Wednesday, January 4, 2012

SIKU 75 BAADA YA KIFO CHA GADDAFI




Mwandishi Wetu na Intaneti
Ilishaonywa kuwa Libya haiwezi kuwa na amani baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wao, Muammar Gaddafi na sasa hali ya hatari imeanza kujionesha kutokana na hasira kali walizonazo wananchi.
Siku 75 zimepita tangu Gaddafi alipokamatwa, kuteswa na kuuawa kabla ya kuzikwa kwa siri, lakini sasa imeibuka hali ya hatari kutokana na wananchi wa Libya kuanza kudai damu ya kiongozi huyo aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 42.
Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Wyre Davies, aliandika ripoti ya uchunguzi wake nchini Libya baada ya kifo cha Gaddafi kuwa Jiji la Sirte, limetanda giza ya chuki dhidi ya Serikali ya Baraza la Mpito (NTC).
Katika ripoti yake, iliyohusisha mahojiano na wananchi waliokuwa tayari kwa mapambano, wakazi wa Sirte wametoa agizo kwenda NTC kuwa ni lazima waoneshe kaburi la Gaddafi pamoja na la mwanaye, Muttasim ambaye alizikwa naye siku moja.
Ripoti hiyo ilieleza pia kuwa wananchi wanataka damu ya Gaddafi ifidiwe, vinginevyo Libya haitakalika abadan!
 Mwandishi huyo aliandika kuwa chuki ya wananchi wa Sirte ni kubwa kwa NTC kutokana na maelezo wanayotoa kwamba Gaddafi alikuwa anapambana kuwalinda, wakati waasi wakisaidiwa na vikosi vya Jeshi la Kujihami la Nchi za Magharibi (Nato), waliendesha mauaji ya raia bila tahadhari.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sirte, Dk. Ahmed Hassan, amezungumza ndani ya ripoti hiyo kuwa maisha ya Walibya yameharibika kwa kiasi kikubwa.
Alisema, enzi za Gaddafi alisaidia maeneo mengi ya kimaisha kwa wananchi wa Libya lakini sasa hivi imekuwa tofauti.
“Gaddafi alitusaidia makazi, wao NTC wameyaharibu. Gaddafi alitulinda raia wa Libya, NTC wameua raia, hawafai hata kidogo,” alisema Dk. Hassan ambaye yeye na familia yake yenye mke na watoto watano, wanaishi kwenye hema baada ya nyumba yao kuharibiwa na milipuko ya mabomu.
Alihoji: “Nitazame, mimi ni mhadhiri wa chuo kikuu hapa. Nilifanya kosa gani mpaka nikastahili maisha haya mabovu?”
Dk. Hassan alifafanua kuwa Walibya walikuwa wanaishi kwa amani, matumaini, furaha na upendo lakini NTC wamevuruga misingi yote bora iliyowekwa na Gaddafi.
“Kwa sasa mimi sijali. Tutaona kitakachotokea. Sioni kitu kinachoweza kunishawishi kuamini kwamba NTC wataifanya Libya kuwa mpya yenye matumaini,” alisema.
Katika ripoti hiyo, mwandishi huyo wa BBC ameeleza kwamba hasira za wananchi na mgawanyiko uliopo, vinafanya amani na umoja wa kitaifa wa Libya viwe ni ndoto kupatikana.
Imezidi kuelezwa kwenye ripoti hiyo kwamba wananchi wao kwa wao wamegeukana, wale waliokuwa wanaunga mkono NTC wanachakazwa na wengi ambao hawakukubaliana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya Gaddafi.
Inaelezwa kuwa NTC kwa kulitambua hilo, imekuwa ikiingilia kati na kuwadhibiti wananchi waliokuwa wanaamini katika huduma ya Gaddafi.
Inabainishwa kuwa wananchi 30,000 wanaoishi kwenye mji wa kaskazini ya Jiji la Mistrata, wametimuliwa kwenye makazi yao, hivyo hawana makazi kwa sasa.
Msichana, Najia Waks, mkazi wa jiji hilo la tatu kwa ukubwa Libya, alisema kuwa wapiganaji wa NTC wamewafanyia udhalilishaji wa hali ya juu, kwa hiyo hawatawasamehe hata kidogo.
“Hawawezi kujirudi na hawawezi kuja tena. Wametufanyia mambo mengi ya kuumiza. Ni mambo ya kutisha mno.
“Wamebaka wanawake, vijana walichukuliwa usiku na mpaka sasa hawajulikani walipo,” alisema Najia, mwenye asili yake kwenye Mji wa Tawergha, Mistrata.
Mwanamke, Umm Saber, akiwa kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Ghost, alisema, Libya hakuna amani na hali iyopo sasa hivi, nchi haina msimamizi sahihi.
“Tunanyanyasika tu na kuteswa. Wanawake tunageuzwa watumwa wa ngono na wapiganaji wa NTC kwa sababu hawana maadili. Ona maisha yalivyokuwa magumu na bei za vitu zimepanda, wakati Gaddafi alirahisisha bei za bidhaa.
“Alilipa marupurupu na mishahara hata kwa wasio na kazi. NTC hatuoni hayo. Tunaambiwa inajengwa Libya mpya yenye umoja na amani, hayo mbona hayatekelezwi, badala yake tunashuhudia ukandamizaji na utesaji wa wananchi?
“Ikijulikana kuna sehemu watu walikuwa wanamuunga mkono Gaddafi wanauawa, tunakwenda wapi? Bila shaka NTC ni wahalifu wa kivita. Mimi nitaungana na wanaharakati watakaojitoa kudai damu ya Gaddafi, tutapambana usiku na mchana,” alisema Umm.
Gaddafi, aliuawa Oktoba 20, 2011 baada ya kukamatwa na wapiganaji (waasi) wa NTC kwa kushirikiana na Nato.
Kukamatwa kwa Gaddafi kulikuja baada ya mapigano ya muda mrefu kati ya waasi wakisaidiwa na Nato dhidi ya kiongozi huyo aliyekuwa amegoma kuachia madaraka.

No comments:

Post a Comment