Waraka uliowaondoa Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo huu hapa
Waraka uliowaondoa Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo huu hapa
MKAKATI WA MABADILIKO 2013
UTANGULIZI:
Taasisi tunayoizungumzia ilisajiliwa rasmi mwezi January 1993 na tokea
wakati huo imeongozwa na wakuu wa taasisi wapatao wawili na aliyepo kwa
sasa ni wa tatu. Wa kwanza aliongoza kwa miaka mitano tangu wakati huo
1993 hadi 1998 na kumwachia aliyefuata ambaye naye aliongoza kwa miaka
mitano hadi mwanzoni mwa 2004 na kumwachia aliyepo sasa. Huyu aliyepo
aliongoza kwa miaka mitano tangu mwaka 2004 hadi 2009 na kisha
akachaguliwa tena mwaka 2009 kwa kipindi cha pili. Tunapenda kwa hatua
ya mwanzo kabisa kutambua juhudi za wakuu wetu wote waliopita
walizozifanya katika kuhakikisha taasisi yetu inakua kwa kutumia uwezo
wote waliokuwa nao na katika mazingira yaliyowakabili. Mwaka 1995 chini
ya mkuu wa kwanza tulipata wawakilishi watatu kwenye chombo chetu kikuu
cha uwakilishi. Mwaka 2000 chini ya mkuu wa pili tukapata wawakilishi
wanne pamoja na wa nyongeza mmoja na kufanya idadi kuwa watano. Mwaka
2005 chini ya mkuu wa tatu ambaye ndiye aliyepo hivi sasa, tulipata
wawakilishi watano na wa nyongeza sita jumla wakawa 11. 2010 chini ya
mkuu huyu huyu wawakilishi wakaongezeka na kuwa 23 na wa nyongeza 25 na
kufanya idadi kuwa 48 kabla ya kupata mwingine mwaka jana na kufanya
sasa wawe 49.
Tunapopongeza juhudi zao hizi tunahitaji pia kuwapongeza wakuu wetu
wawili wa kwanza ambao kimsingi waliweka msingi mzuri sana wa
kutong’ang’ania madaraka na badala yake kuachia mapema na kumwachia
mwingine kidemokrasia bila vurugu. Hawakuwa madikteta na tunawapongeza
sana. Walijitahidi sana kutokuwa wapenda madaraka na kimsingi
walituwekea utamaduni ambao walitaka wote tuufuate na kujenga taasisi
imara inayojali demokrasia na haki ya kila mwana taasisi. Ni kwa msingi
huo waliamua kuandika kabisa katika mwongozo wetu kwamba kiongozi yeyote
katika ngazi yoyote ya kuchaguliwa atakapogombea na kushinda ataongoza
kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na kisha ataweza kugombea na
kuongoza kwa kipindi cha pili cha miaka mitano baada yapo hawezi
kugombea tena katika nafasi ile ile aliyoitumikia kwa vipindi viwili.
Ili kuonyesha kwamba walimaanisha kile walichokisema, wote wawili
hawakuwahi kukaa madarakani kwa vipindi viwili vilivyoruhusiwa katika
mwongozo bali wote wawili walikaa kipindi kimoja kimoja tu.
Lakini kuna matatizo yameanza kujitokeza na tusipochukua hatua haraka
huko mbele tunaweza kupata shida kubwa. Tunapenda kuainisha matatizo
hayo kwa uchache kama ifuatavyo:
Wakati tukiufanyia mwongozo wetu mabadiliko mwaka 2006 hatukugusa
kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya
vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Lakini wakati mwongozo
unachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa
kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele
hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi
waliopo madarakani kwa sasa. Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo
kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika
jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo
mengine makubwa na yenye athari zisizomithirika kwa taasisi yetu.
Ni dhahiri kwamba uongozi uliopo umeishiwa mbinu na kuakisi jambo la
msingi sana ambalo waasisi wetu waliliona tangu mwanzo na kuamua kuweka
kipengele cha ukomo wa uongozi kwenye mwongozo wetu. Kuchoka kwa uongozi
wetu kunaonekana dhahiri katika mipango na mikakati ya taasisi ya miaka
kadhaa. Mfano mwaka 2008 uongozi ulianzisha mkakati wa operesheni
samaki mkubwa (maarufu kama Oparesheni Sangara). Huo ulifanyiwa kazi
katika mikoa kadhaa na hatimaye ikafa kimya kimya. Baada ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010 kulianzishwa matembezi ya maandamano ambayo nayo
yalikuwa yakipeleka ujumbe kwa watu na yalipangwa kufanyika mikoa yote
na wilaya zote.
Kumbukumbu zetu zinaonyesha kwamba yalikuwa yakianzia makao makuu ya
mkoa na kwenda kwenye wilaya zote. Lakini kumbukumbu hizo zinaonyesha
kwamba yalifanyika Mwanza, Musoma, Shinyanga, Kagera na mikoa ya Nyanda
za Juu kusini (Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa) kisha nayo yakafa kifo
cha mende. Kisha mwaka 2012 ikaanzishwa operation ya mabadiliko maarufu
kama Movement for Change (M4C). Hiyo ilikuwa inakwenda kwenye mikoa na
timu kama nne hivi ambazo kwa ujumla zilitathmini hali ya mtandao na
uongozi wa taasisi, kuhamasisha umma kwa njia ya mikutano ya hadhara,
kuingiza wanachama na kusimika uongozi na hatimaye kufanya mafunzo kwa
viongozi. Hiyo ikafanyika Mtwara na Lindi, Morogoro na kisha ikaenda
kufia Iringa. Mwaka huu viongozi wetu wamekuja na ugatuaji madaraka
kutoka makao makuu ya taasisi na kupeleka madaraka kwenye kanda
mbalimbali. Mkakati huu ulikufa kabla ya kuanza pale viongozi wakuu
walipobadilisha maazimio ya kikao kikuu na kutekeleza matakwa yao ikiwa
ni pamoja na kuleta suala la viongozi wa muda kwa muda mrefu badala ya
kuajiri maofisa na wakahakikisha wanaweka watu wao kwenye uongozi wa
muda. Kitendo hiki kwa peke yake, cha kufeli kwa kila mkakati unaoletwa
na viongozi wetu katika hatua za utekelezaji unaofanywa na wao wenyewe
waleta mkakati, ni kiashiria tosha kwamba uongozi uliopo umechoka.
Performance yetu kwenye chaguzi ndogo nayo ni ishara kwamba mabadiliko
yanahitajika. Tangu uongozi huu uingie madarakani, kumefanyika chaguzi
ndogo 8 za wawakilishi kwenye chombo kikuu, kati ya hizo tumeshinda 2 tu
sawa na asilimia 25. Aidha baada ya mwaka 2010 kumefanyika chaguzi
kadhaa za wawakilishi kwenye halmashauri. Mwezi Oktoba 2011, mwezi wa4
2012, mwezi Septemba 2012 na mwezi Juni 2013. Kote performance yetu
imekuwa poor kupindukia. Mfano mwezi wa Juni 2013 tumepata viti 6 kati
ya 22 (27%) na mwezi Septemba 2012 tulipata viti 7 kati ya 29 (24%). Ni
dhahiri mabadiliko yanahitajika kwa kuwa wakuu waliopo wanatumia mbinu
zile zile na kupata matokeo yale yale. Tunahitaji mbinu mpya. Kwa
kifupi, ushindi ambao tumekuwa tukiupata katika chaguzi ndogo haulingani
na ukubwa wa hamasa kwa taasisi yetu iliyopo mitaani. Hii ni kwa sababu
tumekuwa tukitumia mbinu hizohizo katika kila chaguzi. Aidha, tu wepesi
mno wa kuridhika na kujisifu kwa mafanikio madogo badala ya kukaa chini
na kutafakari kwa kina mahala tunapojikwaa.
Matumizi ya fedha za taasisi. Hakuna mtu anayejua hivi sasa fedha za
chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu yaani mkuu kabisa,
mtendaji mkuu na mkuu wa fedha kwenye taasisi yetu. Maamuzi ya vikao
hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi wa 2010 vikao
halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa bali
zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Lakini leo
si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha.
Watu watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje. Mfano mwingine ni maamuzi ya
kikao cha juu mno cha hivi karibuni kilichoamua kwamba kiasi cha fedha
inayotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa na wilaya na kiasi kingine
kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa tano maamuzi hayo
hayajatekelezwa. Lakini kuna michango ya watu binafsi kama yule
mtanzania mwenye asili ya kihindi, hizo nazo hazijulikani zimechukuliwa
lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje. Hapo
hatujataja fedha zinazopatikana kutoka kwenye fundraising events
mbalimbali kama ile ya Dar es salaam na Mwanza. Hizo nazo hazijawahi
kuonekana na walioendesha hizo fundraising, uaminifu wao kwenye masuala
ya fedha ni questionable.
Taarifa za fedha. Tokea baada ya uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna
kikao chochote kilichowahi kupokea na kujadili hadi mwisho ripoti ya
mapato na matumizi ya fedha za taasisi. Kila kikao agenda hiyo inarushwa
kiaina. Wanaojua mchezo huo ni watu watatu tu tuliowataja hapo juu na
malengo ya kurusha hiyo agenda kila wakati na kukwepesha isijadiliwe pia
wanayajua wao. Ni dhahiri tukiendelea na hawa watu tutafika 2015 tukiwa
hatuna pesa hata ya kuweka mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa
tumesimama. Kwa kiasi kikubwa mkuu aliyepo anatengeneza mazingira
yaleyale ya mwaka 2005 na 2010 ya kutaka chama kiwe hakina hela ili
ikifika wakati wa uchaguzi kimpigie magoti. Kisha atatoa pesa bila
kumbukumbu zozote na mara baada ya uchaguzi anapeleka lundo la deni na
kudai alipwe hela aliyekikopesha chama wakati wa uchaguzi. Alifanya
hivyo katika chaguzi za 2005 na 2010. Wakati wote wa kampeni za mwaka
2010, kwa mfano, taasisi yetu ilihangaika sana kwa kukosa hata hela ya
kununua maji kwa wajumbe wa ngome. Lakini ajabu ni kwamba baada ya
uchaguzi mkuu wa taasisi na baadhi wa wapambe wake walilete deni kubwa
la takribani shililingi milioni mia tano akiadi kuwa walikikopesha
chama. Taasisi imewalipa pesa zote hizi kwa muda mwaka mmoja. Sasa
anatengeneza mazingira hayohayo kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Mipango ya kukipatia chama mapato ya ziada kutoka nje ya chama. Wakuu
waliopo hawana hata ndoto ya namna ya kupata fedha za ziada.
Wanachokijua ni kukusanya ‘sadaka’ kwenye mikutano ya hadhara na
kuwapatia kazi watu wanaoonekana kuwa matapeli eti waendeshe harambee za
kuchangisha fedha kwa njia ya matukio. Mawazo mazuri kama lile la
kuanzisha kampuni la uwekezaji la taasisi yetu litakalowekeza kwenye
miradi mbalimbali, halijawahi kufanyiwa kazi, na hivyo uanzishaji wa
miradi mbalimbali ya kuiingizia taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana.
Hatuwezi kufika hata siku moja bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa
hapa jirani juzi juzi wakuu wetu ingawa walishiriki lakini hawaonekani
kama wamejifunza chochote.
Njia haramu za kubaki madarakani. Ili kuhakikisha wakuu wanabaki
madarakani, wameanzisha vikundi vikundi ndani ya taasisi yetu. Siku hizi
ni rahisi sana kuambiwa kwenye taasisi yetu eti huyu ni wa boss na huyu
ni wa dogo. Na wale walio wa boss kwa kuwa boss ndo anashikilia
raslimali za taasisi anatumia mfumo haramu kuwaneemesha watu wake kwa
kutumia raslimali za taasisi na kuwakandamiza wote wanaoonekana
wanapishana naye kimtazamo. Jambo hili limewaibua wachumia tumbo,
wapenda madaraka, na vibaraka lukuki wanaokwenda kujipendekeza kwa wakuu
wa taasisi kwa malengo ya kujinufaisha binafsi. Katika kufanya hivyo
vibaraka hao wamekuwa wakiwaendea wakuu wa taasisi na kuwajaza maneno
mabaya dhidi ya viongozi wenzao na kuzidi kuwafarakanisha viongozi wa
juu.
Kuna mchezo umeanzishwa na wakuu wa taasisi unaitwa ulinzi wa chama
uliogawanyika katika makundi mawili yaani visible na invisible. Visible
ni ule unaoonekana ambao uko chini ya kikosi chetu chekundu ambacho
kinajulikana kwa kila mtu lakini invisible wanajulikana kwa mkuu wa
taasisi na mtendaji mkuu peke yake. Wanafanya kazi kwa maelekezo ya
wakubwa hao wawili na hawajulikani kwa viongozi wengine wa juu. Ni hawa
hawa ambao wanatumika vibaya pale wanapoleta taarifa za kiintelijensia
ambazo zinawahusisha viongozi wasiopendwa na wakuu na usaliti dhidi ya
taasisi. Hakuna kamati maalum inayowathibitisha maaintelijensia hao bali
wakuu wenyewe wanawachukua wanaowataka. Ni katika mfumo huu wa kipuuzi
mida eight amekuwa akitumika vibaya kwa kumshambulia mtendaji mkuu
msaidizi hadharani kwa kutumia mitandao ya kijamii na wakuu wanafurahia
na kumlipa pesa.
Udhaifu wa utendaji wa mtendaji mkuu. Mtendaji mkuu ni dhaifu mno na ni
mara nyingi sana tumeshuhudia mkuu wa taasisi akifanya mambo ya
kiutendaji kinyume na utaratibu kama vile yeye mwenyewe kuja kwenye
kamati ya makatibu na wakurugenzi na kupangua mipango yao na ku-inject
ya kwake na mtendaji mkuu kuadopt tu kana kwamba yeye hawezi kupanga
mambo ya kiutendaji, hata tunapokuwa kwenye operesheni maalum
tumeshuhudia mkuu wa taasisi ndo akipanga watendaji, posho zao na hata
kusimamia matumizi ya pesa na shughuli mbalimbali za kiutendaji. Udhaifu
wa mtendaji mkuu ni udhaifu wa mkuu wa taasisi kwa kuwa amemteua yeye
mara mbili tena mara ya pili alileta jina moja mbele ya Baraza la juu
kuonyesha kwamba aliridhika na utendaji wake kiasi cha kutotaka
kumpambanisha na mwingine. Lakini baada ya kumpendekeza mara ya pili
ndipo tumeshuhudia yeye kuingilia kati mara nyingi sana mambo ya
kiutendaji kana kwamba anamfichia aibu mtendaji wake. Swali kwa nini
alimteua tena? Jibu lake litakuwa rahisi tu kwamba ni kwa sababu
mtendaji huyu ni passivekwa kila takwa la mkuu wake.
Matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi. Taasisi
yetu inayo kamati ya tenda ambayo iko chini ya kamati ya makatibu na
wakurugenzi. Lakini uzoefu unaonyesha kwamba kamati hii haifanyi kazi
imezimwa kimya kimya na wajumbe wote wa kamati ya tenda kwa kuwa ni
wachumia tumbo wanaojigonga kwa wakuu, wamekubali kuzimwa. Leo ikidaiwa
kamati hiyo ilete nyaraka za mchakato wa manunuzi ya magari, pikipiki,
vifaa vya kueneza taasisi, set ya televisheni iliyofungwa ofisini kwa
mtendaji mkuu, hawana. Manunuzi haya yote yote yanafanywa na wakuu hasa
hasa mkuu wa taasisi bila utaratibu wowote jambo ambalo ni hatari na
linarahisisha matendo ya kifisadi. Bila aibu, mkuu wa taasisi ndio
amekuwa mnunuzi wa vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua
mwenyewe na ambaye haihojiwi popote. Huu ni mfano wa wazi wa mgongano wa
kimaslahi jambo ambalo ni hatari kwa kiongozi mkubwa wa taasisi kama
yetu inayojitambulisha katika kupinga vitendo vya ufisadi na uvunjifu wa
maadili ya uongozi kwa ujumla.
Makubaliano ya kifisadi na mtu binafsi anayeuza vifaa vya kueneza
taasisi. Hakuna kikao chochote cha juu kilichojadili ama kilichowahi
hata kupewa taarifa tu kwamba sasa kuna mtu binafsi kapewa tenda ya
kuuza vifaa vya taasisi na taasisi inanufaika vipi na mauzo hayo na kwa
nini vifaa muhimu vya taasisi vinauzwa. Jambo hili linajulikana kwa
wakuu tu.
Mifumo ya uteuzi wa maofisa wa makao makuu ya taasisi imevurugwa na siku
hizi wakuu wa taasisi hasa mtendaji mkuu anateua na kutimua ofisa
anavyotaka na mara nyingi bila hata kamati ya makatibu na wakurugenzi
kujua. Mambo haya yanafanyika mbele ya macho na masikio ya mkuu wa
taasisi jambo ambalo linazidi kuthibitisha kwamba mkuu na mtendaji mkuu
wanajuana na wanafanya kwa kulindana.
NANI TUMUUNGE MKONO KUCHUKUA NAFASI YA MKUU:
Baada ya utangulizi huo unaoonyesha kinagaubaga kwamba tunahitaji
mabadiliko, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuangalia nani anaweza kuleta
mabadiliko tunayohitaji. Ni vema ikazingatiwa kwamba mtu ambaye
tungemuunga mkono lazima awe ni mtu mwenye uwezo mkubwa kuliko
tunayetaka kumtoa. Awe ana qualities za kiuongozi na zaidi sana awe na
uwezo wa kupambana na mkuu aliyeko. Tukileta mtu asiyefahamika sana
kwenye mifumo ya taasisi yetu hata kama angekuwa mzuri kiasi gani
hatachagulika na mkuu aliyeko atarudi kwa urahisi na kuendelea
kuididimiza taasisi.
Katika kuchunguza ndani ya taasisi tuliridhika kwamba mtendaji mkuu
msaidizi ana sifa zote tulizozitaja hapo juu ingawa kila mwanadamu ana
udhaifu wake. Ni dhahiri pia kwamba udhaifu wa mtendaji mkuu msaidizi
unarekebika kuliko wa mkuu aliyepo. Kwa ujumla mtendaji mkuu:
Ni kiongozi anayeweza kuongoza taasisi bila kujenga makundi akijali zaidi kazi ya taasisi kuliko maslahi binafsi.
Ameonyesha kwa vitendo kwamba hana maslahi binafsi kwa kuwa tumeshuhudia
akifanya kazi nyingi za taasisi bila kudai malipo kwa njia ya posho ama
vinginevyo.
Anaheshimika na viongozi wa ndani na nje ya taasisi jambo ambalo ni la
muhimu sana kwa ustawi wa taasisi na kwa yeye kuwa mkuu wa taasisi
tunatarajia wakubwa wengi sana kutoka nje ya taasisi yetu kuiamini na
hata kujiunga nasi katika kuhakikisha tunafanikisha lengo la taasisi.
Ni msomi wa kiwango cha juu na mwenye uwezo mkubwa katika kuchanganua
mambo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kimichezo, nk jambo ambalo ni
muhimu sana kwa kuwa ni hatari kuwa na kiongozi asiye na ujuzi wa
kutosha kwenye masuala kama hayo.
Ndani ya taasisi anakubalika kwa makundi yote ya vijana, wazee na akina mama.
Uongozi wa sasa wa taasisi yetu umefanya tuonekana kwamba taasisi yetu
ipo kwa ajili ya kuvuruga amani ya nchi. Yote hii ni kwa sababu tumekuwa
hatuna mbinu mpya za mapambano zinabadilikabadilika zaidi ya maandamano
ya kila mara. Kwa kuzingatia utamaduni wa watanzania wa kupenda amani,
kuna haja ya kufuta hii taswira na njia rahisi ni kubadilisha uongozi wa
taasisi haraka iwezekanavyo.
Uelewa wake wa mambo ya kiuchumi ni muhimu sana kwa taasisi kwa sasa.
Tunahitaji kuja na vyanzo vipya vya mapato ikiwa tunahitaji kufanikiwa.
Mkuu aliyepo si kwamba ameishiwa bali hana mbinu za maana za kuiimarisha
taasisi kimapato kwa ajili ya malengo yake ya mbele.
Exposure kubwa na kukubalika katika siasa za kimataifa. Tunahitaji
kiongozi ambaye anazifahamu siasa za kimataifa na anayeweza kuungwa
mkono na viongozi wengi wa kimataifa. Ni hatari kutegemea utaweza
kufanikisha malengo kama ya taasisi yetu bila mpango kabambe wa kuungwa
mkono na jumuia ya kimataifa. Mpaka hivi sasa hakuna mpango wowote wala
hata mchakato wa maana kuwa connected na jumuia ya kimataifa. Kiongozi
wetu mkuu wa sasa yupo ‘too local’ na hana mawasiliano yeyote ya maana
na viongozi wengine katika kanda na kimataifa. Ndio maana mkuu huyo na
mtendaji wake mkuu wamekuwa hawaonekani katika matukio makubwa ya
kimataifa. Hata katika kutoa maoni katika mambo makubwa ya kitaifa na
kimataifa viongozi hawa hawapo. Kwa kifupi kwa sababu ya aina ya
viongozi tulio nao, nafasi ya taasisi yetu katika nyanja za kimataifa
haipo!
Aina na staili ya uongozi wa sasa wa taasisi yetu ni kina kwamba nchi
hii haipo hadi taasisi yetu itakapochukua dola. Yaani tunafanya mambo
kama kwamba tutaanza upya kabisa tukichukua dola. Ni kwa sababu
tumegombana na kila mtu katika utawala wan chi, vikiwemo vyombo vya
ulinzi na usalama. Ukweli ni kwamba tutavihitaji vyombo hivi kabla na
baada ya kuingia madarakani na ni ndoto kudhani kwamba tutakabidhiwa
nchi kwa kugombana na kila mtu. Ni kwa sababu ya mtazamo kama huu ndio
maana wakuu wetu wa sasa hawaonekani kabisa katika shughuli za kitaifa
kama vile sherehe za uhuru wan chi, n.k.
Uwezo wa kuwaunganisha wasomi wa kada mbalimbali, wafanyabiashara
wakubwa, watumishi wa umma na sekta binafsi, nk katika kupata muunganiko
wa mawazo na kutoka na sera murua zinazogusa kila sekta. Hili la
kuwashirikisha litaenda sambamba na kutoa elimu kwa wote waelewe na
watuunge mkono. Tunasema hivi kwa kuwa watu wa kada mbalimbali
hawajaelewa sera zetu juu ya mambo yanayowahusu mfano wafanyabiashara
wakubwa, wawekezaji, wakulima, watumishi, wanafunzi,nk na hivyo hawajawa
tayari kutuunga mkono. Kile kinachofanywa wakati wa uchaguzi kwa njia
ya ilani ya uchaguzi na elimu kutolewa kwa njia ya kampeni majukwaani
hakitoshi. Tunahitaji watu wajue tumeunda think tank kwa ajili hiyo na
baadaye wajue nini kimetokana na think tank hiyo ili wajadili na kutoa
maoni na hatimaye tutoke na kitu kinachokubalikwa na wananchi wote. Na
tuna imani hilo tunayempendekeza ana uwezo nalo.
Kubwa zaidi ni kwamba alishaiangalia taasisi yetu na kuona mambo
yanayohitaji mabadiliko na kujiangalia yeye na kuridhika kwamba ataweza
kuleta mabadiliko tunayoyahitaji na ndipo mwaka 2009 aliamua kujitosa
kuutafuta ukuu wa taasisi yetu kabla ya kuombwa kumwachia aliyepo.
SWOT ANALYSIS:
Kwa kutumia uchambuzi huu hapa chini wa uimara, udhaifu, fursa na
vitisho ama vikwazo dhidi ya mtu tunayempendekeza, utaweza kutuonyesha
kama tunayempendekeza ataweza kushinda vita iliyo mbele yetu. Kama SWOT
inavyotaka, tutaangalia sifa njema alizonazo tunayemtaka ambao ndio
uimara wake, tutaangalia pia udhaifu wake, tutaangalia fursa alizonazo
na mwisho tutazingatia vitisho ama vikwazo vilivyopo. Ni muhimu
tukaeleza kwamba katika SWOT analysis tunajikita kwa mambo yanayohusika
moja kwa moja na uwezekano wa tunayemtaka, kuchaguliwa. Kwa hiyo kwa
mfano utakuta kwamba katika sehemu hii hatutazungumzia sifa njema
alizonazo tunayemtaka kama kiongozi lakini sifa hizo zikawa hazina
ushawishi wa kuwafanya wajumbe wa kikao cha uchaguzi kumchagua.
Uimara wa tunayemtaka:
Ingawa si mmoja wa waasisi wa taasisi yetu, lakini ni mwana taasisi
mkongwe akiwa amejiunga na taasisi yetu miaka miwili tu tangu ianzishwe
na mwaka mmoja tangu isajiliwe rasmi na serikali.
Zaidi ya kuwa mwanataasisi mkongwe, hajawahi kujiunga na taasisi
nyingine hapo kabla. Alijiunga na taasisi hii kabla hata haijajulikana
kwa watu na alibaki kuwa mwana taasisi mwaminifu hata pale taasisi
zingine zilipoonekana kuwa imara na maarufu zaidi ya hii.
Kutokana na vipengele ‘a’ na ‘b’ hapo juu, hakuna mtu hata mmoja
anayeweza kusema mtu huyu alikuja kwenye taasisi yetu kwa ajili ya
kutafuta maslahi kama vile uwakilishi kwenye chombo chetu kikuu cha
uwakilishi hapa nchini.
Ni mvumilivu sana. Katika jitahada za wakuu waliopo kuhakikisha
wanaendelea kukalia viti vyao, wamejitahidi sana kumpaka matope lakini
amevumilia. Mahali ambapo wengine wangeshakata tamaa na kuhama taasisi,
yeye alibaki kuvumilia mpaka imefikia wana taasisi wa ngazi za chini
waliokuwa wanadanganywa kwamba mtu huyu ni msaliti, wameanza sasa
kushtuka.
Ana historia nzuri ya utendaji uliotukuka ndani na nje ya chombo cha uwakilishi.
Ana uwezo mkubwa wa uelewa wa mambo mbalimbali ya uchumi, jamii,
utamaduni, michezo, nk. Uwezo wake unachagizwa si tu na elimu yake ya
darasani bali pia vipaji na akili ya kuzaliwa.
Ni mzalendo wa hali ya juu anayeipenda nchi yake kwa moyo wa dhati.
Amethibitisha hilo kwa namna anavyolitetea taifa letu katika medani za
kimataifa na jinsi anavyolipigania ndani dhidi ya mafisadi na
wasiolitakia mema taifa letu. Ni mwakilishi pekee aliyekuwa tayari
kukosa mishahara ya miezi kadhaa kwa kuamua kusimamia ukweli kwamba kuna
ufisadi ulifanyika mpaka akasimamishwa uwakilishi wake kwa mikutano
kadhaa ya chombo chetu cha uwakilishi.
Katika kuzidi kuonyesha alivyo mzalendo tunaweza kusema hapa kwamba ni
kiongozi pekee kutoka upande huu ambaye ameonekana sana kwenye mambo ya
kitaifa kwa mfano kulipigania taifa letu katika mambo ya kimchezo,
kutumia gharama zake kwenda nje ya nchi na kujifunza mambo mbalimbali
yanayoweza kulisaidia taifa katika sekta nyeti kama mafuta, gesi na
madini, nk bila kusahau kwamba amekuwa ndiye mwakilishi pekee
aliyeongoza katika kuibua kashfa nyingi na nzito za ubadhirifu ndani ya
serikali hata kufikia mawaziri kadhaa kufukuzwa kazi.
Mambo hayo tuliyoyataja kwenye vipengele ‘e’, ‘f’, ‘g’ na ‘h’ yamemfanya
kuwa kiongozi wa kwanza kuwa maarufu sana katika taasisi yetu
aliyewapiku hata viongozi wa serikali kwa umaarufu. Hii ya umaarufu ni
sifa muhimu sana linapokuja suala la uchaguzi.
Uwezo wake wa kujieleza kwa kujenga hoja pale anapopewa nafasi. Hata
pale anapokuwa amepakwa sana matope na wenzake, anapopewa nafasi ya
kujieleza huweza kuwashawishi watu wengi wanaomsikiliza. Hii itamsaidia
sana siku ya kujieleza mbele ya kikao cha uchaguzi ambapo ataweza
kupangua hoja zote dhaifu za kumpaka matope.
Ana uwezo wa kuchangamana na makundi yote ambapo vijana humwona kama
mwenzao, wanawake humwona kama mtetezi wao wakati wazee humwona kama
kijana mwenye busara anayeweza kuelekeza kama kiongozi.
Ana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za chini kutokana na
ziara nyingi alizozifanya na kukutana na viongozi wa ngazi za chini
akiwa katika kuijenga taasisi hii. Mahusiano haya mazuri yanachagizwa na
jinsi anavyotumia muda wa kuongea na viongozi wa ngazi za chini
kuzungumza kwa lugha ya upole na kuelekeza viongozi wenzake bila
kuwaonyesha dharau.
Si mtu wa kujipenda nafsi na katika kupambana umaskini wa watu badala ya
umaskini wake, alifikia kuzikataa posho wanazolipwa wawakilishi wakati
wakitekeleza majukumu ambayo kwayo wanalipwa na kuiomba ofisi ya chombo
hicho kuzipeleka posho hizo kwa watu maskini.
Ana limu nzuri sana aliyoipata katika vyuo vinavyoeleweka kitaifa na kimataifa
Ni kijana na hii ni taswira njema kwa sababu taasisi yetu inaungwa mkono sana na vijana
Udhaifu wa tunayemtaka:
Maneno yake mara nyingine hayazingatii anayazungumza katika mazingira
gani na hivyo kuwasha masikio ya wanataasisi jambo linalompunguzia
kukubalika kwake taratibu.
Kama ilivyo kwa maneno, kuna matendo pia ambayo mara nyingine huyafanya
bila kuzingatia mazingira na wasikilizaji wake na hivyo kupunguza imani
ya wana taasisi kwake.
Hali ya ndoa ya tunayemtaka kutoeleweka msimamo wake
Kuna wakati tunayemtaka hu-respondkwa taharuki kubwa dhidi ya
mashambulizi yanayoelekezwa kwake jambo linalomfanya achukue maamuzi
yasiyo sahihi kwa wakati huo. Kwa kifupi kuna wakati tunayemtaka
huonekana kufanya maamuzi kwaemotion zaidi badala ya kutulia kwanza na
kutafakari kwa kina ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri kwa wenzake
kabla ya kurespond.
Jambo lililoelezwa katika ‘d’ hapo juu humfanya tunayemtaka wakati
mwingine kuonekana ana jazba sana kwa sababu akishataharuki na kuchukua
maamuzi akingali kwenye taharuki huwa ni rahisi sana kuonekana anajibu
mapigo kwa jazba sana.
Ustahimilivu: yaliyotajwa katika ‘d’ na ‘e’ hapo juu yanaashiria tunayemtaka si mstahimilivu sana sifa ambayo inahitajika sana kwa kiongozi.
Uwazi: Katika taasisi zetu hizi ni muhimu sana kuepuka kufanya mambo
yote wazi wazi hata kama ni mema ama ni haki ya mhusika ama si makosa
katika jamii tuliyomo. Kuna mambo ambayo ni haki ya mtu mfano mahusiano
binafsi ya kimapenzi, kuwa na marafiki wa damu kutoka upande mwingine wa
utawala, nk. Lakini mambo hayo ni muhimu wakati mwingine ama kwa
kiwango fulani yakafanywa kwa siri kuepuka mitazamo potofu kwa
unaowaongoza.
Fursa alizonazo tunayemtaka:
Utamaduni wa taasisi yetu wa kubadilisha wakuu wa taasisi kila baada ya
vipindi vifupi ili kuleta maono mapya kwenye taasisi unampendelea
tunayemtaka.
Udhaifu ulioonyeshwa na uongozi uliopo chini ya mpinzani wetu katika
kutekeleza program mbalimbali za taasisi nyingi zikiwa zimebuniwa na wao
wenyewe, pia ni fursa kwa tunayemtaka.
Udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na uongozi uliopo kwenye ugawanyaji wa
raslimali za taasisi kama vile fedha za ruzuku, michango mbalimbali ya
wahisani na hata vifaa vya uenezi.
Kujitokeza kwa tunayemtaka kutaonekana kama fursa kwa wanataasisi
kufanya mabadiliko makubwa na kuua kabisa ile propaganda ya kwamba
taasisi yetu ni ya kabila fulani ama eneo fulani kwa kufanya reference
kwa uongozi wa taasisi.
Hoja ya uongozi uliopo kushindwa kabisa kusoma taarifa za fedha tokea
2010 ikifahamika kwa wapiga kura inaweza kuwa machinjio kabisa ya
uongozi uliopo na kumpa fursa kubwa tunayemtaka.
Imani ambayo wana taasisi wengi wanayo kwake. Utafiti mdogo unaonyesha
kwamba bado jina la tunayemtaka linatamkika sana midomoni mwa
wanataasisi pale wanapotajwa viongozi wa juu wa taasisi yetu. Hii
inaonyesha bado wana taasisi wanayo imani kubwa kwake na kwa hiyo
atakapopata fursa ya kupangua matope aliyopakwa atakuwa na nafasi kubwa
ya kuchaguliwa.
Mpinzani wetu hana historia nzuri ya utendaji uliotukuka ndani na nje ya
chombo cha uwakilishi. Hakuonyesha utendaji wowote wa pekee alipokuwepo
kwenye chombo mwaka 2000 -2005 na hata alipopewa uongozi wa upande wetu
ndani ya chombo tokea 2010 hadi leo 2013 hajafanya lolote la kutukuka
ndani ya chombo hicho.
Mpinzani wetu hana uwezo mkubwa wa uelewa wa mambo mbalimbali ya uchumi,
jamii, utamaduni, michezo, nk. Si tuelimu yake ya darasani ni ya
magumashi bali pia vipaji na akili ya kuzaliwa havijaonekana katika
maisha yake.
Uzalendowampinzani wetu unatia shaka akiwa hajaonyesha lolote la maana
katika kulitetea taifa letu kimataifa. Ingawa ameshapata nafasi lukuki
ya kwenda nje ya nchi lakini mara zote akifika huko ni kuiponda tu nchi
yake. Ingawa anayo majukwaa ya kufanya hivyo akiwa ameshakuwa mwakilishi
mara mbili kwenye chombo chetu lakini hatujawahi kumsikia akiibua
kashfa mahsusi ya ufisadi na kuisimamia zaidi ya yeye mwenyewe wakati
fulani fulani kutuhumiwa kwa ufisadi mfano pale alipokopa kwenye shirika
la umma na kugoma kulipa mkopo.
Katika kuzidi kuonyesha uzalendo hafifu wa mpinzani wetu tunaweza
kuangalia jinsi ambavyo mpinzani haonekani kwenye mambo ya kitaifa. Hii
ni fursa kwa tunayemtaka.
Mpinzani wetu si maarufu akilinganishwa na tunayemtaka na hivyo kumpa
fursa zaidi tunayemtaka kumshindani mpinzani wetu kwenye uchaguzi.
Uwezo wa mpinzani wetu wa kujieleza kwa kujenga hoja pale anapopewa nafasi ni mdogo sana.
Mpinzani wetu hajazoea ushindani na changamoto. Ni mtu aliyezaliwa
kwenye utajiri na anadhani pesa ni kila kitu. Ukimnyang’anya pesa
ukamwambia ashindane kwa hoja hawezi na ndo maana anajaribu sana
kuhakikisha anaingia mwenyewe ulingoni bila kupingwa.
Kutokana na tuliyoyasema hapo juu kwenye ‘m’ ni dhahiri kwambapale
mpinzani wetu anaporushiwa kombora la kashfa anakuwa mzito kujieleza
hata kama anapewa nafasi ya kufanya hivyo na hii ni fursa muhimu kwa
tunayemtaka.
Mpinzani wetu ni mgumu sana katika kuchangamana na makundi yote ambapo
vijana humwona kama si mwenzao kiumri na kifedha, wanawake humwona kama
malaya anayependa kutumia miili yao kujistarehesha wakati wazee humwona
kama mtu anayedhalilisha hata nafasi aliyopewa kwa kufanya uhuni
waziwazi hata kuvunja ndoa si ya kwake tu bali hata za watu wengine.
Mpinzani wetu hana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za
chini kutokana na dharau nyingi anazozionyesha pale anapokukutana na
viongozi wa ngazi za chini akiwa katika kuijenga taasisi hii. Hutumia
muda mwingi kuwaponda viongozi wenzake hata kufikia kutamka mara nyingi
kwamba kama kiongozi hawezi kujigharamia nauli na malazi ya kutoka
mahali fulani kwenda mahali fulani kwa siku kadhaa hafai kuwa kiongozi
bila kujali kwamba kuna viongozi wetu wana moyo na taasisi hii na ndo
wameifikisha hapa ilipo lakini hawana uwezo wa kifedha na hivyo kauli
kama hizo za mkuu huyu huona kama anawadharau kwa kuwa yeye ni tajiri.
Hii imemfanya kutopendwa na viongozi wengi wa ngazi ya chini hivi sasa
na kutoa fursa ya pekee kwa tunayemtaka.
Mkuu aliyepo amekuwa na mkakati unaoitwa kuondoa watu wa zamani. Jambo
hili linawaudhi sana viongozi wa ngazi za chini ambao wanaona kama baada
ya kuifikisha taasisi mahali ilipo kwa sasa wanaonekana hawana maana
tena. Wengi wamefikia kuapa kwamba kama mwendo ni wa kuwaondoa watu wa
zamani basi na yeye ni wa zamani lazima aondoke.
Mpinzani wetu amejionyesha dhahiri kujipenda na kujijali nafsi bila
kujali watu wa hali ya chini. Matukio mawili yanamwacha uchi katika hili
pale alipolitangazia taifa kwamba wawakilishi wetu wote hawatachukua
posho za vikao halafu yeye na wengine wote wanazichukua hadi leo na
kumwacha mtendaji msaidizi peke yake. Na la pili linalofanana na hilo ni
pale alipotangaza kutotumia gari la serikali ambalo ni la kifahari
kisha akalirudia kimya kimya.
Kuwepo muhtasari wa kikao cha wazee ambacho mwaka 2009 kilimshauri
tunayemtaka ajitoe na kumwachia mkuu aliyepo na kumtaka mkuu aliyepo
kumwachia tunayemtaka katika uchaguzi ujao na wote wakasaini makubaliano
hayo, nayo ni fursa muhimu sana kwa tunayemtaka.
Mkuu aliyepo anaamini kwamba ameshamsambaratisha tunayemtaka na hivyo
kwa sasa amebweteka na hiyo inatupatia sisi fursa kuendelea kuimarisha
mtandao wetu.
Kwa kuwa ni mwislamu. Hii ni fursa katika kupata kuungwa mkono na
wanachama waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani waislamu
hawatakiwi katika uongozi wa taasisi yetu.
Elimu ndogo na duni aliyenayo mpinzani wetu ambaye ndiye mkuu wa taasisi
yetu kwa sasa. Kwa sasa ni kiongozi pekee katika nchi yetu anayeongoza
taasisi kubwa asiye na elimu ya shahada huku taasisi yetu ikiwa
inaongoza kwa kuwa na wasomi waliobobea katika kila nyanja. Hii ni
kejeli hasa kwetu sisi ambao tumekuwa tukiwasema wenzetu kwamba ‘akili
ndogo’ inaongoza akili kubwa. Kimsingi tumekuwa tukijisema kwa kukubali
kuongozwa na mtu mwenye akili ndogo.
Mkuu wa sasa kutokuwa na msimamo thabiti katika mambo ya msingi. Rejea
swala la maandamano ya kumshinikiza Kawambwa ajiuzulu na kujitoa katika
mchakato wa katiba.
Vikwazo dhidi ya tunayemtaka:
Sisi wenyewe tunaoandaa mkakati huu hatuna uhakika kama tunayemtaka yuko
tayari na yuko serious na business hii, na kwa hiyo huenda tusifanye
kwa nguvu zetu zote ikiwa hatutapata nafasi mapema ya kukutana na
mhusika na akatuhakikishia kwamba yuko serious.
Utayari wa mhusika mkuu kutekeleza yale tunayokubaliana. Inapotokea
baada ya kukubaliana sisi na yeye akapata ushauri tofauti na ukauona uko
more genuine, basi tuwasiliane kwamba nimeshawishika kufanya hivi
badala ya vile tulivyokubaliana kwa sababu hizi ama zile. Hii
haitatukatisha tamaa tofauti na kama tutakuwa tunapanga hivi halafu yeye
anafanya vile bila maelezo yoyote
Kitendo cha mkuu aliyepo kung’ang’ania kuendelea nayo ni kikwazo kwa
kuwa baada ya kuwa madarakani kwa miaka yote hiyo lazima amejipatia watu
wanaomhusudu ama kumpenda ama kumkubali na kuwepo wengine wanaoogopa tu
kwamba mkuu aliyepo akitoka taasisi itakufa hata kama hawana sababu
yoyote.
Tunatazamia mkuu aliyepo atafanya vitendo vingi zaidi vya haramu katika
kumdhibiti tunayemtaka pale tunapoelekea kwenye uchaguzi wenyewe.
Raslimali za taasisi kutumiwa na viongozi waliopo katika kumsaidia mkuu
aliyepo wakati wa kwetu anatumia raslimali zake za mfukoni.
Propaganda chafu zilizokwishapigwa dhidi ya tunayemtaka zimepunguza imani ya wanataasisi kwa tunayemtaka kwa kiasi fulani
Baadhi ya mambo ambayo amekwishayasema ama kuyatenda nayo yameshawapunguzia imani kiasi fulani wanataasisi mbalimbali.
Kutoonekana sana kwenye operations za taasisi yetu pia kumewapa wasiwasi baadhi ya wanataasisi.
Muhtasari wa SWOT analysis unaonyesha kwamba strength na opportunities
za tunayemtaka ni nyingi sana zikilinganishwa na weaknesses zake na
threats dhidi yake. Aidha ukichambua zaidi utaona kwamba weaknesses za
tunayemtaka nirepairable na vikwazo dhidi yake pia ni rahisi kuvikabili
na kuvisambaratisha. Tukishamaliza maandalizi ya mkakati huu tukaonana
na mhusika mkuu na kumpa ushauri akatulia na kufanya kazi, mkuu aliyepo
hatafua dafu. Tunahitaji kutekeleza mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu
aliyepo aendelee kubweteka na ndiyo maana hata lugha iliyotumika ni
ndani hapa ni ya pekee. Tunahitaji tunayemtaka asionekane kama kuna kitu
anafanya na tunafurahi kwamba kuna wakati alitangaza kwamba hana nia ya
kugombea tena waliopo wanatosha. Ikitokea vyombo vya habari vikamuuliza
tena hiyo ndiyo iwe kauli yake ili kuendelea kumfanya mkuu aliyepo
asihangaike na hivyo kuja kummaliza kirahisi. Aidha katika utekelezaji
wa mkakati kama tutakavyoeleza hapo baadaye, tunayemtaka atajitenga
mbali asionekane hata kuwa karibu na sisi. Vikao vyetu na yeye
vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha kupita kiasi
ikiwezekana hata nchi jirani.
Mkakati huu hautatakiwa kupatikana kwenye komputa zaidi ya tatu yaani ya
mchapaji ambaye ni M3, ya M3 na ya MK mwenyewe. Hata hivyo email
zitakazotumika kusafirisha mkakati huu kutoka kwa M3 kwenda kwa M1 hadi
kwa MK hazitakuwa zile za kawaida za hao watu bali mpya kabisa
zilizofunguliwa kwa makusudi haya tu na kwa majina fictitious. Aidha
kila atakayekuwa na mkakati huu kwenye computer yake anatakiwa kuliwekea
file hilo password ili hata mtu wa karibu naye anayeweza kufungua
computer yake asiweze kulifungua file hilo. Pia email address
hazitatolewa kwa sms bali kwa kupiga na kuambiana spelling za address.
MTANDAO WA USHINDI:
Mtandao wa ushindi utakuwa kama ifuatavyo. Kwenye ngazi ya kitaifa
tutakuwa na kamati yenye members watatu tu. M1 ndiye atakayekuwa
anawasiliana na tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika Mkuu). Tumepanga
kwamba kusiwe na mawasiliano mengi kati ya kamati na mhusika mkuu
kuepuka tracking ya wapinzani wetu. M1 ni mtu wa karibu na MM kwa hiyo
mawasiliano yao hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata
wangewasiliana mara nyingi kiasi gani. Hata hivyo, linapokuja suala la
mkakati huu tunasihi mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa
simu na si sms. M1 ndiye atakayewasilisha mambo yote yanayotoka kwenye
kamati ya kitaifa na endapo kuna haja ya MM kukutana na kamati ya
kitaifa, mipango yote ya kikao itafanywa na M1 kwa usiri mkubwa. M2 ni
mtu ambaye yuko kwenye ofisi kuu za taasisi yetu wakati M3 ndiye
mchapaji wa mkakati huu.
Kamati hii imefanywa kuwa na members wachache sana wenye uelewa mpana wa
mambo na wenye elimu nzuri ili kuhakikisha kazi inafanyika kitaalam na
kwa uhakika sana. Kamati ya kitaifa itapeleka mapendekezo yake kwaMM na
yeye pia ataleta ushauri wake kwa kamati kama mishale inavyoonyesha.
Chini ya kamati ya kitaifa kutakuwepo waratibu wa kanda zote kumi
watakaojulikana kama MK1 – MK10. Hawa watatafutwa na kusimikwa na kamati
ya kitaifa kwa kushauriana na MM kwa utaratibu utakaokubalika na pande
zote yaani MM na kamati ya kitaifa. Chini ya waratibu wa kanda
kutakuwapo waratibu wa mikoa yote 30 (MMK1 – MMK30) ambao watapatikana
kwa utaratibu ule ule wa kuwapata waratibu wa kanda. Isipokuwa pale
ambapo inakuwa ngumu, itabidi kamati ya taifa isaidiane na waratibu wa
kanda kuwapata waratibu wa mikoa lakini kamati itashauriana na MM kabla
ya kuwasimika rasmi hao waratibu wa mikoa.Mtandao utakuwa kama
inavyoonyeshwa kwenye mchoro ufuatao:
NAMNA YA KUFANIKISHA MKAKATI:
Kazi itagawanywa katika awamu tatu:
Awamu ya kwanza ni kuanzia sasa mpaka uchaguzi wa ngazi ya matawi
utakapoanza. Katika awamu hii kazi ni kuhakikisha kwamba mtandao mzima
umekamilika mpaka kwenye ngazi ya mkoa. Kazi nyingine itakayofanyika ni
kwa waratibu wa mikoa kuendelea kuspot makada kwenye wilaya na mikoa
ambao tayari wana mtazamo tulio nao ama ambao wanaweza kuingiziwa
kirahisi mbegu hii ya mabadiliko na wakawa tayari na wana uwezo na sifa
za kushinda uongozi kwenye wilaya na mikoa yao bila kusahau sifa ya kuwa
waaminifu wenye uwezo wa kutunza siri. Kulingana na muda hii ni kazi
inayotakiwa kufanyika sasa lakini kwa uangalifu mkubwa. Ni muhimu
kukumbushana hapa kwamba katika awamu hii hakuna anayetakiwa kujua
mpango mzima zaidi ya kamati ya kitaifa na MMili kuhakikisha uwezekano
wa mkakati wetu mapema kwa wapinzani wetu unakuwa minimized to almost
zero.
Awamu ya pili ni kipindi kuanzia uchaguzi wa matawi mpaka uchaguzi wa
mikoa unapokamilika. Katika awamu hii tutasaidiana na waratibu wa kanda
na mikoa kuhakikisha makada tuliowaspot kwenye wilaya wanapanga safu zao
kwenye kata ili kuhakikisha watakaochaguliwa kwenye kata ni watu wao
ili waje wawachague kwenye wilaya.Vivyo hivyo kwa makada tuliowaspot
kwenye mikoa wahakikishe wanaochaguliwa kwenye wilaya ni wale makada
wetu ili nao waje wawachague kwenye mikoa yao. Hapa ndipo kwenye kazi
kubwa ya mkakati wetu na hapa ndipo tutakapohitaji kuingia gharama zaidi
kwa ajili ya kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa asilimia angalau
80.
Awamu ya tatu ni kuanzia baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa mikoa hadi
uchaguzi wa kitaifa utakapoitishwa. Katika kipindi hiki kwa ustadi
mkubwa tutakuwa tukiwaandaa makada wetu waliochaguliwa tayari kuja
kufanya mabadiliko makubwa kitaifa. Ni wakati huu ambapo tutawaingizia
mkakati taratibu lakini kwa ustadi mkubwa tukijikita hasa kwenye
kuonyesha kwa nini tunahitaji mabadiliko. Ni katika kipindi hiki ambapo
kwa ustadi mkubwa tunaweza kuwaspot wale waliochaguliwa ambao
hatukuwaandaa na kuwaingizia pia mbegu ya mabadiliko ili kuwawin na
kuwarecruit kwenye mkakati.
Aidha katika awamu zote tatu kazi ya kuianalyze ofisi kuu itakuwa non
stop kwa kuzingatia kwamba mabadiliko ya wakurugenzi na maofisa yatakuwa
yanatokea na watu nao watakuwa wanabadilika kimtazamo. Analysis ya
ofisi kuu ni kuhakikisha tunajua nani na nani wako na sisi na nani na
nani wako against na pia nani na nani wanaweza kupandikiziwa mbegu kwa
ustadi na wakaungana nasi.
MAHITAJI YA KUFANIKISHA MKAKATI:
Raslimali watu. Tunahitaji watu waaminifu watatu kwenye ngazi ya kitaifa
ambao tayari wapo. Tunahitaji watu waaminifu kumi kwenye kanda ambao
tutawatafuta na pia waaminifu wengine 30 kwenye mikoa yote thelathini.
Fedha. Tunahitaji fedha kwa ajili ya mawasiliano kati ya wanakamati na
wale wa ngazi ya chini. Aidha tunahitaji fedha kwa ajili ya gharama za
usafiri pale tutakapohitaji kwenda kwenye kanda na mikoa husika kwa
ajili ya kusimika watu hao tunaowahitaji.
MAPENDEKEZO MAHSUSI NA HITIMISHO:
Katika kuhitimisha tunapendekeza mambo mahsusi yafuatayo:
Kuhusu Bajeti:
Tunapendekeza kwamba bajeti ya mkakati huu isipangwe hivi sasa. Ni
muhimu tu sote kuelewa kwamba wakati wenzetu wanatumia raslimali za
taasisi kujijenga na kutekeleza mkakati wao wa ushindi, sisi tunapaswa
kuingia mifukoni. Kwa kila kila mmoja wetu atakuwa budget conscious ili
kuepuka matumizi makubwa ya pesa. Hata hivyo, kwa kuzingatia kwamba
lazima pesa inahitajika ni muhimu M1 na MM kujaribu kuangalia namna ya
kuraise pesa na kushauri. Otherwise, tutakapokuwa tunahitaji kufanya
hatua yoyote ama jambo lolote tutakuwa ndo tunapiga hesabu za funds
tunazohitaji kwa jambo husika na kuingia katika utekelezaji.
Kuhusu mwenendo wa MM kuanzia sasa:
Ni maoni yetu pia kwamba kuanzia sasa MM aenende katika mwenendo ambao
utarahisisha ushindi. Mfano tunapendekeza afanye yafuatayo kuanzia sasa:
Apunguze ukaribu na viongozi wa serikali na wa chama tawala na awe crical zaidi na utendaji wa serikali nje na ndani ya bunge.
Ashiriki kikamilifu katika shughuli za taasisi yetu zikiwamo vikao vyote vinavyomhusu, operesheni mbalimbali, chaguzi ndogo, nk.
Aendelee kushusha ‘nondo’ ndani ya chombo chetu cha uwakilishi na
kuendelea kuwa juu ya wawakilishi wengine katika hoja mbalimbali zenye
maslahi ya kitaifa.
Ajitahidi kudhibiti jazba hata pale anapokuwa amebambikiziwa tuhuma
nzito namna gani. Atulie, ashauriane na wazee ili kuona namna nzuri ya
kujibu tuhuma zinazomkera. Tukumbuke kwamba wakati mwingine kukaa kimya
ni jibu zuri zaidi kuliko hoja nzito.
Sambamba na ‘iv’ hapo juu, adhibiti sana emotion ili kuhakikisha kila
kitu kinachofanywa ama kuzungumzwa kinachomgusa asikimbilie kuongea na
vyombo vya habari ama kwenye mitandao ya kijamii bali afuate kile
tulichokizungumza kwenye kipengele cha ‘iv’ hapo juu.
Kuhusu mapambano ya kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii:
Katika hili sisi hatukuona haja ya kufanya hivyo kwa sababu mbili:
Imani yetu kwamba taasisi yetu ni kubwa kuliko watu kwa hiyo ni muhimu
kuzingatia kwamba hatuiui taasisi katika mapambano haya. Tukiendekeza
mashambulizi kwa njia ya mitandao ya kijamii hatutakuwa na ngao ya
kuwakinga watu wa kawaida (wanataasisi na wasio wanataasisi) dhidi ya
kujikuta wakiamini kwamba taasisi hii nayo haina jipya ni sawa tu na ile
tunayotaka kuitoa.
Tutakuwa tumeiua taasisi na mkakati huu hautakuwa na maana sana kama
lengo ni kufanya mabadiliko ya uongozi wa taasisi tu lakini malengo ya
taasisi ya mwaka 2015 yasitimie!
Kujikita kwenye mashambulizi kupitia mitandao ni kuzidi kuwashtua wakuu
waliopo kwamba bado tuko serious na mkakati wa kuwatoa na kuwafanya
wafanye kazi zaidi huku wakiendelea kumpaka matope MM kwamba ndiye
anayerusha makombora hayo kwenye mitandao kwa kusudi la kuhujumu taasisi
maana hiyo ndo lugha yao. Hatukatai kwamba wakuu wanajua kabisa kwamba
bado MM ana nia ya kumvaa mkuu aliyepo lakini tunajua kwamba kwa sasa
wanaamini wamemdhoofisha na hana madhara tena. Ndiyo maana tunataka
kutekeleza mkakati wetu kwa siri sana ili wafikiri MM amekata tamaa
kumbe ndo anakuja na mkakati mzito zaidi.
Hata hivyo, ni muhimu kukumbushana kwamba wenzetu hawatanyamaza kwa
sababu eti sisi tumeacha kuwashambulia kwenye mitandao ya kijamii.
Lazima wataendelea! Wataendelea kumchafua MM kwa kupitia wapuuzi kama
yule kichaa wa ‘ars’ na kundi lake. Nini tutakuwa tunakifanya sasa?
Tutahakikisha tuko busy kupost mambo mema na mazuri yatakayokuwa
yakifanywa na MM kila wakati na kuzidi kusambaza sifa zake njema kila
inapotokea nafasi. Atakayefanya kazi hiyo ni sisi wengine wala si yeye!
Pia tutahakikisha kila post ya kumchafua inapatiwa majibu bila kutumia
ID yake inayojulikana. Ni vema aidha akatupatia majibu na sisi kuyapost
ama afungue ID mpya kabisa ambazo hazijawahi kuwepo kwenye mitandao
halafu ndo awe anazitumia kujibu lakini kwa kuzingatia
tuliyokwishayazungumza hapo juu yaani kutofanya kwa emotion na kuepuka
jazba lakini pia kushauriana na watu wa karibu kabla ya kutoa majibu kwa
jambo lolote linalomhusu.
Kuhusu kamati ya kitaifa (hususan M2 & M3):
Tulikubaliana kwa kauli moja kwamba katika kutekeleza mkakati huu
tunahitaji members hawa wawe wametulia kimaisha. Inakuwa vigumu kwa
mfano kumtaka member aende mahali fulani kwa makusudi ya mkakati huu
wakati hajui familia yake nyumbani anaiacha inakula nini. Tuliona kwamba
M3 tayari hana kazi kwa sasa tena kwa kufanyiziwa na wakuu waliopo. Ni
katika mwendelezo huo huo tunamwona M2 naye akiwa ukingoni kupigwa nje
na kuachwa mtupu na wakuu waliopo katika kile wanachokiita wao reshuffle
ya ofisi kuu. Kwa sababu hiyo tukapendekeza kwamba MM kwa kushirikiana
na M1 kwa hatua ya kwanza wanaweza kutafuta kiasi cha sh. 2m kila mmoja
tukijua kwamba kama members hawa wawili wakisaidiwa milioni mbili mbili
wanaweza kuanzisha projects ambazo zitawasustain hata kama hawana ajira.
Kwa hatua ya baadaye tutasaidiana kuona kama hawa members wanaweza
kusecure good employments mahali, provided hazitawazuia kufanya siasa.
No comments:
Post a Comment