Maafisa wa michezo wauawa Somalia
4 Aprili, 2012 - Saa 18:45 GMT
Wajumbe wa Kamati ya Olimpiki
ya Somalia na viongozi wa chama cha kandanda cha Somalia ni miongoni mwa
watu saba waliouwawa katika shambulio la bomu mjini Mogadishu.
Waziri Mkuu Abdiweli Mohamed Ali pia alikuwepo
wakati wa mlipuko huo katika jumba la maonyesho ya tamthilia
lililofunguliwa upya hivi karibuni lakini aliiambia BBC kwamba
hakudhurika.Jeshi la kuweka amani la Muungano wa Afrika nchini Somalia limelaani shambulio hilo kua ni kitendo "kinachokirihisha" na kusema hakitavuruga juhudi za amani.
Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Somalia , Aden Yabarow Wiish, na mkuu wa shirikisho la kandanda nchini Somalia , Said Mohamed Nur, nao pia waliuwawa. Walikua ni miongoni mwa kikundi cha wageni mashuhuri waliokusanyika kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa kituo cha televisheni ya taifa ya Somalia.
Rais wa shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA ,Sepp Blatter, alisema ameshtushwa sana kwa vifo vya maafisa hao wa michezo.
Waandishi habari watatu wa kituo cha televisheni cha Somalia nao pia walijeruhiwa kwa mujibu wa rubaa zilizoiarifu idhaa ya Kisomali ya BBC.
Jumba hilo la tamthilia lilifungwa katika miaka ya mwanzo ya 1990 wakati Somalia ilipotumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na lilifunguliwa upya mwezi mmoja tu uliopita wakati wa awamu mpya ya matumaini ya kurejea amani.
Waziri mkuu Abdiweli alisema mwanamke aliyejitoa mhanga ndie aliyefanya shambulio hilo.
Akilaani kundi la al-Shabab, alisema ni kawaida yao "kuwaua watu wasio na hatia ".
Salah Jimale,aliyeshuhudia shambulio hilo ameliambia shirika la habari la Associated Press " Mlipuko huo ulitokea wakati wapiga muziki walikua wakiimba huku wakishangiliwa na watazamaji.
"Moshi mweusi ulitanda kila mahali. Watu walipiga mayowe na wanajeshi ghafla wakaanza kufyatua risasi katika lango la kuingia ndani."
Waandishi wa habari waliokuwepo hapo wanasema watu kadhaa walijeruhiwa na wanaelezea kuona viatu na simu za mkononi vilivyojaa damu,na viti kulipuliwa vipande vipande na mlipuko huo.
Katika taarifa yake kundi la al-Shabab limesema ndilo liliohusika na shambulio hilo lakini limezungumzia bomu lililotegwa badala ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga.
Msemaji wa Al-Shabab Sheikh Abdiasis Abu Musab ameliambia shirika la habari la Reuters "sisi ndio tuliopanga mlipuko katika jumba la tamthilia. Tuliwalenga mawaziri na wabunge makafiri na ndio miongoni mwa maafa ya leo."
Wanaharakati hao walitimliwa kutoka Mogadishu na wanajeshi wa Muungano wa Afrika mnamo mwaka jana.
Tangu wakati huo kumekuwepo na kipindi cha utulivu kiasi ambapo shughuli za michezo zilianza upya,mikahawa kufunguliwa pamoja na jumla la taifa la tamthilia.
Lakini al-Shabab imeendelea kushambulia mji mkuu kwa mabomu na makombora. .
Wakati huo huo,mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Somalia, Augustine Mahiga ameelezea kukerwa kwake na shambulio hilo katika Jumba la Tamthilia la Kitaifa.
No comments:
Post a Comment