Friday, January 6, 2012

Makada CCM, CUF, NCCR wafungua kesi ya kikatiba


Makada CCM, CUF, NCCR wafungua kesi ya kikatiba  Send to a friend
Friday, 06 January 2012 20:00
0digg
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
Waandishi Wetu
WANANCHI wa Jimbo la Kigoma Kusini wamefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam wakiiomba  iamuru kusitishwa kwa matumizi ya Ibara ya 71 (1) (f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano juu ya mbunge aliyefukuzwa uanachama katika chama chake.

Pia wapiga kura hao wameiomba Mahakama iliamuru Bunge litunge sheria inayoruhusu mbunge aliyefukuzwa uanachama katika chama chake atambuliwe kuwa mbunge huru au aruhusiwe kuhama na ubunge wake kwenda chama chochote atakachotaka.

Kesi hiyo imefunguliwa siku chache tangu Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila avuliwe uanachama wa NCCR-Mageuzi, hatua ambayo kikatiba inamvua ubunge wake. Kafulia alivuliwa uanachama Novemba 20, mwaka jana. Hata hivyo, amefungua kesi kupinga hatua hiyo.

Kadhalika, siku tatu zilizopita, Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), lilimvua uanachama wa chama hicho Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed hatua ambayo inamfanya apoteze nafasi yake ya ubunge.

Jana, CUF waliwasilisha barua katika Ofisi ya Spika wa Bunge, kumwarifu kuhusu uamuzi wa kumvua uanachama Hamad, huku mbunge huyo akisema uamuzi wa huo ni batili kwani ulikiuka amri ya mahakama iliyokuwa ikizuia kufanyika kwa kikao chake.

Kesi ya Kikatiba
Wapiga kura watatu wa Kigoma Kusini ndiyo waliofungua kesi hiyo ya kikatiba na kila mmoja anatoka katika chama tofauti cha siasa. Mmoja ni mwanaCCM, mwingine CUF na wa tatu anatoka NCCR Mageuzi. Walifungua kesi hiyo kwa niaba ya wananchi wengine wa jimbo hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mlalamikaji wa kwanza katika kesi hiyo ya Kikatiba Namba 1 ya mwaka 2012 ni Juma Shaban Nzengula ambaye ni mwanachama wa CCM tangu mwaka 1980, mwenye kadi ya uanachama namba Aa 581252 ya Februari 5, 2003. Nzengula pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Mkoa wa Kigoma akitokea katika Kata ya Nguruka.

Mlalamikaji wa pili ni Patrick Haruna Rubilo, mwanachama wa NCCR-Mageuzi mwenye kadi ya uanachama namba 045845 ya 2000, pia akiwa Mjumbe wa Kata ya Itebula na Mwenyekiti wa Kijiji cha Bweru.

Mlalamikaji wa tatu ni Fanuel Misigalo Bihole, mwanachama wa CUF mwenye kadi ya uanachama namba 1145401 ya Agosti 17, 2004 ambaye pia ni Katibu wa Wazazi wa Kata ya Mtegowanoti.

Kwa mujibu wa hati ya madai waliyoiwasilisha mahakamani hapo, walalamikaji hao kupitia Kampuni ya Uwakili ya Mpoki & Associates, Ibara hiyo inakiuka haki za msingi zinazoelezwa katika Ibara ya 21 ya Katiba.

Ibara hiyo inatoa uhuru wa kushiriki katika shughuli za umma kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa mujibu wa sheria.
Pia wanadai kuwa Ibara hiyo inakiuka Ibara ya 201 (1) ya Katiba inayotoa uhuru kwa wananchi kushiriki na kutoa maoni kwa uwazi, na kwamba pia inakiuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu ambao Tanzania imeuridhia na kuusaini.

“Matokeo ya Ibara hiyo ni kwamba kuna uwezekano kwamba mbunge wetu tuliyemchagua kwa kura nyingi anaweza kupoteza ubunge wake kwa matakwa ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya NCCR- Mageuzi ambao ni chini ya 30.”

Kauli za wadai
Wakizungumza baada ya kufungua kesi hiyo, walalamikaji hao walisema licha ya kwamba wanatoka vyama tofauti vya siasa uamuzi wao umejengwa katika msingi wa matukio ya kufukuzwa kwa Kafulila na Hamad Rashid.

“Mimi ni mwanachama wa CCM na nilikuwa na mgombea wangu, lakini baada kuchaguliwa mbunge anakuwa ni mbunge wa umma. Kafulila alichaguliwa na wananchi 23,162,” alisema Nzengula.

Kwa upande wake Rubilo alisema mbunge anafunga mkataba na wananchi na kwamba huwa wanatoa ahadi nyingi katika kutekeleza mkataba huo kama vile kusomesha watoto na shughuli nyingine za maendeleo... “Sasa anapovuliwa uanachama na kupoteza ubunge hizo shughuli zitakwama...” alisema Rubilo na kuungwa mkono na Bihole.

Walalamikaji hao walitoa wito kwa watu wengine akiwamo Hamad Rashid wawaunge mkono katika kesi hiyo. Walisema ingawa wao ni wakazi wa Kigoma, wameamua kufungua kesi hiyo Mahakama Kuu Dar es Salaam kwa kuwa hoja yao si ya kijimbo, bali ni ya kitaifa na kwamba itawanufaisha Watanzania wote.

CUF kwa Spika
CUF kimewasilisha barua ya kumvua uanachama mbunge wa Wawi, Hamad Rashid katika Ofisi za Bunge. Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Julius Mtatiro alisema barua hiyo ilipelekwa jana katika Ofisi za Bunge Dar es Salaam na kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Bunge imesema haijapokea barua ya amri ya Mahakama Kuu kuzuia uamuzi wa NCCR-Mageuzi kumvua uanachama Kafulila.

Kaimu Katibu wa Bunge, Eliakim Mrema alisema ofisi yake haijapata barua yoyote kutoka mahakamani inayofafanua amri hiyo... “Hakuna barua kama hiyo hapa ofisini kwetu… labda uiulize mahakama kama imeshatoa hiyo barua.”

Hata hivyo, Kafulila akizungumza kwa simu akiwa Kigoma alisema: “Msajili wa Vyama vya Siasa (John Tendwa) alieleza kuwa barua ya Mahakama inaweza kupelekwa katika Ofisi za Bunge na chama chenyewe (NCCR) au mimi (Kafulila) na ndivyo nilivyofanya.”

Alisema kazi ya mahakama ni kutoa amri baina ya chama na mwanachama na si kupeleka barua katika Ofisi ya Bunge.”

Katibu Mkuu wa NCCR, Samwel Ruhuza alisema hawawezi kupeleka barua hiyo katika Ofisi za Bunge kwa kuwa amri hiyo haikukitaka kibatilishe uamuzi wake dhidi ya Kafulila... “Mahakama imesema kama chama, tusijadili wala kutoa uamuzi wa jambo lolote linalomhusu Kafulila… haikusema kama haitambui uamuzi ya chama.”

Katika hatua nyingine Mbunge wa  Bukoba Vijijini (CCM), Johnson Rweikiza amesema maslahi ndicho chanzo cha vyama vya upinzani kufukuzana uanachama.“Haya yanaonyesha dhahiri namna viongozi walivyo na uchu wa madaraka na si kuwajibika kwa ajili ya jamii,” alisema Rweikiza

Habari hii imeandikwa na James Magai, Fidelis Butahe na Geofrey Nyang’oro

No comments:

Post a Comment