Friday, December 9, 2011

Uhuru miaka 50 sasa tutafakari tulipotoka, tulipo, tuendako


 Send to a friend
Thursday, 08 December 2011 20:40
WATANZANIA leo tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru tukiwa na jambo moja kubwa la kujivunia ambalo ni umoja wa taifa letu.  Ingawa umoja huu umepitia katika mabonde na milima mirefu, kwa maana ya kukabiliwa na mawimbi na misukosuko ya kila aina, bado tumeweza kuulinda  kwa nguvu zetu zote.
    
Tumesisitiza mara nyingi kwamba umoja wetu ulisukwa katika misingi ya kujenga taifa moja lisilokuwa na matabaka, ukabila wala udini, lakini taratibu misingi hiyo ikaanza kukiukwa kwa kulea na kustawisha matabaka ya walio nacho na wasio nacho. Matokeo yake pengo baina ya maskini na matajiri likapanuka. Ule ukabila na umajimbo uliokuwa ukipigwa vita mara baada ya uhuru, ukaibuka kwa kasi kubwa. Udini nao ukaanza kujenga mizizi yake hatua kwa hatua.
    
Mwaka 1961 nchi yetu iliyoitwa Tanganyika ilipopata Uhuru, tuliweka vipaumbele vyetu, kwamba tunataka kutokomeza umaskini, ujinga na maradhi.  Tumejitahidi kiasi fulani,  lakini si kwa kiasi cha kuridhisha.  Bado tunateswa na umaskini. Kiwango cha elimu kinaendelea kushuka na vita dhidi ya maradhi vinazidi kuwa vigumu.  Na hata pale tulipoweka malengo ya milenia ya kupunguza umaskini ifikapo mwaka 2015 hatukuonyesha dhamira ya kufanikisha malengo hayo.
Tunadiriki kusema kuwa, hayo yote yameuweka uzalendo wetu majaribuni, kwa sababu tumeacha kufikiria maslahi ya nchi na kujikita katika ufisadi wa kusaka fedha za kujenga mahekalu,  kununua magari ya kifahari na kuwapeleka watoto wetu ng’ambo ili wapate elimu bora, huku watoto wa familia maskini wakiminyana na kunyukana katika shule za kata.  
Hali ya maisha kwa jumla badala ya kuboreka kwa walio wengi inazidi kudidimia. Baadhi yetu hawana uhakika wa kupata angalao  mlo mmoja kwa siku. Kima cha chini cha mshahara kimebakia katika kiwango cha kumdhalilisha mfanyakazi, kwani hakimtoshelezi kumudu hata huduma za msingi kama chakula, malazi, matibabu, usafiri, maji salama au elimu bora kwa watoto wake. Hesabu za gharama zote hizi na nyinginezo zikijumlishwa kwa kweli tutagundua kwamba mtu huyu anaishi kwa miujiza.  Hiyo ndiyo hali halisi hivi sasa miaka 50 ya Uhuru wetu.
    
Tuliposherehekea miaka 49 ya Uhuru mwaka jana Serikali ilisema kauli mbiu yetu katika sherehe hizo ni ‘Tudumishe Uzalendo’. Lakini sisi tulihoji kama kweli uzalendo unaweza kupatikana katika hali kama hiyo.  Uzalendo unatokana na mtu kuwa na matumaini ya kupata maendeleo na amani.  Mtu ataipenda nchi yake kama nchi hiyo nayo inampenda,  kwa maana ya kuweka mazingira yatakayomuwezesha kujiendeleza na kuendesha maisha yake kwa salama na amani. Uzalendo unachochewa na viongozi wanaoendesha nchi kwa uadilifu, kwa maana ya kuzingatia maadili ya uongozi na kuweka mbele maslahi ya nchi na wananchi wake, siyo kujikita na kubobea katika vitendo vya rushwa na ufisadi.
    
Hatudhani kama kwa umri wa miaka 50 nchi yetu bado inakidhi vigezo vya kuitwa taifa changa, kwani huo ni umri wa mtu mzima ambaye pengine ameshaanza kupata wajukuu. Ndiyo maana tunasema huu ni wakati wa kutafakari wapi tumetoka, wapi tuliko na wapi tuendako

kama taifa ili tupate dira ya kutupeleka tuendako tukiwa bado wamoja.Wakati tukiwatakia Watanzania heri na fanaka katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, tunatoa wito kwamba, iwapo  tunataka kuivusha nchi yetu kuelekea katika neema na maendeleo, kwa maana ya kujenga uchumi imara na kuwakwamua wananchi kutoka katika umaskini wa kutisha waliomo hivi sasa, yafaa sasa tujisahihishe kama taifa.
Hii ina maana kwamba lazima viongozi wetu watangulize uzalendo, wazingatie maadili ya uongozi na kusimamia misingi ya utawala bora. Katiba Mpya ambayo mchakato wake tayari umeanza lazima iwe chachu ya kulinda umoja wetu na kuleta mwafaka wa kitaifa ili kujenga Tanzania mpya yenye uchumi imara na jamii ya watu wanaojiamini na wanaoishi kwa matumaini.

No comments:

Post a Comment