Waziri amkana Mkapa Arumeru | Send to a friend |
Tuesday, 27 March 2012 20:33 |
0digg
ASEMA HAKUNA TATIZO LA ARDHI, WARAKA WASAMBAZWA KUMPINGA SIOIWaandishi Wetu, Arumeru NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodlucky Ole Medeye amewatetea walowezi wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi katika Jimbo la Arumeru Mashariki kwamba wanamiliki mashamba hayo kwa mujibu wa sheria. Kauli ya Ole Medeye ambaye alikuwa akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo inapingana na ile iliyotolewa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alipokuwa akizindua kampeni za CCM, Machi 12 mwaka huu mjini Usa River. Kadhalika, kauli hiyo inapingana na kauli zote za makada wa CCM na vyama vya upinzani akiwamo mgombea wa CCM Sioi ambao wanakiri kuwapo kwa matatizo makubwa ya ardhi Arumeru, huku wakiahidi kuyashughulikia. Mkapa akizungumzia matatizo ya ardhi siku ya uzinduzi huo, kwanza alikanusha kuwa na ubia na walowezi hao lakini akakiri kuwapo kwa matatizo hayo huku akiahidi kwamba atafikisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete ili alipatie utatuzi. Mkapa alikiri kupokea taarifa za kuwapo kwa migogoro mikubwa ya ardhi inayosababishwa na baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa na kusema kwamba kero hiyo iko katika hatua mbalimbali za utatuzi wake. “Yapo matatizo kadha wa kadha, wapo wawekezaji ambao wamehodhi maeneo makubwa wakati hawayatumii, wapo ambao wamechukua maeneo na kubadilisha matumizi yake na wapo ambao wamekiuka sheria za uendeshaji wa maeneo waliyopewa,” alisema Mkapa. Alisema suala hilo atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kumshauri achukue hatua kwa kuwawajibisha watendaji wa serikali ambao wameshindwa kuwajibika na kuchukua hatua za kisheria kwa wawekezaji waliokiuka masharti. Lakini jana, Ole Medeye alisema mashamba yote 13 yanayotajwa yanamilikiwa kihalali na kwamba ikiwa kuna tatizo lolote basi wizara yake itafuatilia ili kuchukua hatua. “Masuala ya umiliki wa ardhi yanasimamiwa na sheria za nchi, kwa hiyo wawekezaji hawa wanaotajwa, wanamiliki maeneo yao kwa mujibu wa sheria. Sasa kama kuna maeneo hayajaendelezwa basi hilo ni suala la kuona jinsi ya kuchukua hatua,” alisema Medeye katika mkutano wa kumnadi Sioi uliofanyika katika Kijiji cha Sing’isi. Medeye ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua madhubuti kutatua kero ya ardhi ndani ya wilaya hiyo na kwa sasa itayatwaa mashamba yote yanayomilikiwa na watu binafsi endapo hayataendelezwa ili yagawiwe kwa wananchi. Aliyataja mashamba ambayo hayajaendelezwa kuwa ni Valeska, Madira na Tanzania Plantation. Alisema akiwa Naibu Waziri wa Ardhi tayari ametembelea mashamba yote na kwamba Serikali inajipanga jinsi ya kutatua migogoro iliyopo. Alisema endapo watamchagua mgombea wa CCM atashirikiana naye kwa kuwa atakuwa anamkubusha juu ya utekelezaji wa kero za ardhi. Alisema hoja za wapinzani kwamba wanaweza kurejesha ardhi kwa wananchi si kweli kwani ili kufikia hatua hiyo lazima sheria zifuatwe. Amvaa Dk Slaa Ole Medeye alimshukia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwamba ameshindwa kutatua kero ya ardhi na maji katika Wilaya ya Karatu alikokuwa mbunge kwa miaka 10 hivyo asirukie hoja ya Arumeru Mashariki. Alisema katika Wilaya ya Karatu inayoongozwa na Chadema, kuna mashamba 32 yanayomilikiwa na wawekezaji ambao kimeshindwa kuwanyang’anya. Alisema Karatu ambako Chadema kinashika dola kwa kuongoza halmashauri, inaongoza kwa tuhuma za ufisadi kwa kuwa baadhi ya madiwani wa chama hicho waligawana eneo la shule mojawapo ya msingi na kisha kujenga vilabu vya pombe na nyumba za wageni karibu na shule hiyo. Alisema mmoja wa madiwani wa Chadema alibaini ufisadi huo na kuandika barua wizarani kwake. Alisema alifunga safari kwenda Karatu ambako alishudia madudu hayo na kisha kuvifuta viwanja hivyo. Waraka wasambazwa Watu wasiojulikana jana walisambazwa waraka ambao unadaiwa kuandikwa na wabunge wa CCM ambao wanapiga vita ufisadi wakitaka mgombea wa CCM, Sioi Sumari asichaguliwe kwani atawaongezea nguvu mafisadi kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Waraka huo ambao jana ulikuwa ukisambazwa katika mitaa mbalimbali ya Usa River na kwenye mikutano ya kampeni ya Chadema na CCM, una kichwa cha habari kisemacho “Chama cha Mapinduzi na Kamati maalum dhidi ya ufisadi.” Katika waraka huo ambao haujasainiwa na mtu yeyote unadaiwa kutumwa kwa wananchi wa Meru na wabunge wa CCM ambao picha zao zimeambatanishwa. “Tunawaandikia waraka huu kwa kuwa tunaamini kabisa kwa kufanya hivyo tunamfurahisha Mungu na kuwanusuru na kiu ya damu ya baadhi ya viongozi wa nchi hii. Mafisadi hawa wameshindwa kabisa kuacha ufisadi na sasa wanatumia fedha walizowaibia Watanzania…” inasomeka sehemu ya barua hiyo. Kadhalika waraka huo unamtaja mmoja wa makada wakongwe wa CCM (jina tunalihifadhi) kwamba ameamua kutunisha misuli yake na kuhakikisha Sioi anashinda ubunge Arumeru, lengo likiwa ni kuonyesha kwamba ana nguvu zaidi kwa kutumia fedha zake. Chadema jana walikana kuufahamu waraka huo na kusema kuwa wenye uzoefu wa kuandika nyaraka za aina hiyo ni CCM. Mkuu wa operesheni wa uchaguzi huo wa Chadema, John Mrema alisema: “Sisi hatuwezi kuandaa waraka kama huu, haya ni mambo ya CCM wenyewe.” Meneja Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba hakupatikana jana kuzungumzia waraka huo. Chadema chadai kadi 668 Polisi Chadema jana kimeitaka Polisi kurejesha kadi za kupigia kura za watu 668 ambazo zinashirikiliwa Kituo chake cha Usa River na Kituo Kikuu cha Arusha. Mrema alisema wamepata taarifa kutoka polisi za kuwapo vitambulisho vya kupiga kura 206 katika Kituo cha Usa River ambavyo vimeachwa na watu waliokwenda kuwawekea dhamana watuhumiwa. Alisema katika Kituo Kikuu Arusha kuna kadi za vijana wa Meru 462 ambao wanafanyakazi za kubeba mizigo ya watalii katika Mlima Meru maarufu kama Wapagazi. Mkuu wa Oparesheni ya Polisi katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki, Isaya Mngulu alisema asingeweza kutoa maelezo yoyote kuhusu madai hayo akisema maofisa wa ngazi za juu wa polisi walikuwa kwenye kikao. CCM wapigwa mawe Jana, msafara wa CCM ulishambuliwa kwa mawe katika Kijiji cha Sing’is ulipokuwa umekwenda kwa ajili ya kumnadi mgombea wake, Sioi Sumari. Katika tukio hilo, mmoja wa vijana wanaoshukiwa kuhusika na shambilio hilo alikamatwa na vijana wanaosadikiwa kuwa wa CCM na kupigwa hadi kupoteza fahamu hadi alipookolewa na polisi waliokuwa nyuma ya msafara huo. Tukio hilo lilitokea saa 6.30 mchana jana wakati msafara huo wa CCM ulipofika eneo la Chama na ghafla walijitokeza vijana watatu mbele ya magari hayo kisha kuanza kuyashambulia kwa mawe. Vijana hao watatu walikuwa wamevaa beji zenye picha ya mgombea wa Chadema, Joshua Nassari. Katika tukio jingine, kijana ambaye hakufahamika jina, juzi jioni alipigwa kwenye mkutano wa CCM katika Viwanja vya Ngaresero baada ya kuishangilia helkopta ya Chadema iliyopita kwenye eneo hilo wakati Sioi akihutubia. Huko Seela Sing’isi, vijana watatu ambao walikuwa wakinyoosha vidole viwili ambayo ni alama ya Chadema, jana walikamatwa kwenye mkutano wa kumnadi Sioi. Vijana hao walikuwa wamesimama nyuma ya eneo la mkutano na walishikiliwa na polisi baada ya Ole Medeye kutamka kwamba wanaoiunga mkono CCM wanyooshe mikono juu na wao wakanyoosha alama ya vidole viwili. |
No comments:
Post a Comment