Friday, December 9, 2011

TANZANIA - Miaka 50 ya makosa ya kisiasa yaliyopaswa kuepukwa

Miaka 50 ya makosa ya kisiasa yaliyopaswa kuepukwa  Send to a friend
Friday, 09 December 2011 13:23



 Lawrence Kilimwiko
KATIKA kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika Serikali ya TANU/CCM ilifanya makosa mengi ya kisiasa kiasi kwamba kwa kuyarekebisha imejikuta inarudi kule kule ilikotoka.
Ilianza kwa kuufuta mfumo wa vyama vingi uliokuwa imesimikwa na Katiba ya Uhuru, lakini ukarejeshwa mwaka 1992. Serikali ya TANU ilizifuta serikali za mitaa lakini zikarejeshwa mwaka 1984 baada ya kuutambua umuhimu wake.
 Vyama vya ushirika vilivyokuwa wamejengeka na kuwahudumia wakulima kwa mafanikio  makubwa vilisambaratishwa ili kutoa nafasi kwa bodi za mazao na mashirika mengine. Baada ya bodi hizi kushindwa, ushirika ukarejeshwa ijapokuwa mambo yalikuwa tayari yameharibika.
Mtindo wa kufanya mabadiliko kwa majaribio umeligharimu sana taifa katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru iliyopita. Cha kushangaza ni kwamba mwisho wa siku watanzania wamejikuta pale pale alipowaacha mkoloni mwaka 1961.
Sababu kubwa ya kuboronga huko ni kwamba, mamuzi mengi yalikuwa ya kisiasa zaidi kuliko uhalisia wa mazingira yaliyokuwepo. Makosa haya yaichelewesha sana maendeleo ya watanzania na nchi yao kwa ujumla.
Wakati Tanganyika iliyojinyakulia uhuru wa bendera mwaka 1961, ilikabidhiwa Katiba ya Uhuru ambayo licha ya kuwa na dosari nyingi, ilikuwa imeainisha vizuri sana nafasi ya Bunge kama chombo cha uwakilishi wa watu na nafasi ya vyama vya siasa kama taasisi za kidemokrasia, ilikuwa bayana.
Kasoro kubwa katika Katiba ya Uhuru ilikuwa ni kule kuendelea kumtambua Malkia kama mkuu wa nchi huru. Kwa maneno mengine, Tanganyika ilikuwa huru lakini siyo jamhuri. Hali kadhalika, kulikuwa na mkuu wa Serikali lakini siyo mkuu wa nchi. Katiba ya Uhuru pia haikuwa na vipengele vya haki za binadamu.
Ukiacha dosari hizo ambazo zingeweza kufanyiwa marekebisho, Katiba ya Uhuru ilikuwa imeweka misingi mikuu ya mfumo wa utawala wa kidemokrasia wa kibunge.
Chini ya Katiba ya Uhuru , Bunge ndicho kilikuwa chombo chenye madaraka ya mwisho kuhusu mstakabali wa nchi. Serikali iliongozwa na Waziri Mkuu kutoka chama chenye wabunge wengi kupitia majimbo ya uchaguzi.
Waziri Mkuu aliongoza baraza la mawaziri waliowajibika kwa pamoja au mmoja mmoja Bungeni. Kwa jinsi Bunge lilivyokuwa limepewa meno isingekuwa rahisi kwa Serikali na watendaji wake kuzembea na ikasalimika.
Lakini kwa kutumia kisingizio cha kasoro ya Malkia kuendelea kuwa mkuu wa nchi iliyohuru, uongozi wa TANU badala ya kukifuta kipengele hicho tu, uliamua mwaka 1962 kuandika Katiba mpya kabisa.
Chini ya Katiba ya Jamhuri, vipengele vyote vizuri vilinyofolewa. Kwanza kabisa madaraka ya Bunge yalihamishiwa kwa Rais. Kwa mabadiliko haya, badala ya Serikali na mawaziri kuwajibika kwa Bunge, sasa  mawaziri wakawa wanawajibika kwa Rais.
Badala ya Rais kuwajibika Bungeni kama ilivyokuwa imedhamiriwa awali sasa akapewa mamlaka ya kulivunja Bunge.
Na hiyo kama haitoshi, Rais akarundikiwa madaraka makubwa mno bila udhibiti wo wote. Hilo likawa ni kosa kubwa la kwanza la kisiasa.
Baada ya kuhamisha madaraka ya mwisho kutoka Bungeni kwenda Rais ,Serikali ya TANU ikaamua sasa kuufuta mfumo wa vyama vingi ili TANU itawale bila mpinzani.
Hoja iliyojengwa kuhalalisha mabadiliko hayo makubwa ya kikatiba, ilikuwa ni kwamba TANU ilikuwa inawakilisha wananchi wote kwa kuzingitia ushindi wa kishindo iliyoupata katika chaguzi mbili zilizotangulia.
Ilichokuwa imesahau ni ule ukweli kwamba hata chama kisichokuwa na wafuasi wengi huweza kujijenga pole pole ili hali kile kilicho na wafuasi wengi kinaweza kuporomoka kwa kadri kinavyoshindwa kuwahudumia wafuasi wake.
Faida ya mfumo wa vyama vingi ni kwamba watu wanakuwa na uhuru kubadilisha uongozi kwa kuvishindanisha vyama. Kile kinachoshindwa kinakaa pembeni na kujipanga upya. Hasara ya chama kimoja ni kujisahau na kufanya kazi kwa mazoea tu.
Ni dhahiri laiti vyama vilivyokuwepo wakati ule visingefutwa hali ya kisiasa ingekuwa tofauti kabisa. Hili nalo likawa ni kosa la kisiasa hasa ikichukuliwa kuwa mfumo huo ulikuja kurejeshwa mwaka 1992 baada ya makosa kuwa yametendeka.
Serikali ya TANU pia iliamua kuzifuta serikali za mitaa sambamba na kuufuta utawala wa machifu. Kwa kufuta serikali za mitaa Serikali ya TANU ilijikuta katika wakati mgumu sana wa kutoa huduma za msingi zilizokuwa zikitolewa na serikali hizo.
Haikushangaza kwamba mwaka 1984 , serikali za mitaa zilirejeshwa lakini madhara makubwa yakiwa yamekwisha tokea. Ikumbukwe kuwa chimbuko la serikali za mitaa ni shughuli za hiari zilizokuwa zikifanywa na majirani katika jitihada za kuboresha mazingira na hudumu za msingi kwenye mitaa  na maeneo yao.
Hata Mwalimu Nyerere alipata kukiri baada ya kustaafu kwamba lilikuwa ni kosa kubwa kuzivunja serikali za mitaa na kwamba kama angepewa nafasi ya kurudi madarakani, hilo ni eneo ambalo asingerudia kufanya kosa kamwe.
Kama hiyo haitoshi, Serikali ya TANU ikaviandama vyama vya wafanyakazi vilivyokuwa vinapigania maslahi ya wanachama wake. Serikali pia ikaviandama vyama vya ushirika vilivyokuwa vinatetea maslahi ya wakulima ili wafaidike na kilimo chao.
Vyama vya wafanyakazi vilifutwa na badala ikaundwa jumuiya ya wafanyakazi liyowekwa chini ya mwavuli wa chama tawala. Hali kadhali, vyama vya ushirika navyo vilifutwa na badala yake ukaundwa muungano wa ushirika uliwekwa kama jumuiya ya chama tawala.
Kwa mabadiliko haya, wakulima walikosa mtetezi na huduma za msingi kwani mamlaka za mazao zilizoundwa na serikali, ziligeuka mnyonyaji mwingine wa wakulima.
Kwa upande wa wafanyakazi,  wao waligeuka vibarua wa serikali wasiokuwa na sauti yo yote juu ya jasho lao.
Kuyanyima makundi haya haki ya kutetea maslahi yao lilikuwa ni kosa jingine kubwa la kisiasa.
Mwalimu Nyerere pia alikuja kukiri baada ya kustaafu kwamba ilikuwa ni makosa kuvunja vyama vya ushirika.
Ikumbukwe tu kwamba, mengi ya majengo makubwa na mazuri yaliyojengwa awali huko mikoani yalikuwa yamejengwa na vyama vya ushirika.
Chama cha Ushirika cha KNCU ndiyo kilichojenga jengo la kwanza kutumia lifti mjini Moshi. Ni KNCU iliyojenga Chuo cha Ushirika cha mjini Moshi ambacho kwa sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu ya SUA. Shule ya Lyamungo pia ilijengwa na KNCU. 
Kwa upande, chama kikuu cha Nyanza kilichokuwa kinawahudumia wakulima wa pamba, kilikuwa kimeshamiri hadi kuwa ndicho chama kikubwa cha ushirika kuliko vyama vyote vya ushirika barani Afrika.
Lakini kama kuna kosa ambalo  lilivuka mpaka, lilikuwa ni operesheni vijiji. Hili ni zoezi litakalo kumbukwa kwa muda mrefu kwa vile liligusa maisha ya watu takriban 14 milioni.
Mpango huo ulihusu kuwahamisha kwa nguvu watu kutoka kwenye vijiji vyao vya asili na kuwapeleka kwenye vijiji vya ujamaa. Maelezo yaliyotolewa ilikuwa, ni kuiwezesha serikali kusambaza huduma za kijamii hasa  elimu, maji na afya kwa wote.
Licha kwamba Serikali haikuwa na fedha za kugharamia huduma hizo, bado iliendelea na mpango wake ulioendeshwa kwa ubabe na ukatili mkubwamno.
Watu walibomolewa nyumba zao na kuhamishiwa kwenyemaeneo yaliyokusudiwa hata kama hakukuwa na maandilizi. Watu waliliwa na wanyama poro na kuumwana na nyoka. Akina mama walijifungulia maporini huku mvua ikinyesha bila msaada. Watu walipoteza mifugo na mali nyingine  walizokuwa wamezihangaikia kwa maisha yao yote.
Mwisho wa zoezi ilielezwa kwamba watu takriban million 14 walikuwa wamehamishiwa kwenye vijiji vipatavyo 8,299 kote nchini.
Baada ya hapo ikifuata njaa kwa vile watu walikuwa wamepelekwa mbali na mashamba yao. Mwaka 1974/75 watu wanaponea unga wa mahindi ya njano yaliyotolewa msaada na serikali ya Marekani.
Athari nyingine iliuwa ni kushuka kwa uzalishaji wa mazao yote ya chakula na biashara. Viwanda vya korosho  vilivyokuwa vimejengwa wakati huo vilishindwa kufanya kazi kwa kukosa korosho baada ya wakulima kuhamishwa mbali  na mashamba yao.
Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, huduma zilizokusudiwa kutolewa hazikuwafikia wote kwa vile serikali haikuwa na fedha. Ilitegemea misaada ya wafadhili.
Lengo jingine la kujenga ujamaa pia lilifeli vibaya sana. Hata vile vijiji vilivyoweza kupata mafanikio vilisambaratika kutokana na ubadhirifu uliofanywa na mamlaka za mazao pamoja na ulafi wa viongozi wa kisiasa waliojenga tabia ya kula mali za vijiji bure.
 Kuanzia wakati huo, wakulima wamekabiliwa na ukosefu wa mashamba kutokana na msongamano wa watu katika vijiji vilivyogeuka miji. Hili nao ni kosa la kisiasa.
Makosa mengine ya kisiasa yaliyopaswa kuepukwa na serikali ya chama makini ni pamoja na uuzaji wa nyumba za serikali, ubinafsishaji wa mashirika ya umma pamoja na kuondoa miiko ya uongozi iliyokuwa imeainishwa wakati wa Azmio la Arusha.
Makosa yote haya yamechangia kwa kiasi kikubwa kudumaza maendeleo ya watanzania katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

No comments:

Post a Comment