Saturday, December 31, 2011

Hitimisho bila utafiti ni uvivu wa kufikiri II- MAKALA

Hitimisho bila utafiti ni uvivu wa kufikiri II

Maadui hawaitakii mema CHADEMA
Kama tulivyoahidi, wiki hii tunaendelea na sehemu ya mwisho ya makala ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, akimjibu mmoja wa wachangiaji hoja na waibuaji mijadala katika gazeti hili, Mayage s. Mayage.
Mayage angelifanya utafiti angeligundua hoja ya Katiba mpya ilikuwa ndani ya Ilani ya CHADEMA. CCM imeibeba baada ya kushinda uchaguzi kama walishinda na siyo ‘kuiba kura’ (Katiba hairuhusu kuhoji matokeo hivyo hatuna pa kutolea ushahidi wetu). Sisi hatuna shida na hilo.
Tunasisitiza kama wamechukua hoja ambayo hawakuwa nayo waitekeleze vizuri kama ilivyobuniwa na walioibuni. CHADEMA ndiyo iliyoibuni, na kusema...ndani ya siku 100 mchakato wa Katiba mpya utaanza” Hakuna chama kingine chochote kilichosema hivyo kwenye ilani yake.
Ni dhahiri Mayage haelewi, kuwa ‘Mchakato ukiwa mbovu, tunda lake yaani Katiba itakayopatikana itakuwa mbovu’. Wengine tuna uzoefu si wa kusoma tu magazetini bali kushiriki mchakato wa Tume ya Rais ya Jaji Kisanga. Ni hovyo. Ndiyo maana tangu siku ya kwanza nimepinga Tume ya Rais badala ya Tume ya Wananchi itakayoundwa na mkutano wa Katiba.
Mayage haelewi kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa Katiba na kuwa haki haitapatikana kama Katiba itaendelea kubeba Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ni ndoto kufikiria uchaguzi huru na haki 2015 kama Katiba Mpya haitapatikana. Matukio yote ya wananchi kupigwa mabomu, kuzuiliwa mikutano ya upinzani mara kwa mara, kubadilishwa kwa matokeo ya uchaguzi yote haya ni matokeo ya Katiba mbovu.
Mayage hajui kuwa migogoro mingi kwenye ardhi ni matokeo ya Katiba mbovu! Hajui kuwa robo tatu ya bajeti ya taifa leo inatumika kwenye uendeshaji wa Serikali badala ya mipango ya maendeleo kutokana na Katiba mbovu? Mayage siyo tu hajafanya utafiti, lakini pia si makini katika kujenga hoja zake. Anajipinga mwenyewe mara aseme chama gani kimesimamia hoja zake, mara aseme CHADEMA kinapoteza muda kujadili hoja zenye manufaa kwa Watanzania. Tumuamini kwa lipi katika hali hii?
Mayage sisi tuliisha kumaliza utafiti na udadisi kuhusu Katiba.  Huhitaji kwenda mbali, nenda Ghana na Kenya. Tunayo michakato iliyotumika kupata Katiba na tunazo pia nakala za Katiba zao.
Nani kapotea kati yako wewe ambaye huna hata mfano mmoja na CHADEMA inayofahamu tangu awali nini kinahitajika kupata Katiba mpya!
Tuache ulimbukeni tunapozungumzia maslahi ya taifa. Mayage anaenda mbali kiasi cha kufananisha CHADEMA na “bundi katika msafara wa ndege dhaifu”! Kama yeye alijisikia kutukanwa je, na CHADEMA ambaye si mtu mmoja inajisikiaje na upotoshwaji na matusi ya kiasi hiki?
Ukisoma kwa umakini, kwake Mayage CHADEMA ni “chama cha ovyo” ndiyo maana anawashawishi Watanzania kuanzisha chama mbadala wa CCM.
Mayage amelundika vyama vyote 17 vya upinzani katika kapu moja. Ni kweli kuwa hafahamu CHADEMA ni chama pekee cha upinzani kinachoongoza halmashauri zaidi ya saba? Hajui kuwa CHADEMA imeshindwa kwa idadi ndogo sana katika halmashauri nyingine nane?
Mayage ameshindwa kutambua kuwa CHADEMA ni chama kinachokua kimkakati na vigezo ni vingi chukua idadi ya madiwani ambayo katika uchaguzi wa 2010 imeongeza kwa asilimia zaidi ya 400, mafanikio ambayo hakuna hata chama chochote cha upinzani kimefikia?
Mayage hajui kuwa katika vyama 17 viko ambavyo tangu vianzishwe havijawahi kupata kiongozi hata serikali moja ya mitaa angalau mwenyekiti wa kitongoji, wakati CHADEMA ina maelfu ya viongozi hao?, Mayage ameamua kuzipuuza makusudi kwa malengo anayojua na pia kwa ‘uvivu wa kutokufanya utafiti’ angalau kupiga simu tu kwa wahusika. Madhara yake ni kuwaambia watanzania “..tulivyonavyo sasa (vyama vya siasa/NGO’s). Hivi haoni hata aibu kulinganisha chama kinachoongoza halmashauri zikiwemo Jiji la Mwanza na NGO ambayo malengo yao si kuchukua dola?
Haya siyo matusi tu kwa Watanzania bali kwake mwenyewe aliyejifanya mtaalamu akashindwa kufikisha ujumbe ambao pengine hata mtoto wa shule ya msingi angeliweza kuufikisha vizuri zaidi.
Wanachama,wapenzi na Watanzania wapenda mabadiliko ambao walikuwa hawajagundua dhamira ya Mayage kuanzia makala ya kwanza ni vema wakarudi kusoma makala zake za mwanzo na kuzichambua kwa kina ili kuepuka upotosha uliojificha kwa hoja za kuuma na kupuliza.
Dk. Slaa nisingeliweza kwa namna yoyote kufumbia macho upotoshwaji huu ambao nia na lengo lake ni dhahiri.
Mayage anaonyesha udhaifu mkubwa pale anaposema hajaridhishwa na CHADEMA kwa kushindwa kusimamia hoja moja tu “…ya posho ya vikao kwa wabunge”. Kwani CHADEMA ndiyo inayolipa posho hiyo?
Hajui mgogoro wa sasa wa posho kulipwa kinyemela na jinsi CHADEMA kama chama inavyopiga kelele, hajui jinsi CHADEMA ilivyodai fomu ya mahudhurio ukumbini bungeni itenganishwe na fomu ya posho, na uongozi wa Bunge umekataa kufanya hivyo?
Labda hajui msimamo wa CHADEMA kwa kuwa si mpenda kusoma wala hajui ilani ya CHADEMA kifungu cha 5.5.1 (2 na 6) ya Agosti  2010, kinasema nini.
Lakini sishangai kwa vile anaandika kwa hisia badala ya utafiti. Kama ambavyo hajui pia kuwa kamati kuu ya CHADEMA kila kikao kwa mujibu wa kanuni, inatakiwa kupokea utekelezaji wa programu ya kazi kutoka kwa wabunge na  halmashauri zinazoongozwa na CHADEMA na kila kamati tendaji ya kata inapokea taarifa ya utekelezaji kutoka kwa madiwani wake.
Inawezekana utekelezaji wa mipango katika maeneo yanayoongozwa na CHADEMA unasua sua na kwa maeneo mengine hauridhishi.
Lakini pia angetafiti kidogo angegundua halmashauri zenye uzoefu za CHADEMA zimepiga hatua kiasi cha kuanzisha chuo chake cha waalimu kupunguza kero ya upungufu wa waalimu, kuanzisha chuo cha madaktari (clinical officers) na manesi kupunguza kero ya upungufu wa wataalamu hao na sasa wako mbioni kuanzisha chuo cha kilimo.
Haya yanapatikana tu kwa wenye nia na dhamira ya dhati ya kutaka kujua bila kutoa hukumu mezani. 
RC Mwanza, ma-DC wametuhujumu
Angelifanya utafiti angeligundua jinsi mkuu wa mkoa wa Mwanza alivyoingilia na kuvuruga utekelezaji wa mipango ya Jiji la Mwanza iliyoko chini ya CHADEMA, na vivyo hivyo kwa wakuu wilaya katika halmashauri zingine.
Utafiti ungelimwonyesha kuwa demokrasia kwa wengi wa viongozi wa Serikali iko kwenye midomo zaidi (lip service) lakini yanayoendelea maeneo mengi nchini ni kinyume cha demokrasia. Haya hutayajua kama huna dhamira ya kutaka kuyajua na wala hufanyi utafiti. Ndiyo msingi mkubwa wa ushauri wangu kwa Mayage.
Ni dhahiri Mayage angelifanya utafiti angeligundua maandamano yalivyowaunganisha Watanzania kudai siyo tu haki zao mbalimbali, bali kupaza sauti yao dhidi ya makali ya maisha kama vile sukari, bei ya sembe, mafuta ya kupikia, mafuta ya taa pamoja na kuwakatalia watawala kodi yao isitumike kulipa madeni ya Dowans..
CCM wameiga hawakufanikiwa
Anachokiita Mayage uanaharakati, angelijikita kwenye utafiti angeligundua matokeo yake ni nini hadi CCM wenyewe waliokuwa wakikandia maandamano wakaamua kuyaiga walipojaribu kuandamana Mbeya japo hayakufanikiwa.
Ni dhahiri Mayage amejikita kwenye mbinu mgando akidhani namna pekee ya kufanya siasa ni kufungua matawi kwa mtindo wa CCM.
Kwa kuwa hajafanya utafiti anashindwa kugundua kuwa mbinu za CCM za kufungua matawi haziwezi kufuatwa na chama kingine chochote makini kwa kuwa CCM inatumia mfumo wa dola kufanya kazi zake-watendaji wa vijiji, kata, makatibu tarafa, wakuu wa mikoa, wilaya, kwa ujumla mfumo mzima wa Serikali.
Polisi wanaingilia mipango yetu
Angetafiti angeligundua hata matawi niliyofungua au kufanya yafunguliwe kutokana na ziara ya Katibu Mkuu Jimbo la Mbinga Magharibi (Mbamba Bay), bendera zote zimeshushwa kwa amri ya OCD.
Angelikuwa mtafiti angeligundua chama makini kama CHADEMA kinakumbana na matatizo na vikwazo gani. Angelitoa ushauri jinsi ya kupambana na changamoto hizo nisingelikuwa na sababu ya kumjibu Mayage na au ningemjibu kwa kumpongeza.
Ushauri wake ungetokana na utafiti nina hakika ungewasaidia sana kuwafungua macho Watanzania badala ya kuwapotosha.
Kauli ya Mayage kuwa ‘..Ndani ya siasa wako wanasiasa wazuri tu, lakini hao hawana sauti wala nafasi ya kukielekeza  chama hicho…wenye sauti na ushawishi ndani ya chama ni wanaharakati hali inayokifanya chama kiendeshwe kiharakati kwa asilimia 80..” inathibitisha siyo tu Mayage hajafanya utafiti, lakini pia hajui ‘ABC’ ya siasa na hivyo hastahili kuandikia hata mada za kisiasa.
Chama cha siasa hakiendeshwi kwa ‘influence’, au uanaharakati kama anavyodai Mayage bali na Katiba, kanuni na taratibu za ndani ya chama husika kama zipo.
Kwa faida ya wapenzi wa CHADEMA na Watanzania kwa ujumla CHADEMA inaendeshwa misingi ya Katiba yake, na toleo la mwisho ni la mwaka 2006. CHADEMA ni kati ya vyama vichache vyenye kanuni za uendeshaji, maadili ya viongozi na wanachama, kanuni za uendeshaji wa halmashauri zinazoongozwa na na  CHADEMA ikiwa ni pamoja na serikali za mitaa zilizoko chini ya CHADEMA na hatimaye kanuni za nidhamu ikiwa ni pamoja na kanuni za nidhamu za wabunge, madiwani, na wenyeviti wa serikali za mitaa (na wajumbe wao).
Uamuzi wa CHADEMA hufanywa kupitia Sekretariati ya Kamati Kuu ya chama, Kamati Kuu, Baraza Kuu na mkutano mkuu ambacho ndicho chombo kikuu na cha mwisho cha uamuzi.
Je, ni kuwadi wa maadui zetu?
Kwamba CHADEMA inaendeshwa na wenye ‘influence’ ni kielelezo cha kile nilichokisema kuwa kauli kama hizo zinatoka tu kwa watu wenye uvivu wa kufikiri na kufanya utafiti.
Vinginevyo Mayage ana ajenda yake ambayo hajaiweka hadharani na au ni kuwadi tu wa maadui wengi wa CHADEMA.
Kama nia yake ni njema kama anavyotaka kuonyesha na kuwa anatoa ushauri kwa nia njema, huwezi kumshauri mtu usiyemfahamu, na huwezi kumfahamu mtu kama angalau humtembelei, kumjulia hali, kuomba nyaraka zake na kadhalika.
Wakati ninawapokea waandishi wengi na wa vyombo takriban vyote ofisini kwangu Mayage hajakanyaga wala hajaomba taarifa yoyote iwe kwa simu iwe kwa mahojiano. Huu ni uthibitisho kuwa Mayage ana ajenda zake anazozijua.
Kwa taratibu hizi uanaharakati na “influence” inapata wapi nafasi? Au Mayage anataka kufanya kazi kwa mapenzi ya mtu mmoja mmoja mathalan hiyo asilimia 20 anayoisema?
Je, ni kweli kuwa hiyo influence imepenya kwenye ngazi zote kuanzia sekretariati, kamati kuu, baraza kuu hadi mkutano mkuu. Kama hivyo ndivyo si ndivyo pia jina letu linavyodhihirisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo?
Au Mayage anataka tukiuke misingi ya demokrasia na asilimia 80 ya viongozi waongozwe na asilimia 20? Huo ni ulimbukeni katika siasa na itakuwa ni mfumo mpya unaobuniwa na Mayage katika chama chake kipya anachosema kitakuwa makini”.
Wapenzi na Watanzania kwa ujumla hakuna sababu ya kuwa na hofu na watu wa aina hii, na kwa taarifa yenu wako wengi wasiotutakia mema.
Naamini ufafanuzi huu wa kina utakuwa umewatoa wote hofu wale waliokuwa na shaka baada ya kusoma makala za Mayage.
Naomba nirudie tena katika hitimisho, sina tatizo na wale wote wenye nia ya kuanzisha chama kingine kipya akiwemo Mayage kama nilivyosema ni haki yao ya kikatiba.
Kwa wale ambao tumekwisha kuanza safari ya kuing’oa CCM kupitia ‘meli yetu’ ya CHADEMA, tuendelee na mikakati yetu na kila mmoja akitimiza wajibu wake, Novemba 2015 CCM itaingia kwenye kumbukumbu ya historia kama ilivyo UNIP (Zambia) na KANU (Kenya), tena vyote ni vyama vinavyojulikana kama vyama vya ukombozi.
Mwalimu aliwahi kusema “play your part, it can be done” kila kiongozi wa CHADEMA kwenye ngazi na nafasi yake atimize wajibu wake na apuuze propaganda za maadui zetu zikiwemo hizi za Mayage.

No comments:

Post a Comment