Monday, October 31, 2011

HIVI KANISA LINAENDA WAPI JAMANI?

Jaji atoa ushauri kumng'oa Kakobe  Send to a friend
Sunday, 30 October 2011 20:43
0digg
James Magai
JAJI wa Mahakama Kuu, Augustine Shangwa amewashauri walalamikaji katika kesi inayomkabili Askofu Zachary Kakobe kuwashawishi waumini wa kanisa hilo, wamng'oe madarakani kama wana hoja za msingi.

“Kama mnaona kuwa Askofu Kakobe anakwenda kinyume, basi muwekeni kiti moto na kama mnaona sasa amekuwa dikteta, hawafai basi tumieni nguvu ya waumini kumpindua katika nafasi hiyo,” alisema Jaji Shangwa.

Jaji Shangwa alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya kutoa uamuzi wa kama Askofu Kakobe anastahili kushtakiwa au la.

Hatua hiyo imekuja baada ya Askofu Kakobe kuwawekea pingamizi walalamikaji kwa kile alichoieleza Mahakama kuwa hawana haki kuzungumzia masuala ya kanisa kwa kuwa si viongozi tena.

Uamuzi wa ama walalamikaji hao wana haki ya kumshtaki Askofu Kakobe au la, utatolewa Novemba 30, mwaka huu.

Askofu Mkuu huyo wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), anakabiliwa na kesi ya madai Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akituhumiwa kwa ubadhirifu wa mali na fedha zaidi ya Sh14 bilioni pamoja na ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo.

Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2011, ilifunguliwa na Dezedelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma ambao wanadai kuwa ni wachungaji wa kanisa hilo.

Hata hivyo, Kaduma amejitoa baada ya kupata ajali mbaya na kufanyiwa upasiaji kichwani, lakini msimamizi wa kanisa hilo wilayani Liwale, Mkoa wa Lindi, Mchungaji Ignas Innocent ameiomba Mahakama hiyo imwunganishe na walalamikaji hao katika kesi hiyo.

Akisikiliza kesi hiyo juma lililopita, Jaji Shangwa mbali na kuwashauri waumini hao kuimaliza kesi hiyo wenyewe, alipendekeza walalamikaji hao wafungue kesi ya jinai katika maeneo yanayoonekana kuwa ni makosa ya jinai.

Akisoma madai ya walalamikaji hao kipengele kimoja kimoja, Jaji Shangwa alihoji ni vipi Mahakama inaweza kuamua madai yanayohusiana na mapato na matumizi ya kanisa na taratibu nzima za uendeshaji wake.

Jaji Shangwa alipendekeza kuwa kwa madai yanayoonekana kuwa ya jinai, walalamikaji hao wafungue kesi ya jinai badala ya madai.

Alisema madai kama ya wizi na kusababisha kifo cha muumini, hayastahili kuchanganywa na madai kwa kuwa yenyewe ni ya jinai.

“Madai kama haya ni ya jinai hivyo inabidi mfungue mashtaka ya jinai. Kama DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) akikataa mnaweza kufuata utaratibu wa private prosecution (mashtaka binafsi),” alisema Jaji Shangwa.

Hii ni mara ya pili kwa Jaji Shangwa kuwashauri walalamikaji hao kutumia njia mbadala wa Mahakama kumaliza mgogoro wao dhidi ya Askofu Kakobe. Agosti Mosi, mwaka huu aliwashauri walalamikaji hao kutafakari upya juu ya madai yao ili kuona kama yana msingi.

Pia aliwatahadharisha kuwa iwapo wataamua kuendelea nayo na katika uamuzi wa mahakama, wakashindwa, watajuta kwa sababu watatakiwa kumlipa Askofu Kakobe fidia kubwa na gharama za uendeshaji kesi, ambazo hana hakika kama watazimudu.

Kabla ya kuwashauri walalamikaji hao, Jaji Shangwa alianza kwa kuonyesha wasiwasi wake juu ya msingi wa madai ya walalamikaji kuhoji matumizi ya fedha za kanisa hilo. Alisema kwa mfumo wa FGBF, Askofu Kakobe ndiye kanisa na kwamba mapato ya kanisa hilo ni mali yake kwa sababu, alilianzisha mwenyewe na kuhoji iweje wamhoji mtu anayetumia mali yake.

“Kwani ni nani alimpa Kakobe uaskofu? Kakobe alijifanya mwenyewe, ni tofauti na maaskofu wa Katoliki ambao mpaka waende wakasomee.”
Msiniambie nina-prejudge (nihukumu kabla), maana huwa mnatulaumu kesi kurundikana mahakamani. Mimi hapa natafuta suluhu na suluhu ni pamoja na kuondoa kesi mahakamani,” alisema Jaji Shangwa.

Alihoji kosa la Askofu Kakobe kukusanya michango kutoka kwa wana jumuia na kwenye mikutano ya mahubiri anayofanya nchi mbalimbali kujengea nyumba yake kama walalamikaji wanavyodai.

“Lakini si anatumia fedha zake? Mimi najiuliza maana ndiye alianzisha kanisa, kama kulikuwa na wafadhili ndipo akawafundisha na nyie mkawa wachungaji. Hizi fedha hapewi na Serikali ni za wale anaowatibu na wanaokuja kuombewa mapepo. Kwa hiyo anazikusanya kwa huduma, sasa mtamwulizaje na chake? Labda mngesema kuwa hawapi au anawapunja mshahara wakati mnashinda kanisani mnaombea mapepo, maana hii ni kazi kubwa.”

Katika madai yao, walalamikaji hao walieleza kuwa, Askofu Kakobe alikusanya michango kutoka kwa waumini inayofikia Sh14 milioni kwa ajili ya kununulia kiwanja cha kanisa, lakini ikabainika kuwa kiwanja hicho kilinunuliwa kwa Sh4 milioni tu.

Madai mengine katika kesi hiyo ni Sh2 bilioni wanazoeleza kuwa alipewa Askofu Kakobe kwa ajili ya kujengea makazi ya Kiaskofu, lakini mpango huo umekufa na badala yake anataka kuhamia Marekani kabla ya kurejesha fedha hiyo.

Wachungaji hao pia wanataka Askofu Kokobe arudishe Sh800 milioni alizopewa kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuanzisha kituo cha matangazo ya televisheni kwa maelezo kuwa vifaa hivyo havikununuliwa kwa kuwa eneo la mradi huo, limeathiriwa na mradi wa umeme wa msongo mkubwa.

Kuhusu kifo cha mmoja wa waumini, walalamikaji hao wanadai kuwa, Askofu Kakobe aliwashawishi waumini kufunga siku saba bila kula, jambo lililosababisha mmoja wao kufariki dunia.

Hati ya madai inaeleza kuwa walalamikaji hao wanamtuhumu Askofu Kakobe kuwa amekuwa akikusanya fedha nyingi kutoka kwa waumini wake kwa madai ya kufanyia shughuli na miradi mbalimbali ya kanisa na kuzitumia kinyume cha malengo.

Mbali na kuzitumia isivyo, kama vile kugharamia kampeni za kisiasa kinyume cha katiba ya kanisa hilo, pia wanadai kwamba amekuwa hatoi taarifa ya mapato anayokusanya wala matumizi yake.
Kuhusu ukiukwaji wa Katiba ya kanisa hilo, walalamikaji hao wanadai kuwa katiba inataka kuitishwa kwa mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano, lakini Askofu Kakobe hajawahi kuitisha mkutano huo tangu mwaka 1989.

Pia wanadai kuwa katiba ya kanisa hilo, inataka kanisa liwe na katibu mkuu na mweka hazina, lakini Askofu Kakobe amekuwa akifanya kazi zote hizo peke yake.

No comments:

Post a Comment