Mkuu wa majeshi Burundi akemea wanasiasa
- 3 Mei 2015
Mkuu
wa majeshi nchini Burundi Meja Jenerali Prime Niyongabo ametoa wito kwa
wanasiasa kutotumia jeshi la taifa kwa manufaa yao ya kisiasa.
Jenerali
Niyongabo amekariri tangazo lililotolewa na waziri wa ulinzi Jumamosi
kuwa jeshi la nchi hiyo litahakikisha kuwa mkataba wa Arusha
umetekelezwa kikamilifu na kuwa jeshi hilo halitumiwi na mtu au chama
chochote cha kisiasa.Kuhusiana na maandamano yanayoendelea, mkuu huyo wa jeshi amesema kuwa maandamano hayo sio halali na wanaichi wanapaswa kutumia mbinu za sheria zilizopo kutatua mizozo yao.
Wakati huo huo Meja Jenerali Niyongabo amesema jeshi hilo litasalia kuwa lenye nidhamu ya hali ya juu na tiifu kwa taifa la Burundi na wala sio kwa mwanasiasa yeyote.
Ameongeza kusema kufikia sasa jeshi limefanya kazi nzuri kuhakikisha kuwepo kwa usalama nchini Burundi na katika mataifa mengine wanakohudumu katika vikosi vya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika.
Mkuu huyo wa majeshi amesema wanajeshi wataendelea kushirikiana na polisi kushika doria ili kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo nchini Burundi.
Huku hayo yakijitokeza muungano wa upinzani umesema kuwa maandamano yataendelea siku ya Jumatatu baada ya mapunziko ya siku mbili.
Upinzani umepinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza ya kuwania muhula wa tatu kama rais.
No comments:
Post a Comment