Saturday, December 31, 2011

Mwandishi wa BBC John Ngahyoma afariki

Mwandishi wa BBC John Ngahyoma afariki

 30 Disemba, 2011 - Saa 17:10 GMT
Marehemu John Ngahyoma
Mwandishi wa BBC John Ngahyoma alifariki Ijumaa mjini Daresalaam
Mwandishi wa BBC John Ngahyoma amefariki dunia Ijumaa asubuhi nyumbani kwake mjini Dar Es Salaam.
Bwana Ngahyoma ameugua maradhi ya moyo kwa kipindi kirefu, na mwaka huu unaomalizika wa 2011 alifanyiwa upasuaji nchini India.
Amemwacha mke na watoto watatu.
Kaka mkubwa wa marehemu John, Ngalinecha Ngahyoma ameambia BBC kwamba mazishi yatafanyika jumapili, katika makaburi ya Kinondoni.
Ngahyoma ametumika katika BBC kwa kipindi kisichopungua miaka kumi.
Marehemu John Ngahyoma alizaliwa mwezi November mwaka 1960. Baada ya elimu ya Msingi alisoma katika sekondari ya Azania mijini Dar es Salaam na baadaye kuchukua Diploma katika chuo kikuuu cha St Augustine jijini Mwanza wakati huo kikijulikana kama Nyegezi Social.
Baadaye aliajiriwa katika magazeti ya Mwafrika na Daily News na baadaye Radio One na Itv Kabla yaa Kujiunga na Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Alikuwa mkuu mkuu wa Ofisi ya BBC Tanzania hadi mauti yalipomkuta Ijumaa asubuhi.
Waandishi mbali mbali wamekuwa wakituma risala za rambi rambi kufuatia kufariki kwa Bwana Ngahyoma.
Mwandishi wa BBC visiwani Zanzibar Ally Saleh Alberto ameandika haya kuhusu alivyomfahamu marehemu Ngahyoma.
Kwa karibu ya mwaka mmoja na nusu hivi sauti ya John Ngahyoma imekuwa haisikiki kukata mawimbi ya idhaa maarufu kuliko zote duniani BBC. Ni sauti
iliyokuwa imezoeleka. Kumbe mwenzetu alikuwa akipata majaribu ya Muumbaji ambaye aliamua kumpamaradhi ambayo ni yeye peke yake ambaye ndio angeweza kuyatoa hata waganga
na waganguzi wa dunia nzima wangekusanyika.


Muumbaji akaamua pia hatimae achukue roho ya kiumbe chake, ambacho hukiomba kwa kufumba na kufumbua na pamoja na maringo yetu yote binaadamu lakini
nguvu hii ya Muumba hutuamulia juu ya kilele cha mafanikio yetu, kama ambayo Ngahyoma alikuwa amefanikiwa kuyafika.


Nilianza kumjua Ngahyoma kama mwandishi wa Independent Television ITV na hasa nikimuona akitangaza habari za michezo. Alikuwa na fasaha nzuri ya
Kiswahili kama vile anatoka Pwani na mara nyingi nikawa nasema huyu atafika mbali.


Mara nikawa namuona akisoma taarifa ya habari. Huyu pamoja na kutoka mabara lakini alikuwa anamudu matamshi yote ya Kiswahili vilivyo na alikuwa mwingi
wa nahau na ndio maana mara akaajiriwa na BBC kwa maana BBC ilikiona kipaji chake.


Ni sifa ya BBC kwamba muajiriwa hutakiwa kufanya vitu vingi au niseme kila kitu. Mbali ya kuongoza vipindi, lakini muajiriwa pia huwa muandishi na
huko kwenye uandishi basi huwa ni fani zote.


Na kwa wengi huo huwa mtihani na ndio maana kuna wachache wetu ambao wamejikita katika fani chache, lakini wengi wetu ukitutupa kwenye uchumi
utafikiri wachumi, kwenye siasa utafikiri wahadhiri wa siasa na kwenye michezo ohooo huko ndio usiseme.


Hiyo pia ilikuwa ni sifa ya Ngahyoma. Aliweza kujijengea heshima katika kada ya uandishi alipojiunga na BBC kwa sababu talenta yake, chembilecho
wanavyosema Wakenya ndipo ilipokuja sio tu kujulikana kwa ufasaha lakini pia kun'gara kama mwezi.


Jina Ngahyoma likaanza kujulikana Tanzania na ikawa ni moja ya alama za BBC nchini Tanzania na watu wengi wakataka kujitambulisha nae na kwa hivyo
milango ya kupata habari ikawa wazi zaidi kwa BBC kote Tanzania.


Alijichanganya kirahisi. Kwenye michezo alijenga vyanzo vya habari lakini zaidi marafiki; kwenye biashara alipenya lakini akaweza kupenyezewa taarifa
nyingi zilizoipa sifa BBC na kwenye siasa alikuwa mwepesi wa kujua mstari wake unaishia wapi na kwa hivyo akaheshimika na kila kiongozi na chama cha
siasa.


Hakuna wakati mgumu alioupata Ngahyoma kama alivyohamishwa na mkubwa wetu wakati huo Tido Mhando kwenda Zanzibar, wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu
wa 2005 ambako alipiga kambi huko kwa miezi 6 kuiwakilisha BBC.


Ngahyoma alijikuta katika ushindani mkali wa kisiasa huko Visiwani ambako siasa zilikuwa ni ngumu na ushindani baina ya CUF na CCM ukiwa mkali na
kutishia hata uhuru na usalama wa waandishi wa habari.Ninalomsifu Ngahyoma kulimudu ni kufanya kazi yake kisawa sawa kabisa na kila upande ukaridhika kuwa ameripoti kipindi cha Uchaguzi bila ya kulalia
upande wowote ule.


Na hapo ndipo Ngahyoma alipokuwa amewiva na sikuona ajabu basi baada ya kuondoka Vicky Ntetema kama Mkuu wa Kituo cha Dar es salaam alikuwa ni
Ngahyoma aliyechukua nafasi hiyo.Kama Bosi wangu ilikuwa rahisi kufanya kazi na Ngahyoma. "Ehe Brother Ally," kama alivyozoea kuniita, maana mimi ni mkubwa kiumri kwake, " Kuna
nini leo Zanzibar."


Alikuwa rahisi kufanya kazi na watu na alimpa kila mtu uhuru wake lakini hakuwa akiogopa kumkosoa mtu au kutoa muongozo kwa analolihisi linafaa
kufanywa kwa faida ya BBC.Mbele ya Mungu ni dhambi kusema hakuna pengo la binaadamu ambalo haliwezi kujazwa, lakini kwa binaadamu ni dhaifu tunasema kuwa pengo la Ngahyoma
linataka mtu wa mbegu maalum kulijaza.


Si rahisi kumpata mtu rahimu, karimu, mchangamfu, mchapa kazi, mtu wa watu,msaidizi, muongozaji, mcheshi, mchekeshaji ndani ya binaadamu mmoja na
hivyo ndivyo alivyokuwa Ngahyoma.Ni sisi tuliokuwa nae karibu ndio tunaojua ni jinsi gani tumempoteza mtu miongoni mwetu na inshallah Mwenyenzi Mungu atupe subira, lakini asitume
sahau ya kumsahau Ngahyoma, maana kutokana na kuendelea kumkumbuka ndipo ambapo tutamuenzi

No comments:

Post a Comment