Friday, March 30, 2012

Wafuasi Chadema watawanywa kwa Mabomu Songea

Wafuasi Chadema watawanywa kwa Mabomu Songea  Send to a friend
Thursday, 29 March 2012 21:06
0digg
Boniface Meena, Songea
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma juzi jioni lilirushia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana kutokea katika mkutano wa hadhara wa kampeni za udiwani kuelekea katika ofisi za mkoa za chama hicho baada ya kumsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Msafara wa wafuasi hao wa Chadema ambao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za chama hicho walipita karibu na mkutano wa CCM uliokuwa ukihutubiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi ndipo polisi walikuwa katika eneo hilo waliwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.

Hatua hiyo ya polisi kupiga mabomu ya kutoa machozi ilisababisha wafuasi hao kukimbia kila kona kutafuta mahali pa kujificha ili kujiokoa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma,  Michael Kamhanda alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema; "Sina taarifa."

Akizungumzia tukio hilo, Zitto alisema aliwashangaa polisi hao kuwatawanya wanachama hao kwa kuwapiga mabomu ya kutoa machozi na kuwashauri kuwa wasome alama za nyakati wanaposhughulikia masuala ya raia.

Alisema ni kawaida kwa wanachama wa Chadema mjini Songea kuandamana baada ya mkutano hadi katika ofisi za chama kuagana, hivyo polisi walipaswa kuelewa hilo na kutokuamua kutumia nguvu.

Awali, akihutubia katika mkutano huo wa Lizaboni, Songea katika kampeni wa uchaguzi mdogo wa udiwani unaotarajiwa kufanyika  Aprili mosi, mwaka huu aliwaambia wakazi wa Songea kuwa atahakikisha wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ambao wamekuwa na tabia ya kuiba mafuta ya jenereta za kuzalishia umeme wanachukuliwa hatua za kisheria haraka iwezekanavyo, ili kuondoa tatizo la umeme linaloukabili mji wa Songea na viunga vyake.

Zitto alisema akiwa Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), atashughulikia tatizo hilo kwa kufanya mambo mawili ambayo ni kuwahoji kwa nini umeme ukatike hovyo Songea na matumizi ya mafuta yanatumikaje ambayo yanalalamikiwa kuisha mara kwa mara.

“Hili halina mjadala wakija na kuwahoji kwa kuwa wanaripoti kwangu mtiti (mgogoro) wake mtauona. Nimeweza kumshughulikia mkurugenzi wa Tanesco, hivyo kwa Songea itakuwa ni kitu kidogo kwangu,” alisema Zitto.

Katika kuondoa tatizo la umeme katika mkoa wa Ruvuma, alisema ujenzi wa mitambo mikubwa ya kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe inajengwa Mbinga yenye uwezo wakuzalisha megawati 120 na mji wa Songea utapata kilovoti 220 na kulifanya tatizo hilo kuwa ndoto na kwamba mkoa wa Ruvuma utaunganishwa na gridi ya taifa kutoka Makambako, mkoani Njombe.

Zitto alimsihi Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma (RPC), akitaka wasimamie haki na kuacha mpango wao unaodai kuwa mgombea udiwani wa kata ya Lizaboni kwa tiketi ya chama hicho ana tuhuma zinazomkabili tangu mwaka 1988.

“Chadema imeinasa barua waliyoandikiana wakuu hao wa Jeshi la Polisi. Tunataka kujua inakuwaje tuhuma hizo zifumbiwe macho tangu mwaka 1988 zije kuibuliwa sasa. Muda wote huo walikuwa wapi, wakati mgombea alikuwa kiongozi wa mtaa kwa vipindi viwili?,” alihoji Zitto.

Alisema katika barua hiyo, diwani huyo anaundiwa zengwe linaloonesha kuwa yeye alikuwa anachochea waendesha pikipiki waandamane na kuleta fujo katika kipindi cha mauaji yaliyotokea miezi michache iliyopita mjini hapa.

Zitto amelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji yaliyotokea na si kutishia raia na kwamba, ili kukomesha tabia hiyo ya polisi, ameahidi kupeleka barua hiyo bungeni.

Aliongeza kwamba jeshi la polisi lina mpango wa kuleta polisi wengine kutoka nje ya mkoa wa Ruvuma siku ya uchaguzi ili kuwadhibiti wananchi wa Lizaboni washindwe kupiga kura siku ya uchaguzi, kwakuwa kwa sasa polisi wa Songea wengi ni Chadema.

Akiwa Mbeya

Juzi, Zitto alisababisha kuvunjika kwa Soko la wilaya ya Rungwe baada ya kufanya maandamano makubwa kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo  uliofanyika Kiwira Madukani.

Zitto alifanya maandamano hayo ambayo yalihudhuriwa na mmia ya wananchi wa Kiwira kuanzia saa 9:30 na wakati wakipita katika soko hilo, wafanyabiashara waliokuwa wakichuuza katika soko hilo waliacha biashara zao na kuhamia eneo la mkutano huku wakiimba wimbo wa Chadema wa 'Presha inapanda, presha inashuka'.

No comments:

Post a Comment