Friday, December 9, 2011

TANZANIA - Miaka 50 ya Uhuru:Tusonge mbele

Miaka 50 ya Uhuru:Tusonge mbele  Send to a friend
Thursday, 08 December 2011 21:17
0digg
Fredy Azzah na Gedius Rwiza
WATANZANIA leo wanasherehekea miaka 50 ya Uhuru huku wakisifia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho na kutaja changamoto kadhaa zinazopaswa kufanyiwa kazi.Sherehe hizo ni kumbukumbu ya siku ya Uhuru wa Tanganyika uliopatikana kwa njia ya amani Desemba 9, mwaka 1961 kutoka nchi ya Uingereza.Wakizungumzia maadhimisho hayo ya  taifa kufikisha nusu karne kwa nyakati tofauti jana, watu hao wa kada tofauti walisema ingawa nchi imepitia misukosuko mingi, imefanikiwa mambo mengi, ikiwamo kuhakikisha tunu ya uhuru inalindwa.Tanganyika ilikuwa nchi ya kwanza kupata uhuru katika Ukanda wa Afrika Mashariki na ilikuwa Jamhuri mwaka 1962 kisha Aprili 26,1964 ikaungana na Zanzibar na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wasomi
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Ruth Meena, alisema kwa kupindi cha miaka 50 iliyopita Tanzania imepiga hatua kwa kuwa na shule za kutosha, hospitali na  wataalamu wa nyanja mbalimbali.

Alisema pia kumekuwa na mafanikio ya kuridhisha katika uhuru wa kutoa maoni na kupunguza ukandamizaji wa wanawake na watoto.“Lakini, pamoja na hayo, bado tuna changamoto ya kuhakikisha tunapata elimu bora.
 Pia jambo jingine linalonisikitisha ni kuona zaidi ya wanawake 50,000 wanafariki kila wanapokwenda kujifungua, hili linatakiwa liangaliwe kama janga la kitaifa,”alisema Profesa Meena.Kwa mujibu wa Profesa Meena, changamoto nyingine inayolikabili Tanzania ni kuhakikisha vijana wake wanaweza kushindana katika soko la utandawazi.
“Utandawazi ni changamoto tunayotakiwa tuifanyie kazi kwa ukaribu, siku hizi vijana kutoka upande wowote wa dunia wanaweza kuomba kazi mahali popote, hii ni changamoto tunayotakiwa tuitazame kwa vijana wetu, ubora wa elimu wanayopata utawawezesha kushindana?” alihoji Profesa Meena.
Profesa Chris Peter Maina kutoka UDSM, alisema katika eneo ambalo Tanzania imefanikiwa  ni kwenye kudumisha umoja uliokuwapo tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.“Tumekaa pamoja tangu tulipopata uhuru wetu, tumejitahidi kuudumisha, lugha ya Kiswahili pia imefanikiwa kutuunganisha zaidi kama nchi,” alisema Profesa Maina.
Alisema kwamba, changamoto kubwa iliyopo ni kwa Watanzania pamoja na viongozi waliopo kuhakikisha kuwa, umoja wa kitaifa uliopo, unadumishwa kama vile ulivyoachwa na waasisi wa taifa hili.Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala, alisema  katika miaka 50 iliyopita, jambo kubwa linalotakiwa Watanzania wajivunie ni kupata uhuru na kuweza kuulinda kwa kuwa na msimamo wa pekee unaolinda maslahi ya taifa.
“Tumeheshimika kwa hili, tumeweza kujenga utaifa licha ya kuwa na makabila mengi  na dini za kila aina, hata kwa majirani zetu tunatambulika kwa umoja wetu na upendo. Hicho ni kitu kikubwa sana cha kujivunia kwa wakati huu,” alisema Profesa Mukandala.Alifafanua kwamba changamoto kubwa inayotakiwa kufanyiwa kazi ni kuendelea kujenga utaifa na kuhakikisha kila jambo linalouhatarisha linashughulikiwa mapema.
Mama Maria Nyerere
Mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria, alisema awamu ya kwanza ilikuwa ni ya kutafuta uhuru, ndiyo sababu wakati huo muda mwingi ulitumika kwenye ukombozi wa nchi nyingine za Afrika. “Miaka 50 ya uhuru imejaa malalamiko kwamba hatujafanya kazi tuliyotegemea. Lakini tumefanya kazi ya ukombozi kwa nchi za jirani.
Kulikuwa na muungano wa nchi 14 za Afrika ambazo zilihitaji ukombozi,” alisema Mama Nyerere.WanaharakatiMkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia haki za Wazee HelpAge nchini, Smart Daniel, alisema haipendezi kuona nchi inasherehekea miaka 50 ya uhuru huku wazee ambao waliupigania uhuru huo, wakiwa hawana uhakika wa kupata mlo wa siku wala sehemu ya kulala.“Sawa nchi inaadhimisha miaka 50 ya uhuru, lakini wazee waliopigania uhuru huo wametelekezwa,” alisema Daniel.
Edwin Mtei
Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Edwin Mtei, alisema Tanzania imepita safari ndefu yangu ilipopata uhuru mpaka hivi leo ambapo inatimiza miaka 50 ya uhuru wake.
“Nakumbuka mwaka 1978/79 hali ilikuwa mbaya sana kiuchumi, tulikosa fedha za kununua vitu nje, bei ya vyakula ilipanda, tukakosa vitu vingi muhimu,” alisema Mtei.Kwa upande wa mwanasiasa mkongwe nchini, Job Lusinde, alisema katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru, nchi imejitahidi katika kuyafikia malengo yaliyokuwapo wakati wa kupigania uhuru.
“Kulikuwa na lengo la kuinua wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara kwa kuanzisha vyama vya ushirika, kama vile Nuta, Juwata, na vinginevyo,” alisema:Walimu walalamikaKwa upande wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema wakati leo nchi inaadhimisha miaka 50 ya Uhuru mafanikio katika sekta ya elimu bado ni madogo hivyo kuhitajika jitihaza za makusudi kwa ajili ya maboresho.“Hatuwezi kujisifia katika upande wa elimu.
Wakati kuna watu wanaojiita wasomi, elimu inazidi kushuka kwa kisingizio cha kukosa fedha wakati nchi imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi. Kwa hiyo elimu tuliyoipata baada ya uhuru haijatusaidia,” alisema Gratian Mukoba ambaye ni kiongozi wa CWT.
“Tungeweza kujivunia mafanikio ya elimu kama wasomi wetu wangeweza kuibadilisha nchi kupitia rasilimali za nchi, lakini nadhani kila mmoja ni shaidi nchi inapoteza rasilimali zake wakati kuna watu ambao ni viongozi na wanaojiita wasomi sasa nini maana ya elimu yetu?” alihoji Mukoba.Alisema  amesikitishwa na kitendo cha wabunge kuona wao ndio watu muhimu kuliko walimu na kusema kwamba maisha ya Dodoma ni magumu wakati hata walimu nao kuna wanaoishi Dodoma.

No comments:

Post a Comment