Mashtaka mapya watuhumiwa CCM | Send to a friend |
Friday, 02 December 2011 21:24 |
0digg
NI WANAOTAJWA KWA UFISADI,TUME YA MAADILI YAZUA HOFUMwandishi Wetu MASHTAKA mapya yanaandaliwa dhidi ya makada wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya chama hicho, kabla ya kufikishwa mbele ya Tume ya Maadili, kujibu tuhuma zinazowakabilia, Mwananchi limebaini.Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa kazi ya kukusanya ushahidi dhidi ya watuhumiwa hao ilianza mara baada ya kumalizika kwa vikao vya juu vya CCM, ambavyo ni Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC). Kwa mujibu wa habari hizo, kuundwa kwa Tume ya Udhibiti wa Nidhamu na Maadili ya CCM ambayo imepewa nguvu za kutoa uamuzi bila kulazimika kusubiri NEC na CC ni sehemu ya mchakato wa kuanza kuchukua hatua dhidi ya makada waliogoma kujivua gamba, huku wakiwa wanatuhumiwa kwa vitendo kadhaa vya ufisadi. Katika vikao vyake vya juu vilivyomalizika Novemba 24 mwaka huu mjini Dodoma, CCM kiliamua kwamba, suala la kujivua gamba lirejeshwe chini ya Kamati Kuu ambayo kupitia kamati za maadili katika ngazi zote, watuhumiwa wote wa ufisadi na wale watakaobainika kukiuka maadili ya chama hicho, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Taarifa kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa tuhuma zinazoweza kuwakabili makada hao, ni pamoja na kuendesha siasa za makundi zinazowagawa wanachama wa CCM, kutumia njia chafu kwa ajili ya kuusaka urais wa 2015, kuwatukana viongozi wakuu wa chama hicho na kukusanya kundi la viongozi wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) mjini Dodoma kwa lengo la kuvuruga vikao vya juu vya chama hicho. Mwananchi lilidokezwa kuwa, wakati watuhumiwa wa ufisadi watakapofikishwa mbele ya kamati za maadili na Tume ya Maadili kwa wale wa kitaifa, hawatashtakiwa kwa makosa yanayotajwa sasa pekee, bali pia makosa mengine mengi waliyofanya katika harakati za kujinasua katika tuhuma zinazowakabili. “Sikiliza nikwambie, hata kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa UVCCM wa mikoa hapa Dodoma ni moja ya mashtaka ambayo yameandaliwa dhidi ya watuhumiwa, maana waliowapa fedha wanafahamika na ushahidi wote upo kwa hiyo, waliokesha wakisherehekea pengine niseme hawajui ‘politics’ (siasa),”alidokeza mmoja wa viongozi wa CCM. Makosa ambayo yamewahi kutajwa hadharani na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara) Kapteni John Chiligati ni pamoja na ufisadi wa ununuzi wa rada, kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond na kashfa ya wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje kupitia Benki Kuu ya Tanzania, EPA hususan Kampuni ya Kagoda iliyokwapua kiasi cha Sh40 bilioni. Mitizamo ya kimakundi Kurejeshwa kwa suala la kujivua gamba kwa watuhumiwa wa ufisadi ndani ya CC kulipokewa kwa mitizamo tofauti na makundi yanayokinzana ndani ya CCM. Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mukama alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa NEC alisema: “Takribani miezi saba (7) baada ya azimio hilo kupitishwa, bado hatujapata mwitikio wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi yoyote wa chama chetu ambao ni walengwa wa azimio.” Aliongeza: “Bila shaka sasa wakati umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika, lakini, utekelezaji wake hauna budi ufanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa ndani na kanuni za CCM za uongozi na maadili.’’ Hata hivyo, kundi linalopinga utekelezaji wa falsafa hiyo ndani ya CCM lilikesha likisherehekea kile lilichokiita, ‘ushindi wa awali’ kwamba hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani makada katika ngazi ya Taifa wanaotuhumiwa kwa ufisadi, iwapo watafikishwa kwenye kamati za maadili. Mmoja wa makada ambaye ni mtetezi wa watuhumiwa hao, alisema baada ya kikao cha NEC kuwa: “Hapo hakuna kesi tena, mfano wanaposema mtu anatuhumiwa kwa suala la Richmond au Rada, watapata wapi ushahidi wa kuthibitisha tuhuma hizo, hii kesi imekwisha naona wameona wameshindwa na hii kampeni ya kujivua gamba imeshindwa kwa sababu ilikuwa ikiwalenga watu fulani tu ndani ya chama.” Hata hivyo, habari mtazamo wake ulikuwa tofauti na mawazo ya makada wengine wawili ambao walisema kuwa kurejeshwa CC kwa suala la kujivua gamba ni hatua ya kupata fursa ya kuwabana zaidi watuhumiwa hao na kwamba zamu hii “hawaponi”. “Hawa jamaa (watuhumiwa) wanaungwa mkono sana NEC, kwa hiyo suala hili kujadiliwa na NEC huenda wangewageuzia kibao wabaya wao, kwa hiyo busara kwamba lirejeshwe CC ni hatua ya kutoa fursa ya kuwatendea haki, wewe tusubiri tu, haponi mtu hapo,”alisema mmoja wa makada hao. Kuli za Katibu Mkuu Kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu Mukama na mabadiliko ya Kamati ya Maadili ya chama hicho ambayo imegeuzwa kuwa Tume ya Udhibiti wa Nidhamu na Maadili, ni miongoni mwa mambo yaliyozua hofu kubwa miongoni mwa makada wa chama hicho. Mikutano miwili ambayo Mukama ameifanya na waandishi wa habari katika muda wa wiki moja, imeshuhudia mtendaji huyo mkuu wa CCM, akitoa kauli zinazoashiria kuwepo kwa mkakati maalumu wa “kuwachukulia hatua kali watovu wa nidhamu na wakiukaji wa maadili ndani ya chama”. Habari ambazo Mwananchi imezipata, zinasema kuwa hatua ya Mukama kuamua kuzungumza mwenyewe kuhusu uamuzi wa chama hicho akiwa mtendaji mkuu wa CCM, una maana kubwa mbili. Kwanza ni kusisitiza udhati wa utekelezaji wa uamuzi wa chama hicho kuwachukua hatua makada wake waliogoma kujivua gamba katika muda wa miezi takribani saba waliyopewa, kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali, hasa za ufisadi. Hatua hiyo pia ni kuwakata makali watu waliokuwa wakimwandama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba ‘alipotosha’ azimio la NEC kuhusu watuhumiwa wa ufisadi ambao walipewa siku za kujitathimini kisha kuchukua hatua za kujivua madaraka waliyonayo kwa faida ya chama chao, CCM. Hasira dhidi ya Nape na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara, Kapteni John Chiligati zilionekana ndani ya kikao cha NEC hasa pale mmoja wa wajumbe kutoka mkoani Arusha, alipohoji sababu za wajumbe hao wawili wa Sekretarieti kuzunguka nchi nzima, wakipigia debe mkakati wa kujivua gamba na kuyaweka kando maazimio mengine 26 ya NEC yaliyopitishwa Aprili mwaka huu. Mjumbe huyo aliotoa hoja hiyo akitanguliwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa ambaye pia aliwashambulia Nape na Chiligati kwamba wamekuwa wakizunguka nchi nzima kwa kutumia fedha za chama, wakimwita yeye fisadi bila kuwa na ushahidi wowote. Hata hivyo, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika mjini Dodoma baada ya kikao cha NEC, Mukama aliwajibu waliotoa tuhuma hizo kwa kusema: “Maazimio yote 26 yaliyopitishwa na NEC ya mwezi Aprili mwaka huu, yamewekewa mpango wa utekelezaji, isipokuwa azimio la 27 ambalo lilikuwa ni la kipekee na hili utekelezaji wake ni tofauti na haya mengine”. Akirejea maagizo ya NEC kuhusu azimio hilo la 27 katika vikao vyake vilivyofanyika kati ya Aprili 10 na 11 mwaka huu, Mukama alisema “Viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama. Wasipofanya hivyo chama kitawawajibisha mara moja.” Wakati umma ukisubiri utekelezaji wa maazimo hayo, Jumanne wiki hii, Mukama alikutana na vyombo vya habari na kuzungumzia kuundwa kwa Tume ya Maadili ya CCM inayochukua nafasi ya Kamati ya Maadili. Tume hiyo ndiyo iliyozusha hofu mpya kwamba sasa hukumu dhidi ya watuhumiwa wa makosa ndani ya CCM haitakuwa ikisubiri NEC wala CC, badala yake itakuwa na mamlaka ya kutoa uamuzi wa mashtaka yote yatakayofikishwa mbele yake. Mukama alisema mipango ya namna tume hiyo itakavyoendesha shughuli zake, imekamilika na kilichobaki ni upatikanaji wa wajumbe wake 14 watakaoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa. Siasa za Makundi Ndani ya vikao vya juu vya CCM, Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, January Makamba aliripotiwa kuwasilisha mada kuhusu hali ya siasa ndani ya chama hicho ambayo ilionya kwamba mgawanyiko uliopo unaweza kukisambaratisha chama hicho siku zijazo. Makamba alinukuliwa akisema, kadri siku zinavyokwenda makundi ndani ya CCM yamekuwa yakipata nguvu na kuonya kuwa ikiwa hali hiyo itaendelea, kuna uwezekano mkubwa wa wanachama wasio na kundi wakashindwa kuendelea na ukada na uanachama wao. Chanzo chetu ndani ya NEC kilidokeza kuwa Makamba katika taarifa yake aliyakosoa makundi yote mawili yanayowindana ndani ya CCM na kusema kwamba siasa hizo zinapaswa kukoma, ili kukiruhusu chama hicho tawala kuisimamia Serikali kwa lengo la kutatua matatizo ya wananchi. Mtoa habari wetu kutoka ndani ya NEC alisema: “Alisema kwa uwazi kabisa, kwamba ipo siku wanachama wapya wakiingia ndani ya chama watatakiwa wajue wanakwenda katika kundi gani, akaonya kuwa hali hiyo siyo nzuri hata kidogo kwa afya ya chama, ni kama alizisema pande zote.” Habari hizo ziliendelea kueleza kuwa miongoni mwa mambo ambayo Makamba aliyaweka bayana kwamba yanahitaji usimamizi, ni pamoja na kupaa kwa bei ya mafuta, kushuka kwa thamani ya shilingi, kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali na tatizo la njaa katika maeneo kadhaa ya nchi. |
No comments:
Post a Comment