Monday, December 5, 2011

BAHATI BUKUKU SIFAI KUWA MKE


Na Brighton Masalu
MWIMBA Injili mwenye  muonekano wa ‘mama mwenye nyumba’  aliye pia na sauti ya uponyaji, Bahati Lusako Bukuku amefunguka akisema hafai kuwa mke na wala hafikirii kuolewa, paparazi wetu amebugia sentensi zenye ushahidi.

Bukuku aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akianika mwanya mbele ya ‘balozi’  wetu baada ya kumnasa shambani kwake, Bunju A Tegeta, jijini Dar es Salaam.
Alisema miongoni mwa wanawake walioumbwa kwa ajili ya kuishi bila ndoa ni yeye na ndiyo maana alitimka kwa mumewe, Daniel Basila.

Aidha, alisema mwanaume huyo ni jasiri kwa sababu alimvumilia kwa vimbwanga na vituko vingi alivyokuwa akimfanyia ndani ya nyumba.
Staa huyo wa wimbo wa Waraka, alizidi kukwea na mistari kuwa, Basila alidhani amepata mke bora kumbe alikosea uchaguzi jambo alilolifananisha na kuchukua mbavu za mbuzi kuzipeleka kwa tembo!
“Unajua jambo likikushinda huwezi kulazimisha, mimi nilidhani nafaa kuwa mke kumbe si kweli. Kifupi ni kwamba mimi kama Bahati Bukuku, sifai kuwa mke vinginevyo ni kumpa mwanaume stress (mawazo) zisizo na maana,” alitiririka Bukuku.

Pamoja na hayo, Risasi Jumamosi likaendelea kumchimba ili kutoka na ‘kavareji’ iliyoshiba kwa kumhoji kama kwa sasa anafikiria kuingia tena katika ndoa;
Bukuku: Kama nilivyosema hapo awali hutakiwi kulazimisha jambo ambalo huliwezi, mimi suala la ndoa jamani siliwezi.
Risasi Jumamosi: Kwa hiyo ni kama una nuksi?
Bukuku: Hapana, siamini katika hilo, wala sijutii maana ni mipango ya Mola.
Risasi Jumamosi: Wewe ni mtumishi wa Mungu, kwake hakuna kinachoshindikana, sasa kwa nini usimuombe  akubadilishe na kukupa mume bora na mwema?

Bukuku: (akilikazia macho gazeti hili) mume bora nilipewa lakini yeye aliangukia kwa wrong person (mtu ambaye siye). Sasa labda kuna ambaye amempanga yeye, lakini nadhani nitaishi peke yangu hadi mwisho.

Risasi Jumamosi: Sasa jamii inakuchukuliaje? Kwani mwonekano na huduma unayoitoa unastahili kuwa na mume, maana wakati mwingine utahitajika kutoa ushauri kwa wanandoa ikiwa kama mtumishi.

Bukuku: (Kwa macho ya aibu) Duh! Labda husomi vizuri Biblia, maana ndoa inaruhusiwa kuvunjika na mimi niliwahi kuolewa na hata jamii inajua hilo. Ukweli ni kwamba siwezi kumhudumia mume ipasavyo.
Risasi Jumamosi: (likiongeza umakini zaidi) kwa nini?

Bukuku: Mfano, mume anakwambia mwende beach (ufukweni) na mimi nabeba khanga na gauni refu au wakati mwingine nakaa chumbani na mume wangu nikiwa nimevaa kimama zaidi, si nitamkera? Kifupi siwezi kuishi na mwanaume hasa kwa sasa, maana  kama ni ng’ombe, ameshazeeka.

Bahati Bukuku aliwahi kuolewa na Daniel Basila na kufanikiwa kupata mtoto mmoja ambaye alifariki dunia mwaka 2006.

Views: 1924
Tags: risasi11

No comments:

Post a Comment