Tuesday, April 3, 2012

Siri ya ushindi wa Chadema Arumeru

Siri ya ushindi wa Chadema Arumeru  Send to a friend
Monday, 02 April 2012 21:44
0digg
Mbunge Mteule wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akiwapungia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Leganga, kwaajili ya kuwashukuru kwa kumchagua. Picha na Edwin Mjwahuzi
USHINDI wa Chadema katika Jimbo la Arumeru Mashariki na kata tatu za udiwani, umezidi kukiweka pabaya, CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku sababu za ushindi huo zikitajwa kuwa ni matumizi mazuri ya kasoro za chama hicho tawala katika mambo mbalimbali.

Chadema kimepata ushindi katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki baada ya mgombea wake, Joshua Nassari kuwashinda wenzake saba katika kinyang’anyiro hicho.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hii kwa chama cha upinzani kushinda uchaguzi mdogo katika jimbo ambalo kabla halijawa wazi kwa sababu zozote zile, lilikuwa mikononi mwa CCM.

Arumeru Mashariki limekuwa wazi tangu mwanzoni mwa mwaka huu baada ya aliyekuwa mbunge wake, Jeremia Sumari (CCM), kufariki dunia.

Nassari ameshinda kwa asilimia 54.91 wakati mpinzani wake wa karibu, Sioi Sumari wa CCM alipata asilimia 44.56 ya kura halali 60,038 zilizopigwa katika vituo 327 vya kupigia kura.

Sababu za ushindi
Chadema kiliingia katika kinyang’anyiro hicho kwa kujishusha hivyo kupata muda wa kujifunza jinsi ya kwenda kuishi na wananchi wa Arumeru kwa maana ya kufahamu lugha ya kuzungumza nao, kutambua mahitaji yao, kisha kutafuta majawabu ya kuwapa juu ya mahitaji hayo.

Kilijenga timu imara ya kuratibu kampeni zake kwa ufanisi, na jukumu hilo liliangikia kwa watu watatu, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse na Meneja mwenza wake, Vicent Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini na Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge, John Mrema ambaye alipewa jukumu la kusimamia oparesheni zote.

Nyerere pia alichukuliwa kama kete ya Chadema kuwashawishi wananchi wa Arumeru ambao wanaaminika kuwa waumini wa siasa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kupata uthibitisho kwamba hata katika familia yake, wapo watu wa upinzani.

Licha ya CCM kutuma timu nzito ya vigogo katika kampeni zake, Mwenyekiti na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Mlezi wa CCM Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uratibu na Uhusiano, Stephen Wassira, Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye bado mgombea wake aliangushwa.

Hata hivyo, uchaguzi huo umefanyika wakati CCM kikiwa katika mpasuko mkubwa ambao umechangiwa na siasa za makundi. Makundi hayo ni ya vigogo wa chama hicho, ambao wanajipanga kuwania Urais mwaka 2015 na kwa sasa kila kundi linaendesha mipango wa kujiimarisha katika kila eneo muhimu kuanzia ngazi za chini.
Ishara za kushindwa
Ishara za kushindwa CCM zilianza kuonekana katika mchakato wa mwanzo wa kura za maoni ndani ya chama hicho, kwani wanachama ambao walijitokeza kugombea na kushindwa, wengi wao hawakuvunja kambi zao.
Makundi yaliyokuwa na nguvu ni yale yaliyokuwa na makada wa chama hicho, William Sarakikya, Elirehema Kaaya na Elishiria Kaaya ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM Mkoa wa Arusha.
Pia siasa za makundi ndani ya CCM Mkoa wa Arusha, ambako bado vigogo wa chama hicho, hasa Katibu wa Mkoa, Mary Chatanda na Mwenyekiti wake, Onesmo Nangole hawana uhusiano mazuri kunaelezwa kuwa ni moja ya sababu za kuanguka.
Awali, Chatanda ambaye anadaiwa kuwa na mgogoro na wana-CCM wengine wa Arusha, alitajwa kumpinga waziwazi Sioi katika kura za maoni na alimpa karata yake Sarakikya na Elishilia Kaaya ambao wote walishindwa.
Pia wanasiasa waliotumika katika kampeni za CCM katika uchaguzi huo mdogo ni moja ya mambo ambayo yalikiathiri chama hicho.
Lugha zilizokuwa zikitumiwa na baadhi yao dhidi ya viongozi wa juu wa Chadema na wabunge wake kwa mfano, alizokuwa akimwaga jukwaani, mpiga kampeni nguli wa wake, Livingstone Lusinde ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), ni moja ya mambo yanayooelezwa kuwa yalichangia kupunguza kura za mgombea wa chama hicho.
Pia kuhujumiana ndani ya chama kwa kuvujisha taarifa za vikao vya siri vya mikakati ya ushindi, kiasi kikubwa kumechangia chama hicho kushindwa kwa tofauti ya zaidi ya kura 6,000.
Moja ya mambo ambayo yanadaiwa kutoka ndani ya CCM, ni siri ya kuongeza vituo vya kura, mpango wa kubadilishwa baadhi ya matokeo ya fomu za mawakala, kuingizwa kura bandia kupitia mabalozi wa nyumba kumi katika vituo mapema alfajiri na pia, kuhongwa kwa baadhi ya mawakala.
Mipango hiyo inadaiwa kukwama hata kabla ya siku ya kupiga kura hali ambayo inadaiwa kuwa iliichanganya kambi ya CCM.
Hata katika upangaji wa ratiba ya kampeni na wazungumzaji katika kampeni hizo, kunadaiwa kulikuwa na hujuma miongoni mwa wazungumzaji huku kundi moja likituhumiwa kufika katika jimbo hilo, kuhujumu kampeni kwa kutoa lugha ambazo haziwapendezi wananchi na hivyo kuwachukiza.
Sababu nyingine ni gtuhuma za ufisadi zinazowakabili baaadhi ya makada wa chama hicho. Hilo limewafanya baadhi ya wananchi kukichukia wakiamini kuwa mafisadi ambao hupigwa vita na Chadema ndiyo chanzo cha umaskini mkubwa unaowakabili Watanzania.

Kampeni

Uzinduzi wa kishindo wa kampeni za chama hicho ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Star, Machi 10, mwaka huu uliashiria kwamba Chadema kilikuwa kimedhamiria kushinda.

Mbali na shamrashamra za hapa na pale, mkutano wa uzinduzi ulipanga ajenda za kampeni za chama hicho na aliyekuwa mgombea, Nassari na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe waliweka bayana kwamba suala la ardhi ni miongoni mwa mambo ambayo yatapewa umuhimu mkubwa.

Ajenda nyingine ambayo pia iliwekwa wazi na Nassari ni matatizo ya maji katika maeneo mengi ya jimbo hilo ambalo kuna chanzo kikuu cha maji kwa Miji ya Arusha na Monduli.

Ajenda hizo za ardhi, maji na nyingine pia zilibebwa na timu za kampeni wabunge wa chama hicho ambao walikuwa wakifika nyumba hadi nyumba mbali na mikutano ya hadhara vijijini.

Matumizi ya helkopta katika siku tisa za mwisho za kampeni, yalimwezesha Nassari na timu yake ya kampeni kuwafikia wananchi wengi zaidi katika muda mfupi sambamba na kuongeza hamasa kwa maana ya kuwa sehemu ya kushawishi watu kufika kwenye mikutano katika sehemu mbalimbali.

Viongozi wakuu wa Chadema, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa walikuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha ushindi wa Nassari.

Kulikuwa na kila dalili kwamba viongozi hawa wanakubalika na kuaminika kwa wananchi kwani kila walipofika na kuhutubia, idadi ya watu ilikuwa kubwa na utulivu ulionekana kuwa wa hali ya juu.

Uwepo wa viongozi hao ulimwongezea nguvu kubwa mgombea wao ambaye pia alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza akitumia lugha rahisi kuzungumzia matatizo yanayowagusa watu katika eneo husika.

Ni kama alikuwa amefanya utafiti wa kila alikokweda, kwani hotuba katika kijiji kimoja haikuwa na uhusiano na hotuba ambayo angeitoa katika kijiji kilichofuata.

Kauli za mgombea huyo kuhusu maisha duni ya watu hasa kina mama ambao wamekuwa wakitozwa ushuru kwenye magulio, kukemea uonevu unaofanywa na walowezi kwenye mashamba makubwa na kuzungumzia kwa ufasaha mahitaji mengine ya wananchi kulimfanya kueleweka kwa urahisi kwa watu wa kawaida.

Lakini pia Nassari alikwepa kuingia kwenye mitego ya kujibu tuhuma mbalimbali zilizorushwa kwake na wapinzani wake hasa CCM na mara zote alikuwa akisema: “Mimi namwachia Mungu.”

Nassari aliingia kwenye uchaguzi huo kwa mara ya pili baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010 ambako alipambana na marehemu Sumari na kupata kura zaidi ya 19,000.

Udhaifu wa CCM
Timu ya kampeni ya Chadema ilimsaidia Nassari kutumia udhaifu wa CCM katika kufanikisha malengo yake.

Siasa za matusi majukwaani ambazo baadhi ya wapiga debe wake walizitumia hazikupata majibu kutoka Chadema na badala yake, Nassari alitumia msemo: “Tulianza na Mungu na tutamaliza na Mungu.”

Majibu ya baadhi ya tuhuma dhidi ya Chadema na mgombea wake yaliyotolewa na watu ambao si sehemu ya chama hicho yalikijenga zaidi. Mathalan, Kanisa Katoliki lilitoa tamko kwamba halijawahi kumtuhumu Dk Slaa kuhusu wizi wa fedha kama ilivyodiwa na CCM.

Mengine ni kauli ya mtoto wa kwanza wa Hayati Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere kwamba Vicent Nyerere ni ndugu yao tofauti na madai ya Rais Mstaafu Mkapa kwamba hakuwahi kumfahamu, huku wazazi wake Nassari wakijitokeza jukwaani kupinga kile kilichosemwa na Wassira kwamba mgombea huyo wa Chadema hakuwa na baraka za wazazi wake kugombea nafasi hiyo.

Kauli hizo ziliwafanya makada wa CCM waonekane kuwa si wa kweli mbele ya umma na hata yaliyosema baadaye yalichukuliwa na baadhi ya watu kuwa ni uzushi na uongo.

Maoni ya wadau
Wasomi na wanasiasa nchini wamesema ushindi huo wa Chadema ni fundisho kubwa kwa CCM kwamba watu sasa wanataka mabadiliko.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema huo ni ushindi mkubwa kwa wananchi wanaopenda mabadiliko.

“Hii ni ishara kwamba watu wanaotaka mabadiliko hapa nchini watawashinda watu wasiotaka mabadiliko, Arumeru Mashariki ni sehemu tu ya mabadiliko hayo,” alisema Dk Mkumbo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Alisema hata kwenye chaguzi nyingine za kata katika Mikoa ya Mwanza, Mbeya na Tanga wananchi wameonyesha kuwa wanataka mabadiliko.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya alisema wananchi wa Arumeru Mashariki wameipelekea CCM ujumbe kupitia masanduku ya kura.
“Wamekiambia chama tawala kupitia ujumbe wa kura kwamba hawaridhishwi na hali ngumu ya maisha wanayoishi hivi sasa,” alisema Nkya.

Alisema wananchi hao wamechoshwa na ahadi za uongo ambazo zimekuwa zikitolewa kila baada ya miaka mitano na sasa wanataka mabadiliko.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alikipongeza Chadema na kusema kwamba uchaguzi huo unaonyesha kwamba wananchi hivi sasa wanataka mabadiliko.
Hata hivyo, Mtatiro alisema wakati umefika sasa kuweka utaratibu wa kuzuia uwepo wa chaguzi ndogo kwa sababu zinatumia fedha nyingi za walipakodi.

“Tuandae utaratibu wa kuachana na chaguzi ndogo zinatumia fedha nyingi. Wenzetu Msumbiji na Ghana wameacha mfumo huo, mbunge anapofariki chama kinatoa mbunge mwingine bila ya kuitishwa kwa uchaguzi,” alisema.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema ni vyema vyama vilivyoshinda na kushindwa vikafanya utafiti ili kufahamu nini cha kufanya hapo baadaye.
“Hata chama kilichoshinda ni vizuri kikafanya utafiti wa kwa nini kimeshinda uchaguzi huo ili kiweze kuendeleza sababu hizo za kushinda,” alisema.

Alisema ni vyema utafiti ukafanyika ili kufahamu ni kwa nini hivi sasa katika mfumo wa vyama vingi idadi ya wananchi wanaopiga kura ni ndogo.

“Wakati wa mfumo wa chama kimoja watu wengi walijitokeza kupiga kura kuliko sasa katika mfumo wa vyama vingi ni lazima tufahamu kwa nini?”
Mkutano wa shukrani

Jana, maelfu wa wakazi wa Arumeru Mashariki, walijitokeza katika mkutano wa uliofanyika kwenye Uwanja wa Leganga ambao chama hicho kilizindulia kampeni zake, kumpongeza Nassari kwa ushindi huo.

Mamia ya watu, wengi wao wakiwa vijana walitembea kwa miguu hadi uwanja ni hapo wakitokea katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo na Arusha Mjini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe aliwashukuru wakazi wa jimbo hilo, kwa imani kubwa na heshma waliyokipa chama chake kwa kumchagua, Nassari kuwa mbunge wao.

"Tunajua mlipata shida nyingi, mmekanwa sana, mmepigwa mabomu, mmekamatwa lakini mkasema lazima mtamchagua kijana wenu kuwa mbunge,”alisema.

Aliwataka vijana wenye shahada kuzitunza kwa ajili ya uchaguzi ujao na wale ambao hawana wahakikishe wakati wa kujiandikisha kwenye daftari jipya wanajitokeza.

Kwa upande wake, Nassari alisema mara baada ya kutagazwa mshindi asubuhi, baada ya dakika 15 tu, alianza kazi ya kuhakikisha vijana waliokuwa wamekamatwa na polisi wakisherehekea ushindi wake wanaachiwa.

Imeandikwa na Neville Meena, Peter Saramba na Musa Juma, Arumeru na Raymond Kamnyoge, Dar.

s

No comments:

Post a Comment