Usingizi na jeni zahusiana
5 Disemba, 2011 - Saa 17:03 GMT
Wanasayansi wanasema mahitaji ya usingizi kwa watu yana uhusiano na jeni zao yaani genes.
Wamegundua kuwa watu wenye aina ya jeni iitwayo
ABCC9 wanahitaji takriban dakika thelathini za ziada za usingizi kila
usiku kuliko wale wasiokuwa nayo.Wanasayansi hao wa Ujerumani na Uingereza wamesema matokeo hayo ni muhimu kwasababu ukosefu wa usingizi unahusishwa na matatizo mengi ya kiafya, kama vile maradhi ya unene na moyo.
Viongozi wa kisiasa, kuanzia mtawala wa zamani wa Ufaransa Napoleon hadi aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher walikuwa na sifa ya kuweza kufanya kazi zao bila matatizo licha ya kulala muda wa saa nne au tano tu kila usiku.
Lakini kwa wengine akiwemo mwanafizikia Albert Einstein hata muda wa saa 10 wa usingizi haukumtosha.
Sasa wanasayansi wanasema tofauti hizi katika mahitaji yetu ya usingizi yanaweza kuelezeka kwa kutazama muundo wa jeni zetu.
Walichambua chembe chembe za asidi nasaba DNA kutoka watu 10,000 kote barani Ulaya- na kuzilinganisha na mitindo yao ya kulala.
Walifikia kauli kwamba watu walio na aina ya jeni iitwayo ABCC9 wanahitaji muda wa nusu saa zaidi usingizini ikilinganishwa na wale wasio na aina hiyo ya jeni.
Mtu mmoja kati ya kila watu watano barani Ulaya wanaaminika kuwa na jeni hiyo ya usingizi mwingi.
No comments:
Post a Comment