Monday, June 20, 2011

POSHO ZA WABUNGE TANZANIA

Sakata la Posho:Chadema wamkaba koo Waziri Mkuu  Send to a friend
Sunday, 19 June 2011 21:04
Waziri MKuu Mizengo Pinda
Waandishi Wetu, Dodoma na Dar
SUALA la kufutwa kwa posho za wabunge na watumishi wengine wa umma bado ni mwiba kwa Serikali, baada ya Chadema kuzidi kumbana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na safari hii wakimtaka afute kauli yake kwamba posho hizo zipo kisheria kwa kuwa si kweli vinginevyo watachukua hatua kali zaidi.Chama hicho pia kimemtaka Waziri Mkuu,  kuueleza umma kwamba kauli yake ya kuwa Wabunge wa Chadema wanazimezea mate posho hizo, si kweli kwani msimamo wa kuzipinga upo kwenye Ilani ya chama hicho ya mwaka 2010.

Katibu wa  Wabunge wa Chadema na Kambi ya Upinzani  bungeni, John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Dodoma kuwa Pinda anapaswa kufanya hivyo kabla ya mwisho wa mkutano huo wa bajeti, vinginevyo wabunge wa chama hicho watakaa na kujadili cha kufanya.

Alisema  kauli ya kuhalalisha posho za wabunge kwa hoja ya kwamba zinahitajika kwa ajili ya kuwapa watu wanaoomba fedha nje ya Ukumbi wa Bunge siyo sahihi kwani ni kinyume na misingi ya Bunge na maadili yake.

“Waziri Mkuu, Pinda anapaswa kufuta kauli yake kwani inapotosha majukumu ya Bunge na wabunge wake yaliyotajwa kwenye ibara ya 63 kifungu cha (2) na (3) ya kuisimamia Serikali, kuwakilisha wananchi, kupitisha mipango na kutunga sheria,” alisema na kuongeza:

“Kauli ya Waziri Mkuu Pinda inahamasisha siasa za fadhila katika taifa, ambazo zimetumika na CCM kupandikiza mbegu za rushwa katika uchaguzi kwa kisingizio cha takrima."

Mnyika alisema kauli hiyo ya Pinda inadhihirisha kuwa hana dhamira ya dhati kutekeleza kwa ukamilifu na kwa haraka maagizo ya Rais Jakaya Kikwete kinyume na Katiba ibara ya 52 (3) inayomtaka atekeleze au asababishe utekelezaji wa jambo lolote ambalo Rais ataagiza kwamba litekelezwe.

Alisema akiwa Katibu wa wabunge wa Chadema anamtaka Waziri Mkuu, Pinda kuelewa kuwa suala la kutaka mabadiliko ya mfumo wa posho ni la pamoja kwa Chadema na hivyo kumtaka Waziri Mkuu huyo kusoma ilani ya chama hicho kupata msingi wa msimamo huo.

“Kama sehemu ya kuimarisha uchumi kwa kuondoa ubadhirifu ilani ya Chadema ya Agosti 2010 kifungu cha 5.5.1 kipengele cha 5 imeeleza bayana kuwa Serikali ya CCM imekuwa ikitenga kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya posho,” alisema Mnyika huku akitolea mfano wa posho za Ofisi ya Rais na Bunge kwa mwaka 2009/10

Aliendelea, "Kipengele cha 6 kwenye ilani ya Chadema ya mwaka 2010 kimeeleza bayana kwamba Serikali ya Chadema itaweka utaratibu ili semina, warsha, mafunzo na vikao katika taasisi mbalimbali za umma zifanyike kama sehemu ya kazi bila uwepo wa posho maalumu za vikao kwa siku.”

Zitto asema Pinda anapingana na Mpango wa Taifa wa Maendeleo

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amemtaka Pinda ajiuzulu au afukuzwe kazi mara moja kutokana na kutetea posho hizo kuwa zipo kwa mujibu wa sheria zilizoanishwa kikatiba na kudai  wapo Wabunge wa Chadema wanaozimezea mate.

Akizungumza na gazeti hili jana, Zitto  alisema, " Mimi nina mambo mawili kwa Waziri Mkuu, anapaswa kuchukua uamuzi ama ku resign (kujiuzulu) au afukuzwe kazi mara moja kwa kutetea posho."

Akitetea hoja yake, Zitto alisema kitendo cha Pinda kutetea posho kimemfanya ashindwe kutekeleza uamuzi wa kisera wa Baraza la Mawaziri ambao pia ulipitishwa na Bunge, hivyo anapaswa kujiuzulu.

"Kwanza, nasikitika kuwa Waziri Mkuu amerejesha suala la posho za vikao kwenye mjadala ilhali lilimalizwa baada ya Bunge kupitisha Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano. Kitendo cha Waziri Mkuu kulilia posho kinaonyesha jinsi asivyo  tayari kusimamia na kutetea sera za Serikali yake anayoiongoza," alisema na kuongeza:

"Anapaswa kuchukua hatua mbili, ama afukuzwe kazi mara moja kwa kwenda kinyume na maamuzi ya kisera ya Serikali yaliyopitishwa na Baraza la Mawaziri kisha Bunge au, ajiuzulu. Hatuwezi kuvumilia viongozi wanaokwenda kinyume na sera za Serikali." 

Zitto alisema uamuzi huo wa Baraza la Mawaziri ambao ni wa Serikali uliomo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa miaka mitano, umeanisha maeneo ya vipaumbele na namna ya Serikali kudhibiti matumizi yakiwamo kukata posho na kupunguza misafara ya safari za viongozi.

Naibu Kiongozi huyo wa upinzani bungeni alifafanua kwamba, baada ya uamuzi huo kujadiliwa ulipitishwa na wawakilishi hao na kuonyeshwa kushangazwa na kauli hiyo ya Waziri Mkuu.

"Kauli ya Waziri Mkuu haiwezi kupita hivi hivi bila kuhojiwa. Waziri Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge), alisema kuondolewa kwa posho za vikao ni msimamo wa Serikali katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Then (kisha ukaletwa na Serikali na Bunge likaujadili na kuupitisha," alisema Zitto na kuongeza,

"Sasa leo hii, wiki moja baada ya kupitishwa na Bunge, Waziri Mkuu anakuja kusema posho ni suala la kikatiba, hivyo anakwenda kinyume na uamuzi wa kisera wa Serikali, kimsingi, anapaswa ku resign ua kufukuzwa."

Aliongeza kwamba, tayari uamuzi huo uliotokana na Baraza la Mawaziri na kisha kupitishwa na Bunge umeanishwa katika mpango huo ukurasa wa  17, hivyo kitendo cha mkuu huyo wa shughuli za kiserikali bungeni ni kuupingana nao.

Zitto alisema akiwa waziri Kivuli wa Fedha, leo anatarajia kuwasilisha hoja bungeni akimtaka Waziri Mkuu ajiuzulu kutokana na mapungufu hayo ya kiutendaji.

"Natarajia kuwasilisha hoja hiyo bungeni kutaka Waziri Mkuu ajiuzulu wakati nikichangia. Haiwezekani Waziri Mkuu apingane na maamuzi ya kisera ya Serikali ambayo pia yamepitishwa na Bunge." 

Mapema mwezi huu Zitto alimwandikia Spika wa bunge barua akielezea kusudio lake la kukataa posho ya vikao vya wabunge bungeni, akijenga hoja kwamba hiyo ni sehemu ya kazi yake, hivyo kulipwa ni makosa akitaka fedha hizo zielekezwe jimboni kwake.

Hata hivyo, hoja hiyo ambayo imetekwa na chama chake cha Chadema inaonekana kuitikisa nchi huku viongozi wa dini, wasomi na watu wa kada tofauti wakijadili kwa mitazamo tofauti.

Askofu awalipua wabunge kuhusu posho

Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao juzi alitema cheche akiwataka wabunge kuacha kutanguliza ubinafsi katika kung’ang’ania kulipwa posho za vikao vya Bunge.

Badala yake, Dk Shao alisema posho hizo na zile wanazolipwa watumishi wa umma waliofikia ngazi ya menejimenti zielekezwe kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wanaofanya kazi katika mazingira magumu vijijini.

Kauli hiyo ya Askofu Shao imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Pinda kutetea malipo hayo ya posho ambayo yamezua malumbano makubwa bungeni kati Wabunge wa Upinzani , CCM na Spika, Anne Makinda.

“Nchi hii kuna uozo huko kwa wakubwa kutanguliza mambo binafsi…mimi kwanza…na hili limesumbua sana kwenye Bunge wiki hii, wakubwa kwanza, waheshimiwa wabunge kwanza,”alisema Dk Shao.

Askofu Shao alisema yeye anaungana na wale wanaopinga kulipwa kwa posho hizo akisisitiza kuwa si haki wabunge kutanguliza umimi na kuwataka wabunge na vigogo serikalini wasiingie katika dhambi ya umimi.

"Posho hizo ziende zikaboreshe  matabibu vijijini, ziende kwa walimu wetu wanaofundisha katika mazingira magumu, kutanguliza umimi siyo haki, tunaomba sana wabunge msiangalie mambo yenu wenyewe,"alisisitiza Askofu Shao.

Dk Shao alisema ni vyema Serikali ikawa na mpango mahsusi wa kuendesha sekta ya afya kwa kushirikiana na mashirika ya dini, ili kuhakikisha hospitali na zahanati vijijini zinakuwa na madaktari na wauguzi mahiri.

Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema, Hai, Kizitto Noya na Masoud Masasi, Dodoma, Ramadhan Semtawa, Dar.

No comments:

Post a Comment