Saturday, December 31, 2011

Kwanini Mkulima Mwamwindi alimpiga risasi RC Dk. Kleruu? Sehemu ya III na IV

 

Kwanini Mkulima Mwamwindi alimpiga risasi RC Dk. Kleruu? III

NAKUMBUKA alitunyoshea mkono akiwa anatabasamu. Tulizungumza kwa kushangaa, tukajiuliza; jamani hivi Serikali leo imempa Said Mwamwindi gari atembelee? Yakafuata yaliyofuatia. Maggid, ninayo mengi ya kukusimulia kwa yaliyotokea katika wakati ule….” Anasema Mzee Nzowa. Endelea kusoma simulizi hii katika sehemu yake ya pili.
“ Ndiyo, nilimfahamu Said, na jina lake hasa aliitwa Said Abdalah Siulanga Mwamwindi. Nyumba ya baba yake ilikuwa pale Mshindo karibu na ukumbi wa Welfare. Baba yake aliwahi kuwa Jumbe enzi  za ukoloni.  Kwa kweli Said alikuwa ni  mtu wa kilimo na nakumbuka alianzia kwenye magari. Alikuwa dereva kabla hajaenda kufyeka mapori ya kilimo kule Isimani.”
Je, unakumbuka wajihi wa marehemu Said Mwamwindi?
“Ah, yule bwana alikuwa pande la jitu. Mrefu na aliyeshiba hasa. Ukimwona utasema huyu jamaa amekaa kiutemi-utemi. Yaani, unavyoomwona mwanae, Amani Mwamwindi sasa, ndivyo kwa kiasi kikubwa alivyoonekana Said Mwamwindi. Wamefanana sana."
Na je, Dk.Kleruu, alikuwa mtu wa namna gani, wajihi wake na mengineyo?
”Alaa, Dk.Kleruu. Tulikuwa vijana wakati ule, na yeye alikuwa Mkuu wa Mkoa kijana hapa Iringa. Nafikiri alichukua nafasi ya Bw. Chamshama. Alikuwa mfupi kidogo. Ila bwana, alikuwa machachari sana . Nikisema ’machachari’ nadhani unanielewa.
Haraka sana tuliona dalili kuwa Dk.Kleruu asingekuwa na wakati mzuri hapa Iringa.
Alianza mapema sana kuonyesha tabia za ubwana na hata kunyanyasa aliowaongoza. Na katika hao aliowaongoza, kulikuwa na watu wazima waliomzidi umri.  Watu wenye hekima na busara kumzidi yeye, ingawa hawakusoma elimu ya darasani.”
Je, unaweza kutoka mfano wa ’ubwana’ mkubwa wa Dk.Kleruu aliouonyesha wakati huo?
”Iko mifano mingi, na ukweli Dk.Kleruu alisemwa vibaya katika midomo ya watu hapa Iringa. Ilifika mahala dereva akilipiga overtake gari la Dk.Kleruu hapa Iringa, basi, atasimamishwa na anaweza kuzabwa vibao na Kleruu mwenyewe. Aah! Jamaa yule alikuwa mbabe bwana!” Anasema Mzee Omary Nzowa huku akicheka kwa sauti. Kisha anaendelea.
”Unajua Dk.Kleruu alitokea Mtwara kabla ya kuja Iringa. Sasa kuna wakati alitamka; 'Hamnijui mimi, kawaulizeni watu wa Mtwara!' Sasa hayo si maneno ya kuwaambia watu wa Iringa, na hata mahali pengine popote,” akisimulia zaidi.
”Na nikwambie kitu kimoja Maggid, muhimu katika maisha ni kuishi vema na watu. Hata kama ni kiongozi, huwezi kufanikiwa katika kazi yako kama huna mahusiano mazuri na unaowaongoza. Na hata katika maisha ya kawaida, unaweza kuingia katika misukosuko isiyo ya lazima kama huna mahusiano mazuri na wenzako katika jamii.
”Nitakupa mfano hai unaonihusu mimi. Mwishoni mwa miaka ya 50 nilikamatwa nyumbani kwa kutokulipa kodi ya kichwa. Tulikuwa bado kwenye utawala wa mkoloni. Nilikuwa nadaiwa shilingi saba tu. Sikuwa nazo.
”Basi, nikaambiwa na askari wa kodi tuongozane hadi ofisini kwa DC. Tena walinifunga kamba mikononi. Nilifahamu, huko kwa DC ningeishia kuchapwa bakora na hata kuwekwa ndani. Unajua Maggid enzi hizo damu ilikuwa ikichemka na sisi vijana ndio tuliokuwa tukionekana kuiunga mkono TANU, ” ananiambia Mzee Nzowa akikumbuka enzi za ujana wake.
”Sasa basi, wakati tunakwenda kwa DC, niliwaomba sana wale askari wa kodi. Walikuwa Waafrika wenzetu. Nikawaambia, jamani ee, tafadhali tupite njia hii ya sokoni. Ni soko lile la zamani ambalo mpaka leo hii bado linatumika. Askari walikubali wakidhani nimechagua mwenyewe njia nitakayoonekana na watu na hivyo kujidhalilisha mwenyewe. Kumbe, mimi nilikuwa na maana yangu.
Tulipofika eneo la sokoni nikasikia jamaa zangu wakiuliza kwa sauti; ” Omary shida gani?”. Nikajibu kwa sauti; ” Kodi, shilingi 7!”. Basi, huwezi kuamini, hata kabla sijamaliza soko, vijana wale wa sokoni walichangishana. Shilingi saba zikapatikana. Kodi ile nikalipa na nikaachiwa huru. Pointi yangu hapo ni umuhimu wa mahusiano mema na watu.”
Je, unafikiri ni kwanini Dk. Kleruu alipata tabu sana kufanya kazi na watu wa Iringa?
Anasema Mzee Nzowa: ” Mi nadhani Kleruu, kwa jinsi alivyokuwa, angepata tabu kufanya kazi mahali po pote pale. Tatizo ni ile hali ya kutanguliza ubwana na kuwadharau wananchi. Hakika wakati ule Mwalimu Julius Nyerere alipata tabu sana na namna ya ku-deal na viongozi kama akina Kleruu. Kumbuka ,Tanzania kama nchi ilikuwa taifa changa sana. Hatukuwa na wasomi wengi. Nilimfahamu Nyerere, hili la Kleruu lilimsumbua sana Mwalimu.
”Nikwambie Maggid, Ujamaa na Kujitegemea kama itikadi na sera za Mwalimu haukuwa tatizo. Tatizo lilikuwa kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya utekelezaji. Hawa hawakuwa wanasiasa, wakati mwingine walionekana kama Wanyapara. Mwalimu wakati ule hakujua kila kitu kuhusu watu aliowateua kumsaidia.
”Ni kweli Mwalimu alitia saini hukumu ya kunyongwa kwa Mwamwindi, lakini naamini hakufurahia, bali hali ya wakati ule ilimlazimisha kufanya vile.
”Sisi tuliomfahamu Mwalimu tunajua kuwa hukumu ile ni moja ya maamuzi magumu yaliyomsononesha sana Mwalimu. Unajua wakati ule kuna Wakuu wa Mikoa waliojenga hoja, kuwa kama Mwamwindi kwa tendo lile asingepata adhabu ile, basi utendaji wao wa kazi mikoani ungekuwa mgumu. Ndiyo, hoja hizo ziliibuka. Kwa kiongozi wa nchi ni mtihani. Siyasemi haya kumtetea Mwalimu bali ni kutambua ukweli kuwa Mwalimu alikuwa ni binadamu kama wewe na mimi.”
Unasema ulimfahamu Nyerere na kwamba unaamini kwa wakati ule tatizo kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa kwa baadhi ya aliowapa dhamana ya kumsaidia katika utekelezaji. Je, Mwalimu aliwahi kulizungumza jambo hili nawe ukamsikia?
”Huo ndio ukweli. Mimi nimekuwa katika chama (TANU) tangu mwaka 1956. Kadi yangu ya uanachama wa TANU niliikatia Mbeya. Ni Nyerere mwenyewe, kwa mkono wake, pale Mbeya, mwaka 1956 alinijazia kadi yangu ya TANU. Alianza na Kanali Ayoub Simba ikaja ya kwangu.
”Hata leo, ukiangalia namba za kadi ya TANU ya Kanali Ayoub Simba na ya kwangu zinafuatana. Tulikuwa bado vijana sana, na Mwalimu alifanya mwenyewe kazi ya kuhamasisha vijana kuingia TANU. Mwenzangu Ayoub yeye akaja akaingia jeshini , akafikia mpaka cheo cha ukanali, akawa mbunge pia, kule Mafia. Yule ni kada wa siku nyingi.
”Sasa nimepata kumsikia Mwalimu akiongea kuhusu hili la uongozi? Kwa kweli si mara moja. Nimemsikia Mwalimu akitamka, kuwa njia iliyo nzuri sana ya kumsaidia katika uongozi wake ni kwa tulio karibu na watu kumwambia moja kwa moja juu ya mazuri na mabaya wanayofanya wateule wake.
”Kwamba ni hatari wananchi wakianza ama kuchoka kulalamika au kuwaogopa viongozi wao. Unajua Mwalimu hakuishia tu kutumia watu wa Usalama wa Taifa, aliwatumia pia watu wa kawaida kupata taarifa sahihi.”  Mzee, turudi kwenye kilichotokea kule Isimani, inasemekana kulikuwa na mtikisiko mkubwa hapa Iringa baada ya Dk.Kleruu kupigwa risasi na Mwamwindi. Je, hali ilikuwaje hasa?
” Ni sahihi, hali ilikuwa ngumu. Wengi tuliathirika na mkasa ule, kwa namna moja au nyingine. Unajua ilifika mahali wakati ule mtu ukigongewa mlango usiku, basi, unavaa kabisa, shati, suruali na viatu, maana huenda ukifungua mlango usirudi tena kitandani kwako!”
Hivi Iringa ya wakati ule ilionekaje, unakumbuka?
Anajibu Mzee Nzowa: ” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”. Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
Wakati tukimsubiri  Mzee Nzowa , Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza;

” E bwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dk. Kleruu. Mimi nilikuwa kijijini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha jirani na alikoishi Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka kumi. Nakumbuka mambo mengi sana , hata Dk. Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa unasikia....” ( Simulizi hii itaendelea)

Add new comment

Kwanini Mkulima Mwamwindi alimpiga risasi RC Dk. Kleruu? IV

HII ni sehemu ya tatu ya simulizi kuhusu kwa nini mkulima Mwamwindi alimpiga risasi Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa wakati huo, Dk. Kleruu. Endelea...
Hivi Iringa ya wakati ule ilionekanaje, unakumbuka? Namwuliza Mzee Nzowa.” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”. Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
Wakati tukimsubiri Mzee Nzowa, Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza; “Ebwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dk. Kleruu. Mimi nilikuwa kijijini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha jirani na alikoishi marehemu Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka 10. Nakumbuka mambo mengi sana, hata Dk. Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa unasikia....”
“Dk. Kleruu alikuwa akija na gari lake. Nyang’olo ni mji wa barabarani. Unajua ndio ilikuwa njia kuu ya kwenda Dodoma mpaka Arusha. Kulikuwa na biashara sana. Kulikuwa na wasomali hata waarabu. Nakumbuka Dk. Kleruu alikuwa akishika kifimbo chake na kuwafokea wazee juu ya mambo ya maendeleo. Kwa kweli wazee wa Nyang’olo hawakumpenda Kleruu,” anasema msomaji huyu ambaye sasa ana miaka 50 na anaishi nchini Uingereza.
Na wakati tukiendelea na simulizi hii ya Mwamwindi zimenifikia habari mbaya. Ni taarifa ya msiba wa Mzee Augustino Hongole Mzee Hongole ambaye, hadi kifo chake alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri wa gazeti la Kwanza Jamii, Njombe  amefariki majuma mawili  yaliyopita. Amezikwa kijijini kwao Lupembe., Njombe.
Kwangu mimi, Mzee Hongole ni  mmoja wa wazee waliochangia sana katika kuifanya simulizi hii iwe na maana kubwa. Maana, katika utafiti wangu juu ya kisa hiki cha Mwamwindi na Mkuu wa Mkoa Dk. Kleruu, nimepata bahati ya kufanya mazungumzo marefu ya ana kwa  ana na hata kwa njia ya simu na marehemu Mzee Hongole.
Na kweli mwandishi wa habari mwandamizi wa magazeti ya HabariLeo na Daily News, Beda Msimbe ndiye aliyenisisitiza sana umuhimu wa kumhoji Mzee Hongole huku kaka yangu Msimbe akisema; “Usichelewe sana, maana wazee hao ndio wanaondoka taratibu”.
Na hakika nimefanya jitihada za ziada za kupokea simulizi za Mzee Hongole juu ya anachokikumbuka katika wakati ule wa tukio.
Na katika hili la simulizi ya Mwamwindi mchango wa marehemu  Mzee Hongole ni mkubwa sana. Mzee Hongole amechangia kutoa elimu kubwa ya kimapokeo. Hakika, nina maelezo mengi ya Mzee Hongole ambayo nimeyahifadhi  kwa simulizi za baadae. 
Huko nyuma  nimewahi kusimulia yafuatayo niliyoyapokea kutoka kwa Mzee Hongole juu ya tukio la mkulima Mwamwindi kumpiga risasi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.
Mzee Hongole aliyepata kuwa mwandishi wa habari kijana sana wakati wa tukio la Mwamwindi kumuua Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu lililopotokea anasema; "Ndio kwanza nilikuwa nimepangiwa kufanya kazi kama mwandishi wa habari kwenye gazeti la Kanisa pale Iringa.
“Lilikuwa tukio kubwa sana. Kama mwandishi nilitamani kuandika kilichotokea na kupata maoni ya watu wa Iringa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla. Kwa wakati ule mfumo haukuruhusu kitu kama hicho. Mwamwindi story was an embargoed one (Stori ya Mwamwindi ilikuwa haiandikiki). Lakini nataka kukwambia: "Watu wengi wa Iringa hawakumpenda Dk. Kleruu kutokana na unyanyasaji wake".
Mzee Hongole anazidi kusema; “Unajua wakati huo kulikuwa na hofu kubwa juu ya dola. Waliokuwa tayari kumtetea Mwamwindi hadharani walihofia kukamatwa na makachero. Na mimi kalamu yangu ikawa nzito kwa kuogopa jela.
Lakini, kikubwa ni kuwa watu wa kanda hii walikuwa wamoja katika kumuunga mkono Mwamwindi.  Shida kubwa ilikuwa kwenye uUtekelezaji wa Azimio la Arusha. Utekelezaji ule kwa mtazamo wangu  ulifanywa kimakosa katika maeneo mengi ya nchi ikiwamo kanda yetu hii. Wananchi hawakuulizwa wanataka nini. Walilazimishwa tu na viongozi.
Nakumbuka kule Ilembula kuna wanafunzi waliolazimishwa baada ya masomo waende wakapande miche ya kahawa kwenye shamba la kijiji. Wazazi hawakupenda kilimo cha kahawa, lakini, Serikali ilitaka walime kahawa. Basi, ikatokea, kwa wazazi kuwaambia watoto wao, kuwa wakifika shambani waigeuze miche ya kahawa. Wapande juu chini. Hivyo hawakupanda, walipandua,” anasema Mzee Hongole.
Mzee Hongole anaendelea kusema; “Unajua ni mazingira kama hayo ndio yaliyochangia uzalishaji upungue. Wananchi walijisikia kushurutishwa. Hawakufanya kazi kwa moyo. Na vyombo vya habari navyo havikuwa huru kuweza kuelezea hali halisi za wananchi. Hapa utaona jinsi tulivyokuwa, kama taifa,  tukitoka kwenye reli. Maggid, nawaonea wivu sana katika wakati wenu huu kama wanahabari.
“Sisi tulisomea taaluma hii. Tena mimi nilipelekwa na Kanisa mpaka Sweden. Lakini, taaluma zetu zikaishia kufanya kazi ya kusifia Serikali tu, hata kwa mambo ya kipuuzi yaliyofanywa na baadhi ya viongozi. Wakati huo wa tukio la Mwamwindi watu wengi walikuwa na hamu ya kutaka kuujua ukweli. Lakini, sisi wanahabari tuliogopa hata kufika kijijini kwa Mwamwindi kuwahoji waliokuwepo siku ya tukio”
Mzee Hongole anasisitiza kwa kusema kuwa wakati umefika kwa Watanzania kuipitia upya historia yao. Hii itasaidia kuwafanya vijana wa kizazi hiki kujitambua. Watajenga mioyo ya uzalendo na kuwa tayari kuipigania nchi yao.
“Mimi nina shaka kuwa vijana wa siku hizi wamekosa kujiamini kwa vile hawajitambui. Hawaijui historia yao. Wana kiu ya kutaka kuifahamu historia yao. Ni kazi yenu nyinyi waandishi vijana kufanya tafiti juu ya historia yetu na kuisimulia,” anasema Mzee Augustino Hongole. . Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi, Amen.

No comments:

Post a Comment