Friday, December 9, 2011

Katibu wa Bunge la TANZANIA anaficha ukweli kumlinda nani?

Katibu wa Bunge anaficha ukweli kumlinda nani?  Send to a friend
Wednesday, 07 December 2011 20:42
0digg
KATIKA siku za hivi karibuni uongozi wa Bunge la Kumi, chini ya Spika Anne Makinda umekuwa ukitoa kauli zinazokinzana, hasa kuhusu suala la nyongeza ya posho za wabunge.
Hali hiyo ya kushangaza imetokana na kiongozi huyo kuonekana kutokuwa na msimamo wa pamoja kati yake  na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, kiasi cha kuibua maswali mengi miongoni mwa wananchi kuhusu namna Sekretarieti ya Bunge inavyoweza kufanya kazi zake kwa ufanisi katika hali hiyo ya kutofautiana katika kufanya maamuzi ya pamoja.
 
Kama habari tuliyochapisha leo katika ukurasa wa kwanza inavyoonyesha, hali  hiyo imeonekana dhahiri kuwaudhi  wananchi wa rika zote wakihoji inakuwaje kauli za viongozi hao zinakinzana kiasi cha kupotosha ukweli.
Itakumbukwa kuwa, baada ya gazeti hili wiki iliyopita kuchapisha habari za kupanda kwa posho za vikao vya wabunge kutoka Sh70,000  hadi Sh200,000 kwa siku,  wasomi, wanaharakati, wanasiasa na wananchi kwa jumla walipaza sauti zao wakipinga vikali kupandishwa kwa posho hizo.
 
Awali kabla ya habari hizo kuchapishwa na gazeti hili kwa mara ya kwanza Jumapili iliyopita, katibu huyo wa Bunge alikuwa amekataa kuthibitisha ongezeko hilo la posho, akisema hakuwa msemaji wa Bunge.
Lakini baada ya mjadala wa posho kushika kasi katika vyombo vya habari, Dk Kashililah aliibuka na kukanusha kuwapo kwa nyongeza hiyo ya posho, ila akakiri  kwamba wabunge walikuwa wameomba kuongezewa posho za vikao, lakini mapendekezo yao yalikuwa hayajaanza kutekelezwa na Serikali, hivyo posho za vikao zinabakia kuwa Sh70,000 kwa siku na sharti hilo halijafanyiwa marekebisho wala kufutwa na mamlaka husika.
 
Lakini katika hali ya kushangaza, sakata hilo la posho za vikao vya Bunge lilichukua sura mpya juzi baada ya Spika Anne Makinda kutoa kauli iliyopinga kauli ya Katibu wa Bunge na kusema tayari  wabunge walikuwa wameanza kulipwa viwango vipya vya  posho za vikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku, mbali na mshahara wa Sh50,000 za mafuta na Sh80,000 za kujikimu ambazo jumla yake ni Sh330,000 kila siku licha ya mshahara wa Sh2.3 milioni kila mwezi .
Alisema wabunge walianza kulipwa viwango hivyo vipya katika vikao vya Novemba 8, 9 na 11 mwaka huu na wiki ya pili ya Bunge la Mkutano wa Tano.
 
Kiongozi huyo wa Bunge alikiri kuwapo nyongeza hiyo jijini Dar es Salaam na kusema hatua hiyo imechukuliwa ili kuwapunguzia wabunge makali ya maisha kwa kuwa gharama za maisha zimepanda na wabunge hawawezi kuzimudu kutokana na alichokiita malipo kidogo wanayopata.  Alisema hayo muda mfupi baada ya kuzindua Ripoti ya Maendeleo ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2011.
 
Tunaungana na wale wote waliojitokeza siyo tu kupinga  nyongeza hiyo ya posho za vikao vya wabunge bali pia waliolaani kitendo cha Bunge na Serikali kuongeza posho hizo kinyemela na kutoa kauli za kuwapumbaza wananchi ambao kodi zao ndiyo hasa zinazotafunwa na wabunge hao hivi sasa.
Ni vigumu kujua sababu zilizomfanya Spika ashindwe kuingilia kati wakati Katibu wa Bunge alipotoa matangazo katika magazeti yaliyogharimu mamilioni ya fedha na kuwadanganya wananchi hadi alipoingia katika mtego wa waandishi akiwa Dar es Salaam wakati akizindua Ripoti ya Maendeleo ya Wanawake Duniani.
 
Haiwezekani kwamba Katibu wa Bunge alitoa matangazo hayo na kuyalipia mamilioni ya fedha pasipo Spika kuidhinisha na kutoa maelekezo. Vinginevyo, angekuwa tayari ametoa taarifa kwa umma kuonyesha hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa dhidi ya katibu huyo wa Bunge.

Huu ni ushahidi tosha wa njama za wabunge na mawaziri wa Serikali kupeana fedha za walipakodi kienyeji na ndiyo maana wananchi wanasema Katiba Mpya kamwe  isiruhusu mawaziri kuwa wabunge au Rais kuwa sehemu ya Bunge. Vinginevyo wananchi wataendelea kusakamwa na umaskini, huku wachache wakinenepeshwa na mfumo wa chukua chako mapema.

No comments:

Post a Comment