Thursday, January 19, 2012

Madaktari, Serikali ngoma nzito

Madaktari, Serikali ngoma nzito  Send to a friend
Wednesday, 18 January 2012 21:02
0digg
Geofrey Nyang'oro
MGOGORO baina ya Serikali na madaktari umeingia sura mpya baada ya wanataaluma hao kutoa madai mapya ikiwa ni pamoja na kuongezewa posho, huku Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya akiwapiga chenga kuhudhuria mkutano wao uliofanyika Dar es Salaam jana.
Juzi, Dk Nkya alitoa tamko la Serikali kuhusu mgogoro huku akitupilia mbali madai ya wataalamu wa tiba ya magonjwa ya binadamu na kutetea uamuzi wa kuwahamisha na kuwapangia vituo vipya vya kazi baadhi yao kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi alisema moja ya sababu za mkutano wa jana ilikuwa ni kujibu kauli hiyo Serikali iliyotolewa na dhidi ya madai yao.

Alisema tamko hilo la Wizara ya Afya lilikuwa la kisiasa zaidi kuliko uhalisia. Alisema madai ya madaktari ni kupatiwa nyumba za kuishi, kuongezewa posho za muda wa ziada za kazi ambazo sasa ni Sh10,000 na mishahara.

Akizungumza katika mkutano huo, mjumbe wa MAT, Dk Hamis Kigwangala alisema: “...Tunataka posho Sh200,000 na mshahara kima cha chini Sh 3.5 milioni.”

Kuhusu mshahara alisema wanayo haki ya kulipwa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa Serikali ina fedha, ndiyo maana imewaongezea wabunge posho za vikao. “Tunastahili kulipwa... fedha ipo. Kwani wanazolipwa wabunge zinatoka wapi?.”
Alisema umefika wakati taaluma ya udaktari iheshimiwe na kuthaminiwa kwani ni kazi ya wito huku akipendekeza kufutwa kwa utaratibu wa kutoa vibali kwa vigogo kwenda kutibiwa nje, akisema ndicho kinachowatia kiburi hadi kuwapuuza madaktari.

“Anayesaini mgonjwa aende nje ni daktari na wakati mwingine hata kama mgonjwa anayeomba kwenda nje angeweza kutibiwa nchini. Utaratibu huo ni mbovu tugome kutoa vibali ili tuanze kuthaminiwa,” alisema.

Kwa upande wake, Dk Zaituni Sanya alisema kumekuwa na vitendo vya kupuuzwa kwa madaktari: “Sasa umefika wakati wa Serikali kuwathamini wana taaluma, tumechoka kunyanyaswa.”

Kabla ya kuanza mkutano wa jana, madaktari hao walituma ujumbe wa madaktari watatu wakiongozwa na Makamu wa Rais MAT, Dk Primus kwenda kumtaka Dk Nkya afike ili azungumze nao ana kwa ana kuhusu matatizo yao bila mafanikio.
“Mheshimiwa tumemwona na tumezungumza naye kwamba mmetutuma kumwita aje, amekubali lakini anaomba apewe muda wa saa moja ili ajiandae,” alisema Dk Saidia mara baada ya kurejea mkutanoni akitokea Wizara ya Afya.

Hata hivyo, baada ya saa moja kupita bila ya Naibu Waziri huyo kutokea, Dk Saidia aliwaambia wajumbe zaidi ya 200 waliohudhuria mkutano huo kwamba alipokea simu kutoka kwa kiongozi huyo akisema kwamba asingeweza kufika jana kama alivyokuwa ameahidi na badala yake akaomba wakutane leo.



Katika madai yake ya msingi, MAT inataka kurejeshwa kwa madaktari wote waliokuwa wakifanya mazoezi ya vitendo MNH na kupitiwa upya uamuzi wa kuwahamisha madaktari bingwa 61, kutoka hospitali hiyo ya taifa.
Madaktari 194 waliokuwa wakifanya mazoezi ya vitendo Muhimbili waliondolewa na kupelekwa katika vituo mbalimbali baada ya kuibuka kwa mgogoro wa malipo.

Msimamo wa Serikali

Katika tamko lake, Serikali ilisema tathmini iliyofanywa na wizara ilibaini kuwa idadi ya madaktari waliokuwa katika mafunzo kwenye hospitali ya Muhimbili ni kubwa kuliko uwezo wake akisema wingi wao ungeathiri mafunzo ya taaluma yao.

Pia ilisema uongozi wa hospitali hiyo ulilazimika kuwaandikia barua ya kuwarejesha wizarani, kutokana na kitendo chao cha kugoma huku ikisisitiza kwamba hawakufukuzwa kazi, bali walirejeshwa wizarani ili kupangiwa vituo vingine vya kazi kumalizia muda wao wa mazoezi kwa vitendo, baada ya kuvunja mkataba na uongozi wa hospitali hiyo.

“Kwa kuzingatia hatua zilichokuliwa na wizara na jinsi wahusika walivyotekeleza maagizo ya Serikali, hadi sasa ni dhahiri kuwa tamko la MAT kuhusu kunyanyaswa kwa madaktari walioko mazoezini halina msingi wowote,” alisema Dk Nkya alipokuwa akitoa tamko hilo juzi.

No comments:

Post a Comment