Friday, January 13, 2012

Uongozi UDSM usikose uvumilivu, utafute suluhu

Uongozi UDSM usikose uvumilivu, utafute suluhu  Send to a friend
Friday, 13 January 2012 10:21
0digg
HABARI kwamba hali ya mambo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) imeendelea kuwa tete baada ya kumalizika kwa  fujo na vurugu zilizotokea chuoni hapo wiki kadhaa zilizopita, hakika zimetusikitisha sana.

Kwamba uongozi wa chuo hicho juzi uliwafukuza wanafunzi 13  na kuwasimamisha masomo kwa muda usiojulikana wengine 86 kunajenga picha kwamba siyo tu matumaini yaliyokuwapo ya kurudia kwa hali ya utulivu na amani chuoni hapo yametoweka, bali pia kwamba njia za mawasiliano kati ya uongozi na wanafunzi sasa zimefungwa kutokana uongozi huo wa UDSM pia kuwafukuza baadhi ya viongozi wa serikali ya wanafunzi (Daruso).  
Viongozi hao wa serikali ya wanafunzi waliofukuzwa ni   pamoja na; Spika, Naibu Spika, Waziri wa Elimu, Naibu Waziri wa Elimu na Waziri wa Mikopo. Viongozi hao ndiyo hasa waliokuwa wanashikilia nafasi nyeti katika serikali hiyo ya wanafunzi, hivyo tunadhani kuwatimua kwa mpigo kwa sababu ya kutetea na kusimamia maslahi ya wanafunzi waliowaweka madarakani ni sawa na kuipindua serikali halali ya wanafunzi.
Wakati tukiweka wazi msimamo wetu kwamba kamwe hatuungi mkono vitendo vya utovu wa nidhamu na vurugu vyuoni, tunalazimika kusema kwamba tangu viongozi hao watimuliwe juzi, wanafunzi wa chuo hicho hakika wamezibiwa kabisa njia za mawasiliano kati yao na uongozi wa Chuo, hasa linapokuja suala la kuwasilisha madai na matatizo yao kwa uongozi, hata kama uongozi huo unadhani madai hayo hayana msingi.
Hali hiyo ni hatari kwa amani na ustawi wa Chuo kwa sababu hali ya kutokuwapo wawakilishi wa kuwasiliana na uongozi itasababisha wanafunzi waishi kwa fununu , tetesi, minong’ono na uzushi na matokeo yake ni vurugu ambazo zinaweza kusababisha mtafaruku mkubwa na hatimaye Chuo kufungwa.  
Tumeelezwa na uongozi wa Chuo kwamba wanafunzi hao wamefukuzwa au kusimamishwa masomo baada ya kuanzisha mgomo wa siku mbili kwa lengo la kuushinikiza uongozi huo kuwarejesha wenzao 48 waliofukuzwa mwezi uliopita. Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema juzi wakati akitangaza adhabu hiyo kwa waandishi wa habari kwamba hatua hiyo imechukuliwa baada ya Baraza la Chuo kuafiki adhabu hiyo.
Pamoja na kumuheshimu sana kiongozi huyo na uongozi mzima wa chuo hicho, tunadhani hatua iliyochukuliwa dhidi ya wanafunzi hao, wakiwamo viongozi wa serikali yao ilitokana na uongozi wa chuo na Baraza la Chuo kukosa uvumilivu, hasa kwa kutilia maanani kwamba wanafunzi hao hawakufanya vurugu au kuharibu mali za Chuo walipoitisha mgomo. Inawezekana kwamba uongozi wa chuo hicho umechoka kutokana na mikikimikiki na harakati za wanafunzi (student struggles) zisizokwisha, hasa baada ya Serikali kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Hata hivyo, Spika wa Bunge la Wanafunzi anadai kwamba  walifuata Katiba ya bunge hilo katika kuitisha mgomo kwa kura 56 za ‘ndiyo’ dhidi ya kura 5 za ‘hapana’ na kwamba baada ya maazimio hayo kupitishwa na Bunge na Rais kuweka saini kuashiria kufanyika kwa mgomo, walishangaa kuona uongozi wa Chuo ukiwataka wabatilishe maazimio ya Bunge wakati katiba haiwaruhusu kufanya hivyo. Alisema kikatiba, Bunge likishapitisha maazimio yeye au naibu wake hawawezi kuyatengua. Huo ndiyo upande wa pili wa shilingi.
Wakati tukiuomba uongozi wa UDSM kufikiria upya adhabu hii kubwa ulioitoa kwa wanafunzi hao na viongozi wao, tunataka ieleweke kwamba kamwe hatuna lengo la kuchochea migomo au vurugu katika vyuo vyetu hapa nchini. Tunachosisitiza hapa ni kwamba busara, hekima na uvumilivu vitumike katika kutatua migogoro badala ya kuichochea. Tunaishauri Serikali na viongozi wa vyuo nchini wafikirie kupanua wigo wa mawasiliano na serikali za wanafunzi ili yapatikane maridhiano katika mambo muhimu, ikiwa ni pamoja na serikali hizo kuwezeshwa kupata katiba zenye kusimamia ustawi wa jumuiya nzima ya wanafunzi katika nchi yetu.

No comments:

Post a Comment