Tanzania ‘ombaomba’ wa tatu ulimwenguni! | Send to a friend |
Tuesday, 06 December 2011 20:31 |
0digg
SIYO
siri tena. Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya
tatu duniani kwa kupata misaada kutoka nchi wahisani, ikiwa nyuma ya
nchi zilizogubikwa na vita za Iraq na Afghanistan. Shirika moja la
Marekani lijulikanalo kama ‘Visual Economics’, limechapisha jarida
lenye takwimu za kushtusha zinazoonyesha jinsi misaada ya maendeleo
inavyotolewa duniani. Shirika hilo linaloongoza duniani kwa kufichua takwimu za siri katika masuala ya uchumi na fedha limesema, misaada ya nchi wahisani kwa Tanzania imepaa kutoka Dola za Marekani 39.19 milioni (Sh66 bilioni) mwaka 1961 hadi Dola 2.89 bilioni (Sh3 trilioni) mwaka 2009 na kuifanya nchi hiyo kuwa kinara wa nchi za Afrika zinazopokea misaada kutoka nje na pia kushika nafasi ya tatu duniani ikitanguliwa na Iraq na Afghanistan. Takwimu hizo zimewashtusha wananchi wengi ambao wamehoji kulikoni Tanzania imepokea misaada mingi kiasi hicho tangu ipate uhuru miaka 50 iliyopita lakini imebaki kuwa moja kati ya nchi chache duniani ambazo wananchi wake bado wanaogelea katika umaskini wa kutisha, kiasi cha wengi kuishi chini ya dola moja kwa siku. Wahisani wakubwa wa mipango ya maendeleo kwa Tanzania tangu uhuru ni Sweden, Norway, Marekani, Japan, The Netherlands, Denmark, Uingereza, Umoja wa Ulaya, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF). Inaeleweka kabisa nchi za Iraq na Afghanistan zinapoorodheshwa na shirika hilo la ‘Visual Economics’ kama nchi ombaomba. Hakuna asiyejua kwamba nchi hizo zimekuwa katika vita kwa muda mrefu kiasi cha uchumi wa nchi hizo kuvurugika na watu wengi kuuawa. Katika mazingira ya vita, ambapo umwagaji damu na mauaji ya kujitoa muhanga hutawala, hakuna shughuli zozote za maendeleo zinazoweza kufanyika. Mkombozi pekee wa wananchi katika nchi hizo ni misaada ya nchi wahisani. Lakini kitendawili kikubwa ambacho kimekuwa kigumu kuteguliwa ni juu ya Tanzania kuwa kinara wa nchi ombaomba barani Afrika na kushika nafasi ya tatu duniani, nyuma ya Iraq na Afghanistan. Kinyume na nchi hizo ambazo misaada nyingi inayotolewa ni ya kijeshi, Tanzania imekuwa ikipata misaada ya maendeleo katika nyanja za elimu, miundombinu, afya, maji, ujenzi, kilimo, nishati na usafirishaji, hivyo isingekuwa maskini iwapo misaada hiyo ingetumiwa kama ilivyokusudiwa. Tanzania, mbali na kupata uhuru wake bila kumwaga damu mwaka 1961, nchi hiyo imekuwa kisiwa cha amani na wananchi wake wameishi miaka yote kwa amani na utulivu bila vita ya wenyewe kwa wenyewe. Nchi hii inao utajiri mkubwa na imetunukiwa na mambo mengi ya ajabu. Angalia ardhi kubwa yenye rutuba na rasilimali nyingine nyingi, zikiwamo madini ya kila aina, gesi, mbuga za wanyama, mazao ya biashara, misitu, mito maziwa, fukwe za bahari na wanyama pori. Tafsiri ya takwimu za shirika hilo la ‘Visual Economics’ ni kwamba Tanzania imeshindwa kusonga mbele kimaendeleo kwa sababu ya utegemezi mkubwa wa misaada ya wahisani na matumizi mabaya ya misaada hiyo, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa utawala bora, kama Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2009 ilivyobainisha na kusema asilimia 20 ya bajeti ya Serikali kila mwaka inamezwa na vitendo vya rushwa. Kutokana na changamoto iliyotolewa na shirika hilo, jambo la kufurahisha ni kwamba wananchi sasa wamegundua Tanzania inaweza kusonga mbele kimaendeleo bila misaada ya wafadhili, kwani misaada hiyo imeshindwa kufuta umaskini tangu tupate uhuru. Siyo siri tena kuwa, rasilimali za nchi zimenufaisha kundi dogo la watawala na mawakala wao walio nchini na nje ya nchi. ‘Visual Economics’ limetufumbua macho. Yatupasa tutafakari wapi tunataka kwenda kama taifa ili tujenge uchumi wa kutukwamua katika lindi la umaskini. Misaada ya wahisani haitufai, tuachane nayo sasa. Njia pekee ni kujitegemea, kwani tunazo rasilimali za kutosha. Kinachotakiwa ni utashi wa kufanya hivyo. |
No comments:
Post a Comment