Thursday, April 19, 2012

Magufuli augua ghafla, alazwa

Magufuli augua ghafla, alazwa  Send to a friend
Wednesday, 18 April 2012 23:06
0digg
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
Waandishi wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliugua ghafla akiwa kwenye Viwanja vya Bunge, Dodoma na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa ambako alilazwa.Taarifa za Dk Magufuli kuugua ghafla mbali na kuthibitishwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Zainab Chaula pia zilitangazwa bungeni na Naibu Spika, Job Ndugai.
Akitoa maelezo hayo muda mfupi baada ya kuanza kwa Kikao cha Bunge, Ndugai alisema Waziri Magufuli akiwa katika maandalizi ya kwenda bungeni, alijisikia vibaya ghafla na alipokimbizwa hospitali ilibainika kuwa alikuwa akikabiliwa na tatizo la shinikizo la damu.
“Waheshimiwa wabunge, Mheshimiwa Magufuli aliugua ghafla leo (jana) asubuhi na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma lakini, tunaelezwa kuwa presha (shinikizo la damu) iliyokuwa inamsumbua sasa imeshuka na kinachoendelea kumsumbua sasa ni vichomi ambavyo bado vimembana,’’ alisema Ndugai na kuongeza:
“Madaktari wanaendelea kushughulikia afya yake ili iweze kuimarika sawasawa kwa hiyo msiwe na shaka juu ya afya yake.’’
Wandishi wa habari na hata baadhi ya wabunge hakuruhusiwa kumwona Dk Magufuli hospitalini hapo na muuguzi wa zamu alisema: “Haiwezekani kumuona. Yupo katika eneo ambalo haturuhusu watu kufika na kumuona lakini anaendelea vizuri.’
Dk Chaula alisema Dk Magufuli amelazwa katika chumba maalumu ili kuwawezesha madaktari kuangalia afya yake kwa karibu… “Siyo kwamba yuko mahututi, bali tumemuweka huko kwa makusudi ya kuwa karibu naye zaidi na utulivu mzuri katika chumba hicho.”
Baadhi ya viongozi akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah walifika hospitalini hapo kwa nyakati tofauti kumjua hali waziri huyo.
Wakati Naibu Spika Ndugai akiwa hakueleza Magufuli aliugua akiwa katika eneo lipi, taarifa kutoka kwa baadhi ya watumishi wa bunge, zilieleza kuwa alipatwa na tatizo hilo asubuhi akiwa viwanja vya bunge.
Hii ni mara ya pili wabunge kuugua ghafla katika Mkutano huo wa Saba wa Bunge baada ya Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Clara Mwatuka kuugua wiki iliyopita na kupelekwa kwenye hospitali hiyo ambako alilazwa kwa siku mbili.
Mtemvu apata ajali
Katika hatua nyingine, Ndugai aliwatangazia wabunge kuwa Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu alipata ajali ya gari mkoani Morogoro na kupatiwa huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
“Napenda kuwatangazia kuwa mheshimiwa Mtemvu amepata ajali leo (jana) saa 12:15 asubuhi maeneo ya Morogoro baada ya gari lake kupinduka,” alisema Ndugai na kuongeza kuwa gari la Mtemvu lilikuwa likiendeshwa na Hussein Ally (30).
Kamanda wa Polisi Mkoani wa Morogoro, Adolphina Chialo alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka eneo la Gairo, Barabara ya Morogoro- Dodoma saa 11:00 alfajiri wakati mbunge huyo akitokea bungeni mkoani Dodoma kuelekea Dar es Salaam.
Kamanda Chialo alisema gari hilo liliacha njia na kugonga ukuta wa nyumba iliyokuwa jirani na barabara hiyo. Hata hivyo, hakuna mtu aliyejeruhiwa katika nyumba hiyo mbali ya kusababisha uharibifu.
Alisema ajali hiyo ilisababishwa na utelezi kutokana mvua iliyokuwa ikinyesha na dereva huyo kufunga breki kwa nguvu na hivyo kusababisha gari hilo kuacha njia na kupinduka.
Katika hatua nyingine, raia wa Rwanda amefariki dunia papo hapo katika eneo la Dumila, Barabara ya Morogoro- Dodoma baada ya gari alilokuwa akiendesha kugonga kwa nyuma gari jingine.
Kamanda Chialo alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 10:30 afajiri na kumtaja marehemu kuwa ni Bigabilo Golam (78) ambaye alikuwa akitokea Dar es Salaam akielekea Kigali, nchini Rwanda.

No comments:

Post a Comment