Friday, January 13, 2012

KIKWETE apokewa kwa, vilio Mabwepande- DAR

JK apokewa kwa, vilio Mabwepande  Send to a friend
Saturday, 14 January 2012 09:00
0digg
Keneth Goliama
RAIS Jakaya Kikwete jana alipokewa kwa mabango na vilio kutoka kwa wakazi wa Mabwepande walioondolewa kwenye maeneo hayo ili kuwapisha waathirika wa mafuriko, Dar es Salaam.Kilio kikubwa cha wananchi hao ni kuondolewa kwenye maeneo hayo bila kulipwa fidia, jambo ambalo wanalitafsiri kuwa ni dhuluma na uonevu.

Mara baada ya Rais Kikwete kuwasili eneo hilo majira ya saa tano asubuhi, watu hao waliokuwa wameandaa mabango waliyanyanyua juu ili kiongozi huyo wa nchi ayaone. Hata hivyo, wakati wakinyoosha mabango hayo, polisi waliokuwa kwenye maeneo hayo waliwanyang'anya.

Kutokana na tukio hilo, polisi walikamatwa watu tisa kwa kitendo hicho cha kuonyesha mabango hayo kwa madai ya kutaka kusababisha vurugu kwenye ziara hiyo ya Rais.

Baadhi ya mabango yalisomeka; “Tumekuwa wakimbizi, tumekuwa waathirika wapya wa maafa badala ya kuwakaribisha wageni wetu (waathirika wa mafuriko).”

Hata hivyo, nguvu ya polisi iliyotumika kuwanyang'anya mabango, ilizima mpango huo wa kufikisha ujumbe kwa Rais. Kuona hivyo, baadhi yao, wake kwa waume walianza kuangua kilio kiasi cha ambacho pia kilimshutua Rais Kikwete.

Wananchi hao walilalamika kwamba waliwasilisha kilio chao katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam lakini hawakusikilizwa na kushangaa kuona greda likiingia kwenye viwanja vyao na kutengeneza barabara.

Hata juhudi za Katibu Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye za kuwatuliza wananchi hao hazikufua dafu kwani walisisitiza kutaka kuonana na Rais Kikwete. Baadaye Rais aliwaendea na kuwahoji viongozi wa mkoa sababu za kilio cha wananchi hao.

Baada ya malalamiko ya wananchi hao kuelekezwa kwa viongozi wa mkoa, Rais Kikwete aliwaagiza wapeleke vielelezo vya viwanja vyao kwa Mkuu wa Wilaya au Mkoa ili kutatua tatizo hilo.

Walimweleza Rais Kikwete kwamba walivunjiwa nyumba zao za kuishi eneo hilo ili kupisha waathirika... “Mheshimiwa Rais sisi tupo hapa kwa miaka mingi. Tunashangaa Serikali kuja na kuanza kuvunja nyumba zetu bila hata kutulipa fidia.”

Wapangaji watambuliwe
Akiwa katika eneo hilo, Rais Kikwete alipingana na uamuzi wa Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Said Meck Sadiki ya kutowatambua wapangaji waliokumbwa na mafuriko mabondeni na kutaka watu hao kufikiriwa na kupatiwa viwanja akisema nao ni Watanzania kama wengine.

Rais alisema hayo wakati akipokea taarifa kutoka kwa Sadiki aliyemweleza kwamba kulikuwa na mahema 300 yaliyokuwa tayari kwa ajili ya kukabidhiwa kwa waathirika wa mafuriko.

Hatua hiyo ya Rais Kikwete inakuja baada ya waliokuwa wa wapangaji walioathiriwa na maafa hayo kukataliwa na kamati hiyo kupewa viwanja.

Rais Kikwete alisema kamati hiyo ya maafa inatakiwa kutafakari kwa kina na kwamba hakuna mtu aliyepanga maafa lakini kutokana na kitu hicho kuja ghafla, lazima Serikali isimamie shughuli ya  kuwatunza waathirika na kwamba waathirika ambao ni wapangaji lazima wawekwe katika makundi maalumu kwa ajili ya kupewa viwanja.

“Ili kuondokana na usumbufu na wapangaji, Mkuu wa Mkoa nakuagiza kutengua maamuzi yenu hasa ya kutowapa viwanja wapangaji, maana hawa wote ni Watanzania wenzetu ambao hawakutamani kuishi hivyo,” alisema.

Aliwaonya viongozi wanaotaka kujilimbikizia viwanja akisema kazi hiyo inatakiwa kufanywa kwa makini ili kuhakikisha kuwa lawama hazitokei katika ugawaji wa maeneo hayo.

Alisema viongozi wote wanatakiwa kuweka mazingira maalumu ili  waathirika kujiwezesha badala ya kuitegemea Serikali. Alisema kazi ya kuwatambua na kuwahamisha waathirika inatakiwa kufanywa kwa umakini ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza.

“Kazi hii ifanyike kwa umakini ili kuondoa migogoro. Nyumba zote zihesabiwe na kila mtu apewe namba kabla ya kufika Mabwepande. Baada ya kupewa namba ahamishwe na nyumba ibomolewe ili kuondoa migogoro ya kulipwa mara mbili,” alisema.

Aliwataka wathamini kuzipiga picha nyumba zote na kuziweka katika kumbukumbu ili kuhakikisha kila anayedai fidia au kutopewa kiwanja ana takwimu ambazo zinaonyesha makazi yake.

Maji na Umeme
Rais Kikwete alionyeshwa kusikitishwa kwake na takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) juu ya upatikanaji wa maji.

Alionekana kukerwa baada ya kuwauliza maswali viongozi hao ambao walishindwa kumpa majibu kwa ufasaha na kuonekana kutupiana mpira. Alisema majibu waliyokuwa wanayatoa hayaonyeshi kwamba kuna hatua za haraka za kutatua tatizo la maji.

Alisema kila siku lazima lita 50,000 za maji zijazwe kwenye matanki kutokana na mahitaji muhimu ya wananchi na kuwataka wahusika kuwa makini.

Aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Mipango Miji, kutenga maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya masoko, viwanda na huduma muhimu ili kuzuia msongamano mjini.

Alisema neno dharura lisitumike kuweka miundombinu mibovu na badala yake Mabwepande itumike kama mfano katika kuliweka jiji la Dar es Salaam katika mpangilio wa kisasa.Kuhusu umeme, Rais Kiwete alisema Serikali kupitia ofisi ya mkoa itahakikisha wananchi hao wanapatiwa huduma ya umeme.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa kupitia kwa Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, Sh550 milioni zinahitajika ili kufanikisha huduma ya umeme eneo hilo.Alisema kazi hiyo inatarajia kuanza wiki ijayo na kukamilika baada ya wiki mbili.

Mvutano Msalaba Mwekundu na CCM
Mvutano uliibuka kati ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania baada ya kutakiwa kuondoa bendera na alama zilizofungwa katika mahema kilichoyajenga kwa ajili ya waathirika hao.Mvutano huo ulianza juzi baada ya uongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kutaka mabango hayo kuondolewa lakini uongozi wa Msalaba Mwekundu ulikataa.

Mmoja wa maofisa wa Msalaba Mwekundu alisema hatua hiyo ya kukataa kutoa alama hizo inatokana na ubaguzi uliofanywa wa kutotaka kukihusisha chama chake kwenye ziara ya Rais Kikwete.
Alisema chama hicho ndicho kilichokuwa na mamlaka ya kukabidhi mahema hayo kwa Rais au kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Taarifa zilizopatikana eneo hilo zilieleza kwamba kulikuwepo na njama za kuonyesha kwamba mahema hayo hayakujengwa na Msalaba Mwekundu, bali ni juhudi za Serikali. Kwa mujibu wa taarifa hizo, Msalaba Mwekundu kilitumia karibu Sh70 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mahema hayo.

No comments:

Post a Comment