Friday, June 8, 2012

Bajeti gani inakuja Tanzania?

Ni bajeti gani inakuja?

editor's picture
Na editor - Imechapwa 06 June 2012
Printer-friendly versionSend to friend
Maoni ya Mhariri
HIVI serikali imeandaa bajeti gani kwa ajili ya Watanzania katika mwaka wa fedha unaoanzia mwezi ujao? Ina vipaumbele vichache vya kuzingatia au utitiri kama ilivyokuwa bajeti inayomalizika?
Imetenga fedha za kutosha kushughulikia tatizo kubwa la nishati ya umeme; au inakuja tena na porojo na mikakati isiyotekelezeka?
Hatuamini serikalini bado hawajaelewa umuhimu wa kulipa eneo hili mtizamo mpya, badala ya ule wa mazoea – kuongeza miradi ya kutumia mitambo ya kukodi ili kuzalisha umeme. Hii ni miradi ulaji.
Tuseme wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza, wanadhani bado ipo nafasi ya kutumia fedha za Watanzania, kutajirisha kampuni za kikabaila na mawakala wao waliopo nchini?
Iwapo serikali ingalipo hapohapo, tutaamini kumbe wanatenda mzaha na hatutaishia hapo. Tutashikamana na wananchi kupinga kwa nguvu maana ni mpango butu ambao haukufaa juzi wala jana na hautofaa leo hata kesho.
Tunataka viongozi wasikie kilio hiki na waheshimu wanataaluma wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wanaohitaji kusaidiwa fedha ili kutekeleza miradi ya maendeleo waliyoibuni. Wakisaidiwa, angalau wataacha kulalamika chinichini kuwa nguvu zao zinabezwa.
Tunalisemea sana hili tukiamini umeme ndiyo injini ya maendeleo. Bila umeme, tena wenye uhakika, hatuwezi kuota maendeleo.
Hakutakuwa na uzalishaji wenye tija, si maofisini, viwandani, mashambani wala majumbani.
Tusipokuwa na uzalishaji maeneo hayo, tumefunga fursa za kukuza uchumi wa taifa na wa familia. Uchumi hukua kwa nchi kuuza bidhaa nyingi nje, na kuzalisha chakula cha kutosha.
Nchi ikiuza zaidi bidhaa nje kuliko inavyonunua, inahifadhi fedha zake za kigeni kwa matumizi ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa mafuta, injini nyingine kwa maendeleo.
Uzalishaji chakula husaidia sana kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa. Takwimu za eneo hili zinasikitisha na zinahitaji kufutwa ili ziende na hali halisi ya uwezo wa wananchi.
Tungependa fedha nyingi zaidi zitengwe kutekeleza miradi ya maendeleo itakayoongeza ajira na kupunguza pengo la wenye nacho na wasionacho nchini.
Tukitanua wigo wa kodi, na kusimamia ukusanyaji wake, ikiwemo kufuta misamaha holela, tutapata mapato zaidi na kujenga uwezo wa serikali kuhudumia madeni ambayo yameanza kuwa mzigo mzito.
Sasa tuone serikali kweli viongozi wake wanasikia au wataendeleza jeuri na hivyo kujiandaa kupata fedheha kama watu walioshindwa kuongoza?

No comments:

Post a Comment