Moto wa Chadema watisha mawaziri | Send to a friend |
Thursday, 07 June 2012 19:58 |
0digg
MKUCHIKA, GHASIA, CHIKAWE NA MEMBE WAENDA KUUZIMA, CCM KUJIPIMA NGUVU JANGWANI KESHOGeofrey Nyang’oro, Mchinga VUGUVUGU la Mabadiliko (M4C) linaloendeshwa na Chadema katika mikoa ya Lindi na Mtwara, limewatisha mawaziri wanne wanaotoka katika mikoa hiyo, ambao wamelazimika kurejea majimboni mwao kusafisha hali ya hewa. Mawaziri waliorejea majimboni kufanya kilichoelezwa ni shughuli za kiserikali ni pamoja Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Kwa wiki takribani ya pili sasa, Chadema kimekuwa kikiendesha operesheni hiyo ya vuguvugu la mabadiliko katika mikoa hiyo ya kusini mwa nchi. Jana, taarifa zilizopatikana mkoani Lindi zilisema Ghasia alifanya mkutano katika jimbo lake la Mtwara Vijijini akiwa katika harakati za kufuta nyayo za Chadema. Oparesheni hiyo ya Chadema jana na leo ilitarajiwa kuingia jimbo la Mtama ambalo linaongozwa na Membe. Vuguvugu hilo linaongozwa na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema, ambao ni Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe ambao wanatarajia kuhutubia mikutano yao katika kata aliyozaliwa Membe. Mkuchika alithibitisha jana kuwa yuko jimboni kwake Newala, na alipoulizwa kama lengo lake ni kufuta nyayo za Chadema, aling’aka, “Kwani kila siku nikija nyumbani kwangu huwa mnaniuliza, mimi nimekuja nyumbani kwangu bwana. Niacheni nipumzike nyumbani kwangu.” Membe alipotafutwa kuzungumzia taarifa hiyo simu yake haikuwa hewani, lakini Msemaji wa wizara hiyo, Assah Mwambene alipoulizwa alipo bosi wake alithibitisha kwamba yuko jimboni kwake. Jana, vuguvugu hilo lilikuwa katika Jimbo la Mchinga mkoani Lindi, lakini lilikumbana na upepo mzito wa kisiasa baada ya bendera mpya za CCM kuonekana kupamba kona mbalimbali za jimbo hilo. Waziri Ghasia na Chikawe pia hawakupatikana kupitia kwa simu zao kuzungumzia taarifa hizo. Msigwa ashambulia mawaziri Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliwashambulia mawaziri hao wanaotoka majimbo ya mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara, akihoji ni kwanini wanaikumbatia CCM. Msigwa alisema CCM imeshindwa kuwasaidia kuleta maendeleo katika mikoa hiyo ya kusini mwa Tanzania, ndiyo sababu, watu wanaishi katika hali ya umasikini wa kutisha. “Mimi ninawashangaa wabunge wa majimbo ya Lindi na Mtwara wakiwamo mawaziri Hawa Ghasia, Mkuchika na Bernard Membe ni kwa nini wanakiunga mkono CCM wakati majimbo yao yamekithiri kwa umaskini,” alisema Msigwa na kuongeza; “Nashangaa Membe, Hawa Ghasia na Mkuchika sijui kiburi wanakipata wapi. Ndiyo sababu wamehama majimbo yao na kuishi Dar es Slaam, haiwezekani leo mikoa wanayotoka, wilaya na hata majimbo yakawa na sura kama ilivyo sasa. Nitakwenda kuwabana bungeni,’’ alisema Msigwa. Msigwa alitamba kuwa yeye na wabunge wote wa Chadema wanaishi kwenye majimbo yao, ndiyo sababu wamekuwa wakifanikiwa katika mikakati yao ya kutetea na kuwaletea maendeleo wananchi wao. Sugu alia umaskini Katika mkutano huo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) alisema ukarimu wa wakazi wa Lindi na Mtwara kwa CCM ndio uliosababisha mikoa hiyo kuwa katika lindi la umaskini. Mbilinyi alisema wabunge kupitia chama hicho hawana uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo kutokana na mfumo wa chama hicho kukumbatia matajiri na kuachana na maskini. Alisema ndani ya CCM, watu wa kipato cha chini hawawezi kupata ubunge, akitoa mfano kwamba fomu ya ubunge ya CCM inachukuliwa kwa Sh100, 000 ilihali ya Chadema ni Sh50,000. “Nawasihi vijana wenzagu kuungana na kuwa na ujasiri wa kuamua katika masuala ya kimaendeleo. Mimi nilikuwa mitaani na muziki wangu, lakini nikatokea Chadema na kunipa nafasi ya kugombea ubunge ,lakini ningekwenda CCM wasingenipa nafasi ya kugombea kwa sababu ya umaskini wangu,” alisema Mbilinyi na kuongeza: “Hivyo, basi wazee na vijana nawasii kuachana na CCM kwa sababu chama hicho kimekosa mwelekeo tangu alipofariki Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, CCM iliyobaki ni ya wanjanja sio wewe ulioko kijijini.” CCM kujipima nguvu Jangwani Wakati Chadema ikizidi kuwasha moto wa vuguvugu la mabadiliko, Chama tawala CCM kesho kitafanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, kutoa msimamo wake kuhusu mambo muhimu yanayogusa taifa. Mkutano huo unafanyika ikiwa zimepita takribani wiki mbili tangu Chadema wafanye mkutano mkubwa katika viwanja hivyo uliohudhuriwa na mamia ya watu, na kuzindua kampeni yake ya M4C’, yenye lengo la kushika dola mwaka 2015. Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana katika mtandao wa chama hicho tawala jana, iliyotolewa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa mkoa huo, Juma Simba ilieleza kwamba mkutano huo utaanza saa 8 mchana. Simba alisema katika taarifa hiyo kwamba, chama hicho kitatumia mkutano huo kuwaeleza Watanzania msimamo wake kuhusu hatma ya maisha yao. “Utaeleza hatma ya maisha ya Watanzania katika suala la ajira, miundombinu ya barabara, reli, bandari na anga, bei za bidhaa mbalimbali, umeme na rasilimali za taifa,” alisema Simba. Alifafanua kwamba jambo jingine litakaloelezwa katika mkutano huo, ni msimamo wa chama hicho kuhusu mchakato wa Katiba Mpya pamoja na vurugu za Zanzibar. Katika mkutano huo watakuwapo viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali na kutoa ufafanuzi juu ya masuala hayo, yaliyoainishwa kama msimamo wa chama hicho. |
No comments:
Post a Comment