Friday, January 6, 2012

Boko Haram washambulia Maiduguri


Kanisa lashambuliwa Nigeria

 6 Januari, 2012 - Saa 03:54 GMT
Nigeria
Nigeria
Maafisa wa polisi nchini Nigeria wamesema kuwa watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki wamewauwa watu watatu katika shambulio kwenye kanisa moja, katika mji wa Gombe ulioko kaskazini mashariki mwa nchi.
Mchungaji wa kanisa hilo John Jauro amesema waumini wa kanisa hilo walishambuliwa wakati wa sala za jioni.
Mchungaji huyo wa kanisa la Deeper Life amesema mke wake ni miongoni mwa watu waliouawa.
Waumini wengine 10 walijeruhiwa na genge hilo lililokuwa limejihami katika jimbo la Gombe, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Boko haram kushukiwa kuhusika

Bado haijulikana aliyetekeleza shambulio hilo lakini kwa kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita, kundi la kiislamu la Boko Haram, limekuwa likishambulia makanisa nchini humo.
Kundi hilo la Boko Haram ambalo limeharamishwa limewataka wakristo kuondoka kaskazini mwa nchi hiyo.
Serikali imetangaza hali ya hatari katika maeneo kadhaa ya kaskazini mwa Nigeria.
Hapo jana washukiwa wawili wa kundi la Boko Haram walikamatwa, baada ya mwanamme mmoja na mwanawe kuuawa mjini Maiduguri, karibu na jimbo hilo la Gombe.

Boko Haram washambulia Maiduguri

 5 Januari, 2012 - Saa 04:37 GMT
mashambulizi yalioyotekelezwa na Boko Haram
mashambulizi yalioyotekelezwa na Boko Haram
Mashambulio mawili ya mabomu yametokea katika mji wa Maiduguri kaskazini mwa Nigeria yakiwa ndio machafuko ya kwanza kutokea tangu kutangazwa kwa hali ya hatari mjini humo.
Hakuna majeruhi yaliyoripotiwa katika ghasia hizi zinazodhaniwa kutekelezwa na wapiganaji wa kundi la kiislam lilopigwa marufuku la Boko Haram.
Kundi hilo linawataka waumini wa dini ya kikristo kutoka kusini mwa nchi hiyo waishio kaskazini mwa nchi kuondoka mara moja.

msichana auawa

Awali, msichana mmoja aliuawa wakati wa ufyatulianaji wa risasi katika ya wapiganaji wanaoaminika kuwa wa kundi hilo la Boko Haram na maafisa wa polisi katika jimbo la Jigawa.
Jumapili iliyopita kundi hilo la Boko Haram lilitoa makataa kwa watu kutoka jamii ya wakristo kusini mwa Nigeria, waondoke maeneo ya Kaskazini mwa nchi.
Rais Goodluck Jonathan ametangaza hali ya hatari katika majimbo manne nchini humo.

mgomo juu ya ruzuku ya mafuta

Mashambulio hayo yanatokea huku maandamano kupinga kuondolewa kwa ruzuka ya mafuta ya petroli yakiendelea.
Katika eneo la Liberation Square mjini Kano , maafisa wa polisi nchini humu wametumia gesi ya kutoa machozi na virungu kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wakiandamana katika eneo lilowazi kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yameshutumu kitendo hicho cha polisi.
Aidha, Raia nchini humo wamechukizwa na tangazo la serikali hapo Jumapili kwamba itaondolewa ruzuku hiyo ambayo inaigharimu serikali mamilioni ya dola katika mapato.

No comments:

Post a Comment