Friday, January 13, 2012

Kanisa Katoliki la laani uchaguzi DRC

Kanisa Katoliki la laani uchaguzi DRC

 13 Januari, 2012 - Saa 04:04 GMT
hesabu za kura
Kanisa katoliki linasema matokeo sio ya kweli
Maaskofu wa kanisa Katoliki wametangaza kuwa hawatambui matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwezi Novemba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakiongozwa na kadinali Laurent Mosengwo, wamewataka wakuu wa tume ya uchaguzi kujiuzulu baada ya kushindwa kusimamia uchaguzi huo.
Rais Joseph Kabila alitangazwa mshindi huku mpinzani wake Etienne Tshisekedi akidai yeye ndiye rais.
Maaskofu hao 35 wamekuwa wakikutana mjini Kinshasa kutathmini matokeo ya zoezi hilo ambalo pia kanisa hilo lilikuwa na waangalizi kote nchini humo.
Viongozi hao wa kanisa wamesema jukumu la bunge la kwanza ni kuhakikisha kuwa tume nyengine inayojumuisha mashirika ya kijamii, vyama vyote vya kisiasa na makanisa inabuniwa.
Awali raia wengi nchini humo walitarajia kuwa kanisa hilo litaitisha maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi huo lakini maaskofu hao wametaka mazungumzo ya maridhiano yafanyike kati ya wanasiasa.
" Tuna hofu kuwa ikiwa utawala utazidi kupuuza ombi la kufanya mazungumzo huenda nchi ikaingia kwenye matatizo ya kisiasa ambayo yalishuhudiwa katika miaka iliopita" alisema katibu wa kundi hilo la maaskofu, Abbot Leonard Santedi.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka mashirika ya kimataifa likiwemo lile la Carter Centre kutoka Marekani, walisema uchaguzi huo ulighubikwa na dosari na ni vigumu kutambua mshindi.
Hata hivyo mahakama kuu nchini humo ilimuidhinisha Rais Kabila kama mshindi.
Rais Kabila mwenyewe alikiri kuwa kulikuwepo na dosari lakini sio kiasi kile mshindi hakuweza kutambulika.

No comments:

Post a Comment