Wafungwa kifungo cha maisha kwa mabomu Rwanda
13 Januari, 2012 - Saa 17:03 GMT
Mahakama kuu mjini Kigali,
Rwanda, imewahukumu kifungo cha maisha jela watu 10 kwa kuwapata na
hatia ya kuhusika katika mashambulio ya mabomu yaliyokumba nchi hiyo
miaka miwili iliyopita.
Jumla ya washukiwa 30 walihusika katika kesi hiyo ambapo wanane wameachiwa huru kwa kukosekana ushahidi dhidi yao.Mahakama kuu imethibitisha maombi ya mwendesha mashtaka na kuwahukumu washukiwa 10 adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kuwakuta na hatia ya makosa ya ugaidi, mauaji na kuwa katika kundi la kigaidi.
Mahakama imesema kuwa pamoja na kuwakuta na hatia ya kushirikiana na wengine katika kusafirisha magurunedi pia walihusika kwa njia moja au nyingine katika mashambulio licha ya kwamba walikana kuhusika.
Kuna washukiwa wakuu saba waliokiri mashtaka na kutaja wale walioshirikiana kusafirisha mabomu hayo kutoka ngome za kundi la waasi wa FDLR mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kufanya kampeni za kundi hilo miongoni mwa wananchi na kuhusika moja kwa moja na ulipuaji wa mabomu hayo katika maeneo mbali mbali ya nchi.
Waliokiri mashtaka hayo wamepunguziwa adhabu na kupewa kifungo cha miaka 20 jela.
Wengine 5 wamepewa kifungo cha miaka kati ya mitano na 15.
Mahakama ikawafutia mashtaka wengine wanane kwa kukosekana ushahidi dhidi yao na kuwaachilia huru.
Walioachiliwa huru walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya ugaidi, kushirikiana na kundi la kigaidi, mauaji na kuvuruga usalama wa taifa.
Mashambulio ya magurunedi yalianza mwaka 2008 katika sehemu mbalimbali za Rwanda kabla ya kufululiza mjini Kigali mwaka 2010 yalikenga vituo vya mabasi ya abiria ambapo watu kadhaa walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.
Wakati ziliposoma hukumu hizo hakuna upande mwingine uliowakilishwa na pande husika zimepewa siku 30 za kukata rufaa ikiwa kutakuwa na yeyeyote ambaye hakuridhika na uamuzi wa mahakama.
No comments:
Post a Comment