Friday, January 13, 2012

Mauaji ya kisasi Sudan Kusini


Mauaji ya kisasi Sudan Kusini

 13 Januari, 2012 - Saa 11:37 GMT
Murle
Mwanamke wa kabila la Murle
Watu wapatao 57, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa katika mashambulio ya kulipiza kisasi Sudan Kusini, wanasema maafisa.
Waziri wa Habari Barnaba Marial Benjamin amesema watu wa kabila la Murle waliwashambulia mahasimu wao wa kabila la Lou Ner katika jimbo la Joglei.
Mapema mwezi huu, wapiganaji wapatao 6,000 wa kabila la Lou Nuer walifanya ghasia na kusababisha maelfu ya watu wa kabila la Murles kukimbia makazi yao.
Jamii hizo mbili zimekuwa na historia ya muda mrefu ya kuibiana mifugo.
Watu takriban 1,000 wameuawa katika kipindi cha mwaka uliopita.
Kufuatia mashambulio ya hivi karibuni, wanajeshi wa ziada wa kulinda amani Umoja wa Mataifa walipelekwa haraka katika eneo hilo na wakati huohuo jimbo la Joglei kutangazwa kuwa eneo la majanga.
Umoja wa Mataifa umeanzisha "shughuli kubwa ya dharura" kusaidia watu 50,000 walioathirika na kuukimbia mji wa Pibor.
Bw Benjamin amesema wengi wa waliouawa katika siku za hivi karibuni walikuwa wanawake na watoto kwa sababu mashambulio hayo yalifanywa jioni na usiku, wakati wengi walikuwa wamelala katika vibanda vyao.
Mwandishi wa habari Hannah McNeish aliyepo katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, amesema watu wengi wanajiuliza kwa nini Umoja wa Mataifa na hata wanajeshi wa nchi wameshindwa kuzuia mashambulio haya kutokea.
Lakini Umoja wa Mataifa unasema ukubwa wa jimbo la Joglei ni sawa na nchi ya Bangladesh na kuwa wanajeshi wa kulinda amani hawawezi kuwepo kila sehemu kwa wakati mmoja.
Wizi wa mifugo ni jambo la kawaida Sudan Kusini, na hata mapigano kati ya makabila hasimu. Umoja wa Mataifa unasema watu 350,000 walipoteza makazi yao mwaka jana kutokana na mapigano ya kikabila mwaka jana.
Hii ni changamoto kubwa kwa serikali ambayo imepata uhuru wake hivi karibuni, ambayo pia inakabiliwa na mvutano wa mpaka na nchi jirani ya Sudan.
Sudan Kusini ni moja ya nchi masikini zaidi duniani - ilipata uhuru wake kutoka Sudan Julai 2011 na haina barabara, reli, shule au hata zahanati kutokana na miongo kadhaa ya mapigano.

No comments:

Post a Comment