Monday, December 12, 2011

Uranium kuanza kuchimbwa mwakani - TANZANIA

Uranium kuanza kuchimbwa mwakani  Send to a friend
Monday, 12 December 2011 11:19
0digg
Mwandishi Wetu
KWA mara ya kwanza, Tanzania itaanza kuchimba madini ya Uranium mwishoni mwa mwaka 2012, shughuli itakayofanywa na kampuni ya Mantra Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na kampuni hiyo jana, shughuli hiyo inatarajiwa kuanza kufanyika katika Mto Mkuju wilayani Ruvuma.
“Tumeshafanya tathmini ya kimazingira ya mradi huo ambayo imepewa Baraza la Mazingira (NEMC), Mradi huo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka kesho (2012),” taarifa hiyo ilimnukuu mwakilishi wa Mantra Tanzania, Asa Mwaipopo.
Ilisema kuwa, mradi huo utasaidia kuinua mikoa ya kusini kimaendeleo na kuliingizia taifa takribani Sh765 bilioni 765 na takribani Sh1.1 trilioni za kodi.
“Mradi huo utasaidia pia kuzalisha ajira zifuatazo 1,600 katika ujenzi
wa mradi huo na ajira nyingine 600 za moja kwa moja uchimbaji ukianza,” ilisema.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa, Mantra Tanzania imeendelea kujizatiti kwa kuzingatia usalama wa hali ya juu katika shughuli mbalimbali za kampuni hiyo jambo lililofanikisha kumaliza mwaka bila ajali yoyote katika kipindi cha uzalishaji kilichoisha Oktoba.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na ukweli kwamba kampuni inathamini maisha ya wafanyakazi na kutoa kipaumbele kwenye usalama wa wafanyakazi katika shughuli mbalimbali  za kampuni hiyo. “Hayo ni mafanikio makubwa katika utendaji wa kampuni kwa ujumla,” alisema Mwaipopo.
Mwaipopo alisema mafanikio ya kampuni hiyo yalitokana na mipango thabiti ya usalama iliyoandaliwa na kampuni hiyo na kutumika katika uzalishaji wa kampuni hiyo wa kila siku.
“Msemo wetu wa “usalama kwanza” umetusaidia sana kufikisha ujumbe kwa wafanyakazi pamoja na watu wote wanaohusika katika shughuli mbalimbali za kampuni yetu. Mafanikio hayo yasingepatikana kama tusingekuwa na ushirikiano wa pamoja,” alisema

Alisema kuwa, mbali na hatua yao ya kuchukua tahadhari kadiri walivyoweza, lakini pia kumaliza mwaka bila kuwepo kwa  kandarasi au mfanyakazi yeyote aliyeumia ni jambo la kumshukuru Mungu.

 “Tumefanikiwa kutimiza saa  522, 868  salama, nia yetu sasa ni  kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira ya usalama, Tutaendelea na msimamo ule ule na ndoto yetu sasa ni kutimiza masaa milioni moja bila kupata ajali ya aina yoyote,” alisema

Uchimbaji wa madini ya Uranium, umekuwa ukivuta hisia za watu wengi katika nchi mbalimbali duniani.
Kwa kiasi kikubwa hali hiyo inachangiwa na hatari iliyopo katika matumizi ya madini hayo kama yataingia kwenye mikono ya watu wasio waaminifu.
Hata hivyo viongozi mbalimbali wa serikali kwa nyakati tofauti, wamekuwa wakiwaondoa hofu wadau wa usalama duniani kuwa, Tanzania inachimba madini hayo kwa shughuli za maendeleo ikiwemo uzalishaji wa nishati.

No comments:

Post a Comment