Ethiopia kuondoka Somalia
6 Januari, 2012 - Saa 13:16 GMT
Ethiopia itaondoa wanajeshi wake
katika maeneo ambayo imeyateka hivi karibuni nchini Somalia, na nafasi
ya majeshi yake kuchukuliwa na wanajeshi wa Umoja wa Afrika.
Uamuzi huo umefikiwa na Baraza la Usalama na
Amani la Umoja wa Afrika, waliokutana kukamilisha uongezaji nguvu wa
jeshi la kulinda amani nchini Somalia.Wanajeshi wa Ethiopia waliingia Somalia mwezi Oktoba kuwasaka wanamgambo wa al-Shabaab, ambao wanadhibiti zaidi eneo la kusini mwa nchi hiyo.
Kundi hilo linalohusishwa na kundi la al-Qaeda sasa linapambana na wanajeshi wa Kenya na Ethiopia, na hata makundi madogo ya wapiganaji wa Kisomali.
Serikali ya mpito ya Somalia inayosaidiwa na Umoja wa Mataifa inadhibiti mji mkuu wa Mogadishu pekee hasa kutokana na msaada wa majeshi ya Umoja wa Afrika (Amisom).
Ethiopia, awali ilipeleka wanajeshi nchini Somalia mwaka 2006 kuwan'goa wapiganaji wenye itikadi kali, lakini wanajeshi hao waliondoka mwaka 2009 baada ya kupoteza wapiganaji wengi.
Kuwepo kwa wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia kuna utata kwa sababu nchi hizo mbili zimekuwa zikipigania mpaka tangu miaka ya 1970.
Somalia haijakuwa na serikali thabiti kwa zaidi ya miaka 20 na imeghubikwa na mapigano baina ya makundi ya kikoo nchini humo.
Umoja wa Afrika umesema mipango yake ya kuimarisha jeshi la Amisom litahanikiza kukomboa maeneo zaidi.
Wanajeshi wa Amisom wanachukua "maeneo yaliyokombolewa kwa msaada wa Ethiopia, kutokana na uharaka wa kutaka kuondoka kwa wanajeshi wa Ethiopia katika maeneo hayo", imesema taarifa.
Djibouti pia itapeleka wanajeshi wapatao 5,700 kujiunga na wanajeshi wa Amisom. Awali ilikuwa ipeleke wanajeshi 1,500. Tayari wanajeshi 200 wamewasili mjini Mogadishu, imesema AU.
Hakuna chochote kilichotajwa kuhusu wanajeshi 1,500 walioahidiwa kutoka Sierra Leone.
No comments:
Post a Comment