AU yashindwa kuchagua mwenyekiti wa Tume
30 Januari, 2012 - Saa 19:19 GMT
Umoja wa Afrika umeshindwa kuchagua mwenyekiti mpya wa tume ya umoja huo licha ya duru tatu za upigaji kura mjini Adis Ababa.
Baada ya kupiga kura mara tatu, hakupatikana
mshindi wa moja kwa moja kati ya wagombea wawili, mwenyekiti wa sasa
Jean Ping kutoka Gabon na waziri wa mambo ya ndani wa Afrika Kusini
Nkosazana Dlamini Zuma.Sasa uchaguzi wa mweneykiti mpya wa Tume ya AU umeahirishwa hadi mkutano unaofuata, utakaofanyika nchini Malawi mwezi Julai.
Baada ya kushindwa kupata mshindi, viongozi wa Afrika waliafikiana Bwana Ping aendelee kama mwenyekiti hadi wakati hio.
Awali taarifa zilielezea kwamba naibu mwenyekiti Erastus Mwencha kutoka Kenya ndiye angeshikilia wadhifa huo hadi uchaguzi utakapofanyika.
Bi Zuma ambaye ni mke wa zamani wa Rais Jacob Zuma, na mmoja wa mawaziri waliohudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Afrika Kusini aligombea kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza kamati hiyo kuu ya Umoja wa Afrika, ambao una wanachama 54.
Bw Ping ambaye amekuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika tangu 2008 alikuwa anagombea kwa muhula wa pili.
Mwandishi wa BBC Noel Mwakugu anasema Bw Ping alikabiliwa na upinzani baada ya kushtumiwa na viongozi wa Afrika kwa kushirikiana na Ufaransa katika kumng'atua madarakani Rais wa Libya Muammar Gaddaffi.
Mwandishi huyo anasema kulikuwa na malalamiko kwamba Bw Ping hakuunga mkono mpango wa Umoja wa Afrika wa kukomesha ghasia nchini Libya, na pia ujumbe wa mapatanisho ulioongozwa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.
Shirika la Nato na waliokuwa waasi nchini Libya walikataa mpango huo wa AU, kwa kuwa haukumtaka Rais Gaddaffi kuondoka madarakani.
No comments:
Post a Comment