na
mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kusababisha vifo vya watu wasiopungua
20 na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa (Tanzania
Meteorological Agency) imeonya kuwa mvua hizo nzito zitaendelea kunyesha
na imeshauri watu wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama haraka.Baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi ni kama Jangwani, Kigogo, Mburahati na Bonde la Mto Msimbazi ambalo linamwaga maji katika bahari ya Hindi.
Kutokana na kiasi kikubwa cha maji kuingia baharini, hata maji katika Bahari ya Hindi yamebadilika rangi na kuwa ya maji machafu ya mafuriko.
Kuna maelfu ya watu wanaoishi katika maeneo ya mabondeni ambao mpaka sasa makazi yao yamebomolewa na wamekuwa wakihifadhiwa katika vituo vya dharura.
Kamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova
"Tulikwenda kuwaokoa baadhi yao na waligoma kuhama wakisema hawawezi kuondoka kwa kuwa wanachunga mali zao"
Mmoja wa waathirika ni Tabu Kibwa aliyeieleza BBC kuwa nyumba yake yote imezingirwa na kumezwa na maji.
"Tumepoteza kila kitu, kwa kweli tumebaki mikono mitupu. Kila kitu katika nyumba kimepotea ikiwa ni pamoja na televisheni na majokofu," aliileza BBC.
Hata hivyo wengi wa wakazi hao wamegoma kuhama kwa miaka mingi licha ya kufahamishwa hatari ya mafuriko.
Kwa mujibu wa Idara ya hali ya hewa, hizi ni mvua nzito zaidi kuwahi kunyesha Dar Es Salaam tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961.
Kamanda wa polisi wa mkoa maalum wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, amewasihi watu kuhama mabondeni, lakini amekiri baadhi yao wamegoma kabisa.
"Tulikwenda kuwaokoa baadhi yao na waligoma kuhama wakisema hawawezi kuondoka kwa kuwa wanachunga mali zao,” alisema.
Ingawa mvua zimeonekana kusababisha maafa makubwa zaidi Dar Es Salaam, lakini zimekuwa zikinyesha kwa nguvu katika maeneo mengi kama Iringa na Rukwa ambako madaraja na barabara vimebomolewa.
No comments:
Post a Comment