Saturday, March 10, 2012

Maelfu watishiwa na njaa eneo la Sahel


Maelfu watishiwa na njaa eneo la Sahel

 9 Machi, 2012 - Saa 12:25 GMT
Eneo la Sahel lakumbwa na njaa
Shirika la misaada la Uingereza Oxfam, limeonya kuwa huenda kukatokea janga kubwa la kibinadam katika eneo la Sahel Afrika Magharibi kutokana na ukame mbaya unaoshuhudiwa katika eneo hilo iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.
Shirika hilo limeanzisha kampeini ya kuomba msaada wa dola milioni thelathini na sita kuwasaidia watu katika eneo hilo.
Athari za ukame huu na bei ya juu ya vyakula zimekuwa zikiongezeka katika eneo hili la Sahel.
Hali hiyo imekithiri zaidi baada ya kutokea tatizo la wakimbizi wanaotoroka mapigano kati ya jeshi la Mali na wapiganaji wa Tuareg kaskazini mwa nchi hiyo.
Watu laki moja wamelazimika kutoroka makwao nusu yao wakiingia katika nchi jirani ya Niger na mataifa mengine ambayo tayari yanakabiliana na hali ngumu ya maisha.
Takriban watoto milioni moja wamo katika hatari ya utapia mlo. Mkurugenzi wa shirika hilo anasema juhudi za pamoja zinahitajika kuwanusuru maelfu ya watu ambao wanakufa kutokana na uzembe wa jamii ya kimataifa.
Inaelezewa kwamba katika baadhi ya vijiji nchini Chad waathirika wanachimba vilima vya mchwa na kuchukua chakula ambacho mchwa hao wamehifadhi kwa lishe yao.

No comments:

Post a Comment